Header Ads

LIYUMBA AFUNGUA KESI YA KIKATIBA

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania,Amatus Joachim Liyumba amefungua kesi ya Kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akiomba mahakama hiyo itamke kwamba kifungu 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 2002, kinapingana na Katiba ya Nchi.


Kesi hiyo ambayo imewasilishwa juzi na wakili wa Liyumba,Onesmo Kyauke tayari imeishapewa namba 36 ya mwaka huu. Na kwa mujibu wa hati hiyo, mdaiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 2002, kina mtaka mtuhumiwa anayedaiwa kuiba zaidi ya sh milioni kumi,atoe fedha taslimu au hati ya nusu ya mali anayotuhumiwa kuiba mahakamani ,ndipo apate dhamana.

Kwa mujibu wa hati ya madai ambayo Tanzania Daima ,imefanikiwa kupata nakala yake, Liyumba anaiomba mahakama hiyo itamke kifungu hicho kinapingana na Ibara ya 13(6)(b) ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977, inayotamka bayana kwamba mtu asichukuliwe kuwa ana hatia hadi pale mahakama itakapomkuta na hatia.

Aidha hati hiyo ya madai inadai kuwa kifungu hicho cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, pia kinapingana na Ibara 17(1) ya Katiba ya Nchi, ambapo ibara hii inatamka bayana kuwa kila mtu ana haki ya kuwa huru.

Liyumba anadai hatua ya mtuhumiwa kutakiwa kutoa fedha taslimu au nusu ya mali wakati bado hajatiwa hatiani na kesi inayomkabili, ni wazi mshitakiwa anakuwa ameishahukumiwa jambo alilodai linakwenda kinyume na Ibara ya 13(6)(b) ya Katiba ya Tanzania.

“Kwa sababu hizo tunaiomba mahakama hii,itamke kifungu hicho kuwa ni batili kwani kinakwenda kinyume na haki za msingi zilizoainishwa kwenye ibara hizo za Katiba ya nchi ambayo ndiyo sheria mama” ilisomeka hati hiyo.

Aidha Liyumba aliendelea kudai kuwa yeye kama Mtanzania ana haki ya kuwa huru kwa mujibu wa ibara hiyo, lakini hivi sasa ameshindwa kupata haki hiyo ya uhuru kwasababu kushindwa kuwasilisha fedha au hati ya nusu ya mali ya bilioni 110, mahakamani ili apate dhamana.

“Hivyo haki zangu kwa mujibu wa ibara hizo za Katiba zimenyang’anywa na kifungu hicho cha Sheria ya Mwenendo wa Janai, hivyo naiomba mahakama iliangalie na hilo wakati ikisikiliza kesi hii ya Kikatiba niliyofungua”.alidai Liyumba.

Julai 15 mwaka huu, Jaji Geofrey Shaidi, alitengua masharti ya kulegeza dhamana ya mshitakiwa huyo yaliyowekwa na Hakimu Mkazi Kisutu, Nyigulila Mwaseba yaliyotaka mshitakiwa huyo atoe fedha au hati ya nusu ya mali yenye jumla ya sh milioni 300, wadhamini wawili watakaosaini bondi y ash milioni 50, kusalimisha hati ya kusafiria, na kutotoka nje ya Dar es Salaam.

Jaji Shaidi akilisema anatengea alikubaliana na rufaa ya DPP-Eliezer Feleshi, na akatengua masharti hayo kwasababu hakimu Nyigulila alipotosha matakwa ya kifungu cha 148(5)(e) ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai 2002.Na badala yake akatamka masharti mapya na kumtaka mshitakiwa huyo atapata dhamana kwa kutoa fedha au hati ya nusu ya mali ya sh bilioni 110.

Mei 28 mwaka huu, Liyumba alifikishwa tena Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na kusomewa mashitaka mapya ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma chini ya kifungu 96(i) na kuisababishia serikali hasara serikali ya sh bilioni 221 kinyume na kifungu 284A(i) vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho 2002.

Liyumba ni mtumishi wa pili mstaafu wa serikali kufungua kesi ya aina hiyo, wa kwanza ni aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia,Profesa Costa Mahalu anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Kisutu, naye mwaka juzi, alifungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu, akitaka mahakama hiyo ifute moja ya kifungu cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, kinachomtaka mtuhumiwa kutoa fedha taslimu au nusu ya mali ndipo apate dhamana na kesi hiyo inaendelea.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima, Ijumaa, Julai 10, 2009

No comments:

Powered by Blogger.