Header Ads

KESI YA MENGI YAPIGWA KALENDA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilishindwa kuanza kusikiliza kesi ya kashfa ya madai ya shilingi moja iliyomkabili Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi kutokana na mawakili wa mlalamikaji, Yusuf Manji kutojiandaa.

Hakimu Aloyce Katemana alisema anakubaliana na hoja ya kuarishwa usikilizwaji wa kesi hiyo ambayo ilipangwa kuanza kusikilizwa jana. katika kesi hiyo Manji anawakilishwa na mawakili Mabere Marando, Beatus Malima, Dk. Ringo Tenga na Richard Rweyongeza.

“Nakubaliana na hoja ya mawakili wa mlalamikaji kwamba leo tusianze kusikiliza kesi hii hivyo naihairisha hadi Februali 3-4 mwaka huu, kwani licha ya mawakili hao kutojiandaa pia mimi ni mgeni na kesi hii na jalada lake bado sijalipitia,” alisema Hakimu Mkazi Katemana.

Awali akijibu hoja ya Wakili Marando ya kutaka kesi hiyo isianze kusikilizwa jana kwa madai upande wa madai haukuwa haujajiandaa, wakili wa Mengi, Michael Ngaro alielezwa kushangazwa na ombi hilo kwa sababu mawakili wa mlalamikaji ndiyo waliifungua kesi hiyo Na.85/2009 na kuhoji ni kwanini hawakuwa wamejiandaa.

“Sisi tunashangazwa na ombi la hawa wenzetu wa upande wa mlalamikaji la kutaka usikilizwaji usiendelee…sisi upande wa mdaiwa tupo tayari kuendelea na usikilizwaji wa kesi hii,”alisema Wakili Ngaro.

Mapema mwaka juzi, Yusuf Manji alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake kumkashifu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 19 mwaka 2011

1 comment:

Anonymous said...

hivi unajua wakili wa washtakiwa amemtaja Mh. Magufuli kuwa mmoja wa mashahidi watakaotoa ushahidi kuwatetea wavuvi hawa?

Powered by Blogger.