Header Ads

USIKILIZWAJI KESI YA MRAMBA WAKWAMA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, ilishindwa kuendelea kusikiliza maelezo ya awali ya kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake, kwasababu kompyuta inayorekodi mwenendo wa kesi hiyo kupata tatizo la kiufundi.


Washitakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.

Kiongozi wa jopo la kesi hilo John Utamwa anayesaidiana na Sam Rumanyika na Saul Kinemela jana saa 8:58 baada ya kutoka mapumziko ya dakika 15 mahakamani hapo, alisema jopo hilo limelazimika kusitisha kuendelea kusikiliza maelezo ya awali kwakuwa mtaalamu wa kompyuta huyo amewaeleza kompyuta hiyo imepata hitirafu.

Utamwa alisema kimsingi kesi hiyo hawezi kuendelea bila ya kuwepo kwa kifaa hicho hivyo akautaka upande wa mashitaka kusitisha kuendelea kusoma maelezo hayo ya awali hadi Septemba 16-25 mwaka huu na kuongeza kuwa kesi hiyo itakuja kutajwa Agosti 31 mwaka huu, kwakuwa sheria inataka kesi itajwe ndani ya siku 30.

Aidha alikubali maombi ya washtakiwa wote ya kutoka nje ya Dar es Salaam yaliyowalishwa na mawakili wao Hurbet Nyange,Joseph Thadayo na Profesa Leonard Shaidi.

Mapema saa tano asubuhi hadi saa 7:30 mchana, Wakili Kiongozi wa serikali Stanslaus Boniface aliyekuwa akisaidiana na Fredrick Manyanda, Tabu Mzee, Beni Lincon alianza kusoma maelezo ya awali dhidi ya washitakiwa lakini hata hivyo alishindwa kumaliza kusoma maelezo hayo kwasababu ya kompyuta kuaribika.

Boniface alidai kuwa washitakiwa wote walikuwa ni watumishi wa wa umma wenye nyadhifa za juu serikalini, na kwamba kati ya 2000-2005 Mramba alikuwa Waziri wa Fedha, na kati ya 2002-2005 Yona alikuwa Waziri wa Nishati na Madini na kuwa 2002-2008 Mgonja alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha.

“Hivyo washitakiwa walipaswa kufanyakazi zao kwa uadilifu na kwa misingi ya sheria”alidai Boniface.

Akiendelea kueleza kupitia dokezo la Machi 2003 lenye kumbukumbu Na.CDA 111/338/01 ,mshitakiwa wapili(Yona) aliomba ridhaa ya Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa kupitia barua yenye Na.SHC/PP.340/P ya Machi 20 ya 2003 la kuletwa mkaguzi huru wa dhahabu.

Lakini barua ya Septemba 11 ya 2002 na Desemba 15 mwaka huo huo, iliyoandikiwa na Katibu Mkuu ofisi ya rais, Mrindoko na Kaimu Mkuu wa kitengo cha Sheria G.M.Nyelo ilikataa ombi la Yona na zikamtaka aheshimuwa sheria kwasababu mchakato uliotumika kumpata mkaguzi huru ni batiri na usitishwe na kumtaka watumie mahabara ya SEAMIC kutafiti jambo hilo kwa gharama kidogo.

Aidha mshitakiwa wa pili alishauriwa na Kamishna wa Madini G.L Mwakalukwa kuptia barua yake Na.CDA 111/338/01 ya Machi 21 2003 kwamba pafanyike uteuzi Assayers Licensing Board kwaajili ya upatikanaji ushauri kutoka Commonwealth Sekretarieti kuangalia jinsi ya kupunguzwa kwa gharama za kuingia mkataba na Alex Stewart (Assayers).

“Lakini Mei 11 ya 2003,Yona aliandika barua kwa rais Mkapa yenye kumbukumbu Na.CDA/11/338/01-M.100/5 aliomuomba rais airuhusu wizara ya Fedha na Benki Kuu zigharamie Golg Asseyers na rais alimjibu ombi hilo kupitia barua SHC/PP.340/Q ya Mei 13 ya 2003, ambayo alikataa ombi la Yona.”alidai Boniface.

Aidha aliendelea kueleza kuwa Mei 15,2003 Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha wakati huo, Abdisalaam Khatibu alimjulisha Yona kupitia barua Na.TYC/M/30/2 maazimio ya kikao kati ya Think Tank ya Wizara ya Fedha na Tax Review Committee ni kwamba uchunguzi zaidi ufanyike kuhuusu kuajili Gold Asseyers na akamshauri asitishe mchakato msima wa kumpata mkaguzi huyo goldi..

Alidai licha ya kupewa taarifa hizo, Yona alipuuza na Mei 20, 2003 ,kupitia barua yake yenye kumbukumbu Na.111/338/01.Na kuwa mshitakiwa wa tatu(Mgonja) naye pia alipuuza maazimio yaliyotolewa na Sekretarieti ya Commonwealth katika barua yake Na.5106/P/58 ya Mei 21 ya 2003.

Aidha washitakiwa kupitia mawakili wao walikubaliana na barua hizo na madokezo kuwa yapokelewe na mahakama ili zijekutumika kama vielelezo vya upande wa mashitaka wakati kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa na hivyo kufanya jopo hilo jana kupokea jumla ya vielezo saba.

Washitakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo mwishoni mwa mwaka jana, wakikabiliwa na makosa mawili ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kisababishia serikali hasara ya sh .bilioni 11.7, kwa kukudharau mapendekezo ya TRA yaliyokataza kampuni ya Alex Stewart isipewe msamaha wa kodi lakini washitakiwa hao walikaidi mapendekezo hayo na kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Agosti mosi, 2009

No comments:

Powered by Blogger.