Header Ads

WANYAMBO WAWASILI DAR

Na Happiness Katabazi

UJUMBE wa watu 74 wa kabila la Wanyambo kutoka wilaya za Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera jana waliwasili jijini Dar es Salaam kwa ajili kushiriki tamasha la kitaifa la Wanyambo linaloanza Ijumaa wiki hii.


Katibu wa tamasha la Wanyambo taifa, Annamerry Bagenyi, alisema Wanyambo hao waliwasili jana saa 5:00 asubuhi katika Kijiji cha Makumbusho Kijitonyama na basi la RS Investment wakitokea Karagwe na walipokelewa na Wanyambo waishio hapa jijini, ambao pia walitoa burudani ya ngoma kwa waandishi wa habari.

Bagenyi alisema, ujumbe huo umejumuisha madiwani, maofisa wa serikali wa wilaya na mkoa wa Kagera, vikundi vya ngoma za Kinyambo na kuongeza kuwa ujumbe mwingine wa watu 60 unatarajiwa kuwasili leo ukitokea wilaya hizo ambazo ndiko wanakoishi watu wa asili ya kabila hilo hapa nchini.

Aidha alisema ujumbe huo umekuja na vitu vinavyotambulisha uasilia wa Mnyambo ambavyo vitatumika kwenye maonyesho ya tamasha hilo linaloanza Ijumaa na kumalizika Jumapili, ikiwa ni pamoja na mavazi, ngoma na vyakula.

Kila mwaka hapa nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii huteua kabila mmoja, kufanya tamasha la kuonyesha utamadani wake kwa niaba ya makabila mengine na kwa mwaka huu, Wanyambo wameteuliwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 19 mwaka 2011

No comments:

Powered by Blogger.