Header Ads

WANYAMBO WAMPIGIA MAGOTI NCHIMBI

Na Happiness Katabazi

WASANII wa vikundi vya ngoma za asili za kabila la Wanyambo wenyeji wa wilaya ya Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera wamemuomba Waziri wa Habari Utamaduni, Vijana na Michezo Emmanuel Nchimbi, kuwatafutia wafadhili ili waweze kuingia studio kurekodi nyimbo zao.


Hayo yalisemwa kwa nyakati tofauti na mkuu wa kikundi cha Makondelee Rwanyango, Salvatory Byarufu, kikundi cha Kihanga Isingiro, Sabinus Leopord, na mkuu wa kikundi cha ngoma sanaa cha Rumanyika Rwantale, Seta Mathias, wakati wakizungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam, ambapo jana tamasha hilo lilihitimishwa ambalo lilidumu kwa siku tatu.


Mathias alisema wanaamini Nchimbi kwa niaba ya serikali ya awamu nne, wizara yake imebeba jukumu la kuulinda na kuusimamia utamaduni wa makabila ya Tanzania hivyo wanaamini kilio chao atakisikia na kukifanyia kazi kwa karibu.


Alisema Wanyambo kila kukicha wamekuwa wakilalamika kuwa wanabaguliwa na kunyanyaswa na maofisa uhamiaji kwa sababu kabila hilo limekuwa halitambuliwi na watu wengi na kuongeza kuwa makabila mengine yamekuwa yakitambuliwa kwa urahisi kutokana na makabila hayo kuuinua utamaduni wa makabila yao ikiwemo vikundi vya ngoma.


Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Wanyambo, Danile Rutasyamuka, aliishukuru serikali kupitia Idara ya Makumbusho ya Taifa kuwaruhusu kufanya tamasha hilo pia aliwashukuru Wanyambo wote waishio jijini Dar es Salaam na wananchi wa makabila mbalimbali na raia wa kigeni waliojitokeza kuhudhuria tamasha hilo.


Katika hatua nyingine Wanyambo wamemwagia sifa Mkuu wa Wilaya yao, Kanali mstaafu, Fabian Masawe, kwamba ni kiongozi wa kuigwa ambaye anafuatilia kwa karibu matatizo ya wananchi wake.


Walipendekeza kwamba Masawe aendelee kuwa mkuu wao wa wilaya, asihame kwa sababu amekuwa na umuhimu mkubwa kwao, tamasha hilo lilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mohamed Babu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Januari 24 mwaka 2011

No comments:

Powered by Blogger.