Header Ads

DOWANS YAIPIGA CHENGA SERIKALI

• SASA KUIBANA SERIKALI KILA KONA MPAKA WALIPWE

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE kampuni ya kufua umeme ya Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Ltd zimewasilisha rasmi ombi la kuomba fidia ya sh bilioni 94 isajiliwe katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Fidia hiyo ni ile iliyoamriwa kulipwa na TANESCO kwa kampuni hiyo baada ya shirika hilo la ugavi wa umeme nchini kutiwa hatiani na mahakama ya kimataifa ya usuluhishi migogoro ya kibiashara (ICC), kwa kile kilichoelezwa kuwa ilivunja mkataba baina yake na kampuni hiyo kinyume cha taratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana mchana jijini Dar es Salaam, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Salvatory Bongole, alisema ombi hilo la Dowans dhidi ya TANESCO, liliwasilishwa Januari 25 mwaka huu mahakamani hapo na wakili wa kujitegemea ambaye anaiwakilisha kampuni hiyo, Kennedy Fungamtama.

Bongele alisema ombi hilo limepewa namba 8/2011 na jaji wa kulisikiliza ameshapangwa ingawa tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa ombi hilo bado haijapangwa.

“Kimsingi Dowans imeshawasilisha ombi la kuiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam isajili tuzo ya fidia ya sh bilioni 94 waliyoishinda TANESCO katika Mahakama ya ICC…na kweli mahakama imelipokea ombi hilo na kulipatia namba na jaji wa kuanza kuisikiliza…na tuzo hiyo iliwasilishwa hapa Mahakama Kuu na mahakama ya ICC wiki iliyopita.

“Kwa hiyo naomba Watanzania wafahamu kuwa tuzo ya hukumu iliyotolewa na ICC kwa Dowans iliwasilishwa mahakamani hapo wiki iliyopita na iliwasilishwa na mahakama ya ICC yenyewe kwa kuwa huo ndiyo utaratibu wa sheria unavyotaka.

“Na kilichofanywa na Dowans Januari 25 mwaka huu, kupitia wakili wao Fungamtama ni kuwasilisha ombi la kuiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam isajili tuzo yao hiyo …kwa hiyo ieleweke kwamba tuzo ya Dowans bado haijasajiliwa kwani taratibu za kisheria zina kwenda hatua kwa hatua, ”Alisema Bongole.

Hata hivyo, taarifa nyingine za uhakika zinasema kuwa Dowans pia imesajili ombi lao hilo katika mahakama moja nchini Uingereza na kwamba mahakama hiyo inatarajia kutoa notisi ya siku 21 kwa TANESCO kutoa utetezi wake kuhusu kuridhia au kukataa kulipa fidia hiyo.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni mbinu ya tahadhari iliyochukuliwa na kampuni hiyo ili kujihakikishia kuwa inalipwa fidia yake hata kama maamuzi ya mahakama kuu ya hapa nchini yatabatilisha fidia yao waliyotunukiwa na ICC.

“Iwapo mahakama hiyo ya Uingereza itaridhia moja kwa moja kulipwa kwa fidia hiyo na TANESCO ikikataa, basi Dowans watawatumia mawakala wa kitaifa wanaofanya kazi ya kufilisi mali za wadaiwa, ili wakamate mali za serikali ya Tanzania zitakazolingana na thamani ya fidia hiyo ya sh bilioni 94,” alithibitisha zaidi mtoa taarifa wetu.

Tuzo hiyo ya Dowans iliamriwa na ICC Novemba 15 mwaka jana baada ya kampuni hiyo kuishinda TANESCO katika kesi yake ya kudai fidia ya kuvunjiwa mkataba iliyokuwa imefunguliwa rasmi Novemba 20 mwaka 2008 na kupewa namba 15947/VRO.

Tangu ICC itoe hukumu ambayo iliipa ushindi Dowans baadhi ya wananchi, wanasiasa wakiwemo na mawaziri walijitokeza hadharani kuitaka serikali isilipe fidia hiyo kwa madai kuwa kuilipa ni sawa na kuwazawadia mafisadi waliolidanganya taifa tangu ilipoletwa kwa kampuni dada ya Richmond ambayo baadaye ilikujagundulika kuwa ni ya kitapeli.

Hata hivyo, wanasiasa wachache wamekuwa wakiitaka serikali ilipe fidia hiyo kwani kutofanya hivyo ni kukiuka misingi ya utawala wa sheria na mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu haki za raia na mataifa ambayo Tanzania imeridhia kuiheshimu na kuitekeleza.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Januari 28 mwaka 2011

No comments:

Powered by Blogger.