Header Ads

JAJI MAKARAMBA UMENENA



Na Happiness Katabazi

KWANZA namshukuru mungu kwa kuweza kunipa uzima na afya njema na hadi Desemba 25 mwaka huu, nikaweza kutimiza umri wa miaka 33.

Nikiachana na hilo,leo nitajadili ushauri uliotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara Robert Makaramba alioutoa Desemba 26 mwaka huu kwa vyombo vya habari kabla ya kufungua tamasha la vipaji kwa vijana Wakatoriki.

Jaji Makaramba aliwataka waandishi wa habari nchini kuungana na kupiga kelele kwa serikali ili ibadilishe sheria ya uchochezi iliyorithiwa kutoka kwa wakoloni kwa kuwa ni hatari na inaweza kusababisha wengi wao kufungwa jela pamoja na vyombo vya habari kufilisiwa.

Alisema lazima waandishi waungane kupitia Press Club zao na kuhakikisha wanadai mabadiliko katika sheria hiyo kwani sheria ya uchochezi ipo na kwa namna yoyote mwandishi anaweza kuambiwa ameivunja na hivyo kujikuta akifikishwa mahakamani.

Mimi binafsi nikiwa kama mwandishi wa habari na mwanafunzi wa fani ya Sheria hivi sasa, napenda kuunga mkono ushauri huo wa Jaji Makaramba kwetu sisi waandishi wa habari kwani endapo waandishi wa habari hivi sasa tutaacha dharau, ubinafsi na ujinga tunaweza kuufanyia kazi kwa vitendo ushauri huo ulitolewa na jaji huyo ambaye alishawahi kuwa mwadhiri wa katika kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kabla ya kuteuliwa kuwa jaji.

Ni wazi kwamba Ibara ya 18(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatoa uhuru wa kila mtu kutoa fikra zake.

Lakini hakuna ubishi kwamba licha haki hiyo imewekwa ndani ya Katiba kwa maandishi lakini wakati huu wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete sote ni mashahidi, vyombo vya habari na waandishi wa habari tumekuwa na uhuru mpana sana wa kujadili masuala mbalimbali na mengine nyeti bila vyombo vya dola kuvamia vyumba vyetu vya habari na kufanya uharibifu au kuwadhuru waandishi wa habari wazi wazi kama tunavyoshuhudia nchi za wenzetu ambapo watawala wamekuwa wakitumia vyombo vya dola kubugudhi wanahabari na kuaharibu mitambo ya vyombo vya habari.
Sisi waandishi wa habari hapa nchini tunafahamiana vizuri tu kwani baadhi ya waandishi habari tumekuwa tukitumiwa na wanasiasa wanaoasimiana au wenye nia ya kuwania madaraka ya juu kupitia vyama vyao vya hasa wale wa Chama cha Mapinduzi(CCM) kuandika habari za kuwachafua wanasiasa wenzao.

Na wanasiasa hao wamekuwa wakati mwingine wamekuwa wakitupatia hata mazungumzo mbalimbali yanayojadiliwa kwenye vikao vya siri vya vyama vyao ambayo mazungumzo hayo yakichapishwa kwenye vyombo vya habari yanakuwa yamemchafua mwanasiasa wanawayehasimiana naye.

Na situ tumekuwa tukitumiwa na wanasiasa, bali hata wafanyabiashara na makundi mengine katika jamii nayo yamekuwa yakiwatumia baadhi ya waandishi wasio waadilifu ama kwa kujua au kutokujua kupenyeza ajenda zao zichapishwe kwenye vyombo vya habari kwa maslahi yao binafsi badala ya taifa.

Na wakati mwingine waandishi wa habari wa aina hiyo wamekuwa wakikubali kuaziandika habari hizo bila ya kuwa na vielelezo vyovyote mkononi jambo ambalo mwisho wa siku serikali au mtu binafsi anapoamua kulishtaki gazeti au kuwafikisha wahariri na waandishi wa habari mahakamani, wanajikuta hawana ushahidi ambao unaounga mkono habari au makala walizozichapisha ambazo zimeleta madhara kwa watu au serikali.

Ikumbukwe kuwa kifungu cha 9 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kinasema kutojua sheria siyo kinga ya kutokuadhibiwa.

Kwa hiyo sisi waandishi wa habari tukae tukijua sheria ya uchochezi ipo na ni kweli ni hatari kwetu sisi waandishi wa habari na endapo siku serikali itakapoamua kuanza kuitumia dhidi yetu ni wazi kabisa tutajikuta tukiangukia kwenye mkondo ule ule wa kufikishwa mahakamani na magerezani.

Somo zuri tumelipata kupitia hukumu mbalimbali zilizotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Mauji ya Kimataifa yenye makao makuu yake mjini Arusha,ambapo tulishuhudua waandishi wa habari walivyotiwa hatiani kwa makosa ya uchochezi na kuhukumiwa kwenda jela.
Lakini pia nimalizie kwa kutoa rai kwa wamiliki wa vyombo vya habari hapa nchini waondokane na uwekezaji uchwara katika sekta ya habari na badala yake waanze kuajili wanasheria kwa wingi ambao wanasheria hao ambao kutwa nzima watakuwa wakishinda ndani ya vyombo vya habari na kuzipitia habari zote zinazoandikwa na waandishi na kuhaririwa na wahariri ili kuweza kunusuru waandishi, wahariri na vyombo vya habari kukumbwa na kadhia ya kufikishwa mahakamani kwa kuandika na kupitisha habari ambazo ni za kichochezi.

Mwisho nimalize kwa kuwakumbusha waandishi wenzangu kuwa kila mmoja atimize wajibu wake kwa maslahi ya taifa hili na siyo kwa maslahi ya manyang’au kwani endapo tutakubali kuandika habari au makala za uchochezi mwisho wa siku tutaangukia mikononi mwa dola jambo ambalo si jema.

Hivyo wakati tukitafakari ushauri wa Jaji Makaramba,na sisi waandishi wa habari miongoni mwetu tujitazame upya na huu uhuru mpana wa kuandika na kuzungumza tuutumie vizuri kwaajili ya kuuletea tija taifa letu na siyo kuwaletea tija wanasiasa manyang’au ambao leo hii wameanza kupiga jalamba kuutaka urais wa Tanzania mwaka 2015 kwa gharama zozote kwani mwisho wa siku madhara ya kufunguliwa kesi yatakapotupata wanasiasa hao manyang’au hawatatusaidia kwa lolote na hiyo ndiyo tabia ya wasiasa wengi hapa nchini.

Nawatakia maandalizi mema ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2012.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
0716- 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Septemba 29 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.