Header Ads

SHAHIDI AFICHUA ALIVYOMKAMATA JERRY MURRO

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa nne wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kushawishi na kuomba rushwa ya Sh milioni 10, inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la TBC1, Jerry Murro na wenzake, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Issa Seleman Chabu (37) ameieleza mahakama jinsi yeye na makachero wenzake walivyoweka mtego na kufanikiwa kumkamata Murro Januari 31 mwaka jana.

Chabu ambaye ndiye aliyeongoza timu ya makachero ya kumkamata Murro alitoa ushahidi huo kwa Hakimu Mkazi, Gabrile Mirumbe wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana wakati akiongozwa kutoa ushahidi na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface.Mbali na Murro washtakiwa wengi ni Edmund Kapama na Deo Mugasa

Mpelelezi huyo kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Ilala alieleza kuwa Januari 30 mwaka jana, saa nne asubuhi akiwa kwenye kazi za nje alipigiwa simu na Station Sajenti Gervas akimwarifu kuwa amepokea taarifa toka kwa Michael Wage kuwa kuna watu wamemtishia kwa silaha na kumwomba rushwa ya sh milioni 10 akanitaka nirudi ofisini.

Alidai kuwa siku hiyo Gervas alikuwa zamu ofisini kwake katika ofisi za RCO-Ilala na yeye akafika ofisini hapo saa nane mchana akamkuta Wage na Gervas wakampatia taarifa za malalamiko hayo kwa kirefu na kuongeza kuwa yeye alifikia uamuzi wa kuwasiliana na Mkuu wake wa kazi-RCO wa Ilala-Duwani Nyanda na kumueleza malalamiko hayo na kwamba mlalamikaji yupo ofisini kwao na kumuomba atupe utaratibu wa kulishughulikia tatizo hilo.

“RCO-Nyanda akanielekeza kwamba nifungue jalada la malalamiko na watuhumiwa wasakwe na wafikishwe kituoni.Na Wage alikuwa akilalamika kuwa kuna watu wawili wamejitambulisha kwake kuwa ni maofisa wawili wa (TAKUKURU )hakuwataja majina na mwingine akamtaja ni Jerry Murro ambaye ni mtangazaji ...na mimi nilitekeleza maagizo kwa kufungua jalada la uchunguzi;

“ Na nikamwelekeza afande Masika achukue maelezo ya Wage na nikamwomba Wage awapigie simu watu hao waliokuwa wakimtisha na kumwomba rushwa na akampigia mmoja wao ambaye alimtaja kuwa ni Murro na simu yake aliiweka kwenye Loud Speaker’ na Wage akamtaka Murro wakutane na Murro akamtaka Wage aje ofisini kwake TBC1 au Bamaga.”alidai Mkaguzi Msaidizi Chabu.

Chabu alidai hata hivyo yeye aliairisha zoezi hilo la Murro kutaka akutane na Wage ofisi za TBC1 na akamwomba RCO-Nyanda zoezi hilo la kuwamata lifanyike kesho yake ombi ambalo lilikubaliwa na mkuu wake wa kazi nakuongeza kuwa Januari 31 mwaka jana,saa nne asubuhi yeye na Wage walitoka katika ofisi za RCO-Ilala na kabla ya kutoka alimwomba Wage awapigie watu hao ili wajue wanakutana nao katika mgahawa wa City Garden.

“Wage akampigia Murro na kumweleza aje amkute katika mhagawa huo ili ampatie mzigo ambao ni sh milioni tisa na Murro akakubali na mimi nikawachukua askari wapelelezi watatu tukafanye mtego katika mgahawa huo na wapelelezi hao ni Station Sajenti Gervas, Sajenti Omary na Koplo Masawe na na tulipofika mimi nilikuwa kiongozi wao na Gervas na Masika niliweka nje ya mgahawa huo na mimi na Gervas tuliingia tuliingia na kukaa ndani ya mgahawa huo saa tano asubuhi;

“Nilipoona Murro atokeo nikamwambia Wage ampigie tena kumwarifu kwamba ameishafika na Wage akampigia huku simu yake ikiwa kwenye Loud Speaker wote tunasikia, Murro akamjibu Wage kuwa anakuja baada ya dakika tano na ndani ya muda huo Murro akafika nje ya mgahawa huo akampigia simu Wage akimtaka atoke nje ya mgahawa ili amkabidhi mzigo huo;

“Wage kabla hajatoka nje nikamkataza asitoke kwanza asubili sisi wapelelezi wawili tuko nje tukawaongezee nguvu wapelelezi wetu wawili tuliowacha nje kwaajili ya mtego, na tulivyotoka na nikamwona Murro akiwa nje ya gari lake amesimama na mimi na wale wapelelezi wenzangu tukapeana ishara zetu za Kiintelijensia na Wage ndiyo akatoka ndani ya mgahawa huo kuja nje na akakutana na Murro ambaye alikuwa akimuita kwa mkono Wage ambaye alikuwa amebeba mkoba ambapo alifungua mlango mwingine wa gari la Murro na kuingia ndani ya gari hilo.

Chabu aliendelea kueleza kuwa baada ya Wage kuingia ndani ya gari la mshatakiwa huyo alifunga mlango haraka na kutaka kuondoka nikamweleza dereva wetu ambaye alikuwa akiendesha gari lenye namba za kiraia akaenda kulizuia gari la Murro ili lisiondoke na ndipo Murro aliposhtuka akamtaka Wage atelemke kwenye gari lake na yakazuka malumbano baina yao wawili na kutokana na hali hiyo yeye alisogea kwenye gari la mshtakiwa huyo na kumuuliza Murro kama alikuwa akimfahamu Wage, mshtakiwa huyo alikana kutomfahamu Wage.

Aidha aliieleza kuwa alimuuliza pia Wage kama alikuwa akimfahamu Murro na Wage alikiri kumfahamu mshtakiwa huyo na kusema kuwa ndiye miongoni mwa aliyemtishia kwa pisto na pingu na kumuomba rushwa y ash milioni 10 na kuongeza kuwa baada ya hapo alijitambulisha kwa Murro kuwa yeye ni ofisa wa polisi na kumweleza kuwa anakabiliwa tuhuma zinazomkabili la na kumtaka afungue gari lake ili yeye na wapelelezi wengine wapande gari lake na aliendeshe kuelekea kituo Kikuu cha Polisi Kati kwa mahojiano zaidi.

“Baada ya kumpa maelezo hayo kwanza Murro alinyamaza akasema haiwezekani kwani katika mgahawa huo yeye alifuatilia habari ya Mchina...nikapanda kiti cha mbele katika gari lake na kumtaka aendeshe gari hadi Kituo cha Kati na alitii amri hiyo na tulipofika nilimwambia afunge gari lake vizuri na anifuatwe kwenye ofisi za RCO-Ilala , tulipofika ofisini nikamuhoji kuhusu tuhuma hizo na alikana na baada ya hapo nikatoa taarifa kwa wakubwa wangu wa kazi kwamba tayari nimeishamata. Shahidi wa sita anaendelea leo kutoa ushahidi wake.

Naye shahidi wa tano wa upande wa Jamhuri, Mkaguzi wa Polisi, Antony Mwita(45) ameeleza kuwa kitabu cha kumbukumbu ya kupokea wageni cha Hoteli ya Sea Cliff kinaonyesha Januari 29 mwaka jana,Murro alifika hotelini hapo siku hiyo.

Mwita ambaye ndiye mpelelezi wa kesi inayomkabili Murro, Edmund Kapama na Deo Mgassa wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza na Majura Magafu, alitoa ushahidi huo kwa Hakimu Mkazi, Gabrile Mirumbe wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana wakati akiongozwa kutoa ushahidi na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface.

Aliieleza mahakama kuwa yeye ni mpelelezi katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZDCO), na kazi zake ni kupeleleza kesi anazokuwa ameelekezwa kuzipeleleza na (ZDCO) na kwamba Januari 31 mwaka jana kiongozi wake alimpa jukumu ya kupeleleza kesi ya kushawishi, kuomba rushwa na washtakiwa kujitambulisha kuwa wao ni maofisa wa serikali huku si kweli inayowakabili washtakiwa.

Mwita alidai Februali 2 hadi 3 mwaka jana, alianza upelelezi wa kesi hii kwa kwenda Hoteli ya Sea Cliff ambapo alipofika kwenye hoteli hiyo aliomba akutanishwe na Meneja wa Teknolojia ya Habari(IT) ili aweze kumpatia picha za kamera za CCTV kutoka kwa meneja huyo kama kweli washtakiwa hao walikutana na shahidi wa tatu(Michael Wage)katika hoteli hiyo siku hiyo ya Januari 29 mwaka jana, akiwemo Murro na wengine.

“Napia kupata maelezo ya mlinzi wa zamu wa siku hiyo Briton Babanyika wa Kampuni ya KK Security na nilichukua maelezo yake na akanipatia kitabu cha kumbukumbu ya wageni walioingia hotelini ambapo kitabu hicho kina majina na namba za magari ya wageni hao;

“Na kitabu hicho kinaonyesha mgeni wa 25 alikuwa ni Jerry Murro na alifika hotelini hapo kwa kutumia gari lake lenye namba za usajili T545 THE aina ya Cresta na mlinzi huyo aliipatia kadi Na.673 na aliingia hotelini hapo saa 7:33 na kuondoka saa 8:48 mchana. ”alidai Mkaguzi Mwita.

Aliendelea kuieleza mahakama kuwa licha ya yeye kukusanya kielelezo hicho cha kitabu pia katika upelelezi wake katika kesi hiyo alienda duka la Mizinga lililopo Upanga jijini, kujiridhisha kama ni kweli Murro alinunua pingu katika duka hilo, na upelelezi wake ulibaini kwamba ni kweli duka hilo lilimuuzia pingu hiyo Mei 26 mwaka 2009 kwa Sh 25,000 na akapewa risiti yenye kumbukumbu na. 34357410. Kwamba mahakama ilipokea risiti ya pingu hiyo kama kielelezo cha nne.Shahidi wa sita anatarajiwa kupanda leo kizimbani kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 26 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.