Header Ads

WAISLAMU TULIENI,HUKUMU YA CCM 2010

Happiness Katabazi

JUMANNE wiki hii, serikali kupitia Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, ilitangaza kutounda Mahakama ya Kadhi na badala yake itatafsiri sheria za Kiislamu na kuzijumuisha kwenye sheria za nchi ili zitumike kwenye mahakama ya kawaida nchini.


Chikawe alisema uamuzi huo wa serikali, unatokana na mapendekezo yaliyowasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na tume ya wataalamu waliochambua mapendekezo ya utafiti uliofanywa na Kamati ya Kurekebisha Sheria.

Kwanza Watanzania tujikumbushe; wakati serikali ikitangaza msimamo huo, ni Chama Cha Mapinduzi(CCM) kwa mujibu wa ilani yake ya 2005-2010 iliahidi kuwaletea Mahakama ya Kadhi Waislamu.

Ni ukweli usiopingika kwamba CCM ilidandia ahadi ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kwa ajili ya kujipatia umaarufu na kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, wakati ikijua wazi isingeweze kutekeleza ahadi hiyo.

Kwa hiyo hata kwenye hoja ya Tanzania kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislam(OIC), pia serikali yetu inajua wazi kabisa haiwezi kuingia katika jumuia hiyo; ila inaendelea kuwahadaa Watanzania na kuwafanyia mchezo wa danganya toto!

Kwa hiyo Waislam wameliwa na katika hilo ilikuwa ni siasa tu. Ahadi hiyo ni sawa na ile nyingine ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania” tuliyoahidiwa na CCM lakini hadi hii leo imebaki kwa watu fulani. Maisha bora yameyeyuka kama theluji ya mlima Kilimanjaro.

Binafsi naweza kusema CCM si wakweli, kwani kwa kawaida chama chochote ambacho ni makini pale kinapotoa ahadi lazima kiitekeleza baada ya kukamata dola.

Nawasihi ndugu zangu Waislaam kwamba wakati wa kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao wawe makini kwa kuchagua chama makini kuliko kugeuzwa wanasesere.

Serikali yetu haishughuliki na mambo ya kiibada, kwani Ibara ya 19 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977,inaikataza.

Kwa hiyo serikali kama serikali kufikiria itachukua sheria za Kiislam na kuzitafsri na kuzijumuisha kwenye sheria za nchi , ni ‘uongo’ uliokubuhu.

Ila Waislam wanaoitaka Mahakama ya Kadhi watajua jinsi ya kuiadhibu serikali na CCM.Siyo siri Serikali ya Awamu ya Nne imejijengea sifa mbaya ya kutoa baadhi ya viongozi wakuu kutoa matamko na ahadi za uongo bila aibu.

Inasikitisha serikali kuwa na sifa kama hii kwani watoto wetu wanaona hali hiyo hivyo mwisho wa siku nao watakuwa viongozi; watarithi porojo kama hizi.

Lakini jambo la kushukuru Mungu baadhi ya wananchi wameishaanza kugundua tabia hiyo ya viongozi na kwa upande wa baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakienda ibada za kuliombea taifa hili ili lisije likatumbukia kwenye machafuko yasiyo ya lazima.

Hivyo wananchi watambue lengo la CCM ni kung’ang’ania kubaki madarakani na siyo kuiletea nchi yetu maendeleo ya kweli na uhakika kama tunavyotamani iwe.

CCM siyo chama cha kuaminika tena.Kwanza Rais Jakaya Kikwete ni Muislamu na alizunguka nchini nzima kunadi ilani ya chama chake na kuahidi angeliingia madarakani angelianzisha mahakama hiyo.

Hivyo namuonea huruma kwani kwa msimamo huo wa serikali uliotolewa na Waziri Chikawe, umethibitisha pasipo shaka kwamba Rais Kikwete na chama chake walikuwa wanatambua kinachoendelea.

Katika hili Waislam waelewe hakuna mtu anapinga wao kufurahia uhuru wa dini yao vile vile wajue uhuru huo umepewa mipaka katika Katiba ya nchi, kwa hiyo wawe makini na aina hii ya wanasiasa.

Kama ni siasa, ni vizuri Waislam wachunguze kwa kina katiba na sera za vyama vyote kabla hawajaanza kupiga kula zao hovyohovyo.

Katika hili , ilani ya CCM iliandaliwa kiujanjaunjanja ili chama hicho kikiingia madarakani baada ya hapo kila mtu abebe mzigo wake.lakini hukumu ya hao waliyowadanganya inatoka mwaka kesho wakati watakapopita kuwaomba muwapigie kura tena.

Mungu Ibariki Tanzania,Mungu Ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Julai 5,2009

No comments:

Powered by Blogger.