Header Ads

KORTI YAWAPA DHAMANA WAVUVI HARAMU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imetupilia mbali pingamizi la serikali katika kesi ya uvuvi haramu inayowakabili raia 32 wa kigeni waliokamatwa kwenye meli ya Tawariq 1,lilokuwa likiiomba mahakama hiyo isipokee ripoti ya tathimi ya meli hiyo kwasababu ripoti hiyo ni ya uongo.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Waliarwande Lema, ambaye alianza kwa kusema kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya yeye kutoa uamuzi kuhusu malumbano ya kisheria yaliyoibuka Ijumaa iliyopita kuhusu ripoti ya tathimini ya meli hiyo.

Hakimu Lema alisema baada ya kupitia kwa kina malumbano hayo ya hoja za kisheria, amefikia uamuzi wa kutupilia mbali ombi la upande wa mashitaka lilokuwa likitaka mahakama hiyo isipokee ripoti hiyo kwasababu amebaini halina msingi.

Alisema mahakama hiyo ilichokuwa ikikitaka ni katika ripoti hiyo ni tathimini na si dosari za uandaaji wa ripoti kama inavyodaiwa na upande wa mashitaka na kuongeza kuwa ripoti hiyo imeiwezesha mahakama hiyo kufikia uamuzi wa kutoa dhamana kwa washitakiwa hao ambao wamesota rumande kwa miezi mitano sasa.

Lema alisema kwa mujibu wa ripoti hiyo ya tathimini iliyofanywa na Dar es Salaam Marine Instute, endapo meli hiyo itauzwa kwenye soko nchini India ni dola 280,000 na katika soko la hapa nchini ni dola 122,000.

‘Pingamizi hilo la serikali kwamba ripoti hiyo ina dosari nyingi na kwamba ni ya uongo, mahakama hii imeliona halina msingi kabisa kwasababu mahakama hii ilichokuwa ikiitaji ni tathimini ya meli ili iweze kutoa dhamana kwa washitakiwa na tathimini hiyo imeainishwa kwenye ripoti hii, hivyo ripoti hii ndiyo imeiwezesha mahakama hii leo (jana) imeifikisha mahakama hii kutoa masharti ya dhamana kwa washitakiwa.”alisema Lema na kufanya mawakili wa serikali kujiinamia.

Akitoa masharti ya dhamana alisema meli hiyo na samaki ambao wanathamani ya sh bilioni 2.7, vitadhaminiwa kwa bondi ya dola za kimarekani 250,000, kila mshitakiwa anadhaminiwa na wadhamini wawili wanaotambulika na ofisi za balozi ambapo wadhamini hao wawili watasaini bondi ya dola 25,000.

Hata hivyo washitakiwa hao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana hiyo jana na walirejeshwa rumande hadi Agosti 5 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Ijumaa iliyopita, wakili wa serikali Deo Nangela na Mganga Biswalo, walitumia saa moja na nusu kuichambua ripoti hiyo na kuishawishi mahakama isiipokee ripoti hiyo kwa kile walichokidai kuwa ina mapungufu mengi,ya uongo na kwamba haitaisaidia mahakama kufikia uamuzi wa kutoa dhamana kwa washitakiwa.

Naye wakili wa utetezi Ibrahimu Bendera aliyekuwa akisaidiana na Elias Nawela walipinga hoja hiyo na kudai kuwa ukweli unabaki pale pale kwamba upande wa mashita siyo wataalum wa masuala ya meli hivyo ni vyema wakaitwa wataalamu waliofanya tathimini na si vinginevyo na kusisitiza ripoti hiyo ni sahihi.

Washitakiwa hao ni mabaharia, Jiojwen Chang (34), Jia Yin Zhao 26), Gexi Zhao (36), Zongmin Ma (36), Dong Liu (25), Yongiao Fang (22), Nguyen Tuan(23), Hsu Sheng Pao (55), Zhao Hanquing (39), Zho Hanging (39) ambaye wote ni wakala na raia wa China.

Wengine ni Tran Van Phuon (33), Pham Dinn Suong (31), Tran Van Thanh (23), Cao Vuong (27), Kristofer Padilla (29) raia wa Vietnam. Wengine ni Mohamed Kiki (61), Anul Mani (24) raia wa Taiwani.

Aidha,washitakiwa wengine ni Jejen Priyana (22), Kuntoto Suratno (27), Tusi Ame (25), Ifan Herman Pandi (21), raia wa Indonesia, Silvano Garanes (32), Benjie Rosano (34), Ignacio Dacumos (31), Marlon Maronon (33), Jhoan Belano (34), Rolando Nacis (35) raia wa Philipins, Wakati Ali Ali Mkota (32), Juma Juma Kumu (40), Jackson Toya(39) raia wa Kenya.

Machi 10 mwaka huu, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka mawili, shitaka la kwanza ni kuvua samaki bila leseni kinyume na sheria ya Uvuvi wa Samaki katika kina kirefu ya mwaka 2009.

Alidai Machi 8 mwaka huu, washtakiwa wote kwa pamoja, saa sita usiku katika ukanda wa bahari ya Hindi ndani ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikamatwa wakiwa wakivua samaki bila leseni.Na washtakiwa wote walikana mashtaka na wapo rumande kwaajili ya wameshindwa kutimiza masharti dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Julai 23,2009

No comments:

Powered by Blogger.