Header Ads

WATUHUMIWA WA PEMBE ZA NDOVU WATINGA MAHAKAMANI

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE vigogo sita wa makampuni binafsi ya kupakia na kusafirisha mizigo nchini, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi za uhujumu uchumi, kwa kusafirisha nje ya nchi jumla ya kilo 11,061 za pembe za ndovu zenye thamani ya sh 791,514,020 kinyume cha sheria.


Mbele ya Hakimu Mkazi Anisetha Wambura, Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila, aliyekuwa akisaidiana na Michael Lwena, Shadrack Kimaro na Abubakar Mrisha, alidai kuwa kesi hiyo inamkabili Eladius Colonerio (39) ambaye ni Mkurugenzi wa Team Freight (T) Ltd, Gabriel Balua (33), Meneja Usafirishaji wa nje na ndani ya nchi wa kampuni hiyo, na Shaban Yabulula (44) ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kigoma M. N Enterprises (T) Ltd.

Wakili wa Mwangamila, alidai kuwa washitakiwa hao katika kesi hiyo namba Na. 3 ya mwaka huu, wanakabiliwa na mashitaka 11.

Alisema shitaka la kwanza ni kula njama, ambapo kati ya Desemba 22 mwaka jana na Januari 15 mwaka huu, jijini Dar es Salaam, washitakiwa kinyume cha sheria, walisafirisha kiasi cha kilo 9,578 za meno ya tembo kwenda Hai Pong, Vietnam, na Manilla Philippiness, zenye thamani ya sh 684,827,000 mali ya Serikali ya Tanzania.
Mwangamila alidai shitaka la pili ni uwindaji haramu kinyume na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2002.

Katika shitaka hilo, alidai kuwa washitakiwa katika muda usiofahamika, ndani ya eneo la hifadhi linalolindwa na sheria hiyo, waliwinda tembo waliowahamisha kwenye jedwali bila kibali halali.

Aidha, alidai mashitaka mengine ni kujihusisha na biashara ya nyara za serikali, kusafirisha nyara nje ya nchi, kumiliki nyara hizo, na kushindwa kutoa taarifa za umiliki kwa ofisa wanyamapori.

Mwangamilia alidai shitaka la nane ni kuwasilisha hati za uongo, ambapo Desemba 2008 hadi Januari 2009 katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa makusudi na kwa lengo la kudanganya, washitakiwa waliwasilisha hati za kuomba kusafirisha mizigo kwenye meli yenye Na. DAR001793 ya Desemba 22 mwaka jana.

Hati nyingine za uongo zilizowasilishwa na washitakiwa hao ni Bill of Lading Na. DAR 002348/1 na DAR 002348, tamko Na. DAR 002347 iliyotolewa na CMA CGM (T) Ltd na tamko la Ushuru wa Forodha lenye namba za usajili R 93832 ya Desemba 23, mwaka jana kwa kontena Na. ECMU 1721884 na ECMU 1642240, lililosafirishwa kwenye bandari ya Hai Phong, Vietnam na Manilla, Phillippiness.

Shitaka la tisa alidai ni kusafirisha nje ya nchi bidhaa zilizozuiliwa na kukatazwa na Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Afrika Mashariki Na. 1 ya mwaka 2004.
Katika muda huo ndani ya Bandari ya Dar es Salaam, washitakiwa wanadaiwa kusafirisha nje ya nchi pembe za ndovu kinyume cha sheria.

Wakili huyo machachari, alidai shitaka la kumi ni kusafirisha nje ya nchi mali iliyofichwa kinyume cha sheria hiyo ya ushuru wa forodha, ikiwa ni pamoja na kusafirisha pembe hizo za ndovu kinyume cha sheria, huku wakidanganya kuwa ni mabaki ya plastiki kwenda Vietnam.

Katika shitaka la mwisho, washitakiwa walidaiwa kutengeneza au kutumia nyaraka za uongo za ushuru wa forodha kinyume cha Sheria ya Ushuru wa Forodha.

Hata hivyo, washitakiwa hao walipewa ruhusa kujibu tuhuma zinazowakabili katika shitaka la kwanza, saba, nane, tisa, 10, 11, kwa sababu mashitaka hayo hayaangukii katika Sheria ya Uhujumu Uchumi, ambapo walikana mashitaka hayo.
Mwangamila alidai upelelezi bado haujakamilika na kueleza kuwa shitaka la pili, tatu, nne, tano na sita ni makosa ya uhujumu uchumi hivyo, washitakiwa hawakupaswa kusema chochote kuhusu mashitaka hayo kwa sababu, dhamana ya mashitaka hayo, hushughulikiwa na Mahakama Kuu na si mahakama hiyo.
“Mheshimiwa hakimu, kifungu cha 29(4)(a) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi kama ilivyofanyiwa mapitio 2002, kinatamka wazi kabisa Mahakama ya Hakimu Mkazi itatoa dhamana kwa kesi ya mali au fedha isiyozidi sh milioni 10, lakini katika kesi hii, kiwango hicho kimezidi hivyo tayari sheria hiyo imeifunga mikono mahakama hii na hivyo haiwezi kutoa dhamana kwa washitakiwa,” alisema Mwangamila.
Hoja hiyo ilipingwa na wakili wa utetezi, Juma Nassor ambaye alisema makosa yanayowakabili washitakiwa yanadhaminika na kuomba mahakama ipuuze madai ya serikali.
Hata hivyo, Hakimu Wambura, alisema hawezi kutoa maamuzi kuhusu malumbano hayo ya kisheria kwa sababu anahitaji muda wa kwenda kuzipitia hoja hizo.
Wambura aliiahirisha kesi hiyo hadi Agosti 6, ambapo atakuja kutoa uamuzi wa kama dhamana ipo au haipo kwa washitakiwa hao.

Wakati huo huo, mbele ya Hakimu Mkazi Mohamed Mchengelwa, Wakili wa Serikali, Abubakar Mrisha aliwataja washitakiwa watano kuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi Na. 4 ya mwaka huu.

Katika kesi hiyo washitakiwa wanadaiwa kusafirisha pembe za ndovu kiasi cha kilo 1,483, zenye thamani ya sh 106,687,020 kwenda Manila, Phillippines kinyume cha sheria.

Wakili Mrisha aliwataja washitakiwa hao ambao pia ni wakurugenzi wa kampuni za kupakia na kusafirisha mizigo, kuwa ni Nebart Kiwale (45) ambaye ni Mkurugenzi wa Uplands Freight Forwarders (T) Ltd, Gabrile Balua (33) wa Team Freight, Issa Lweno (40) wa Uplands Freight Forwarders, Eladius Colonerio (39), Mkurugenzi wa Team Freight (T) Ltd na Abubakar Hassan (38).

Hata hivyo, washitakiwa hao walikana baadhi ya mashitaka yaliyo kinyume na sheria ya ushuru wa forodha na kanuni ya adhabu, isipokuwa hawakutakiwa kusema chochote kwenye makosa ya sheria ya uhujumu uchumi.

Wakili wa serikali Mrisha, naye alidai upelelezi bado haujakamilika na Hakimu Mchengelwa aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 28, atakapotoa uamuzi kuhusu washitakiwa wapewe au wasipewe dhamana na mahakama hiyo.

Kufikishwa kwa washitakiwa hao jana, kumefanya washitakiwa waliokamatwa na pembe za ndovu jijini Dar es Salaam, kufikia kumi sasa.

Wiki mbili zilizopita, mahakamani hapo walifikishwa watuhumiwa wanne, mmoja akiwa raia wa China, waliokamatwa na pembe za ndovu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, wakizisafirisha nje ya nchi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 22,2009

No comments:

Powered by Blogger.