Header Ads

JERRY MURRO ASHINDA KESI




Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imemwachilia huru aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC 1), Jerry Murro (30) na wenzake ambao walikuwa wakikabiliwa na makosa ya kula njama na kuomba rushwa ya sh milioni 10 baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka yao.

Sambamba na hilo, tayari Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Dk. Eliezer Feleshi kupitia Mkurugenzi Msaidizi wa ofisi hiyo, Stanslaus Boniface, jana saa 6:46 mchana aliwasilisha hati ya nia ya kuikatia rufaa hukumu hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na mahakama hiyo imekwisha kuipokea.

Hukumu hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa shahuku kubwa na umma, ilisomwa jana kwa takriban saa mbili na Hakimu Mkazi, Frank Moshi, ambaye alisema baada ya kupitia kwa kina ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa Jamhuri, mashahidi wanne wa upande wa utetezi na vielelezo vilivyotolewa na upande wa Jamhuri, mahakama hiyo imefikia uamuzi wa kuuona upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi yao, kwakuwa ushahidi wao ni dhahifu na umeshindwa kuishawishi mahakama hiyo kuwatia hatiani washitakiwa hao.

Hakimu Moshi alisoma hati ya mashitaka iliyokuwa na jumla ya mashitaka matatu, ambapo shitaka la kwanza ni la kula njama kinyume cha kifungu namba 32, shitaka la pili ni kuomba rushwa ya sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage, kinyume cha kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 ambalo wanadaiwa kulitenda Januari 29, mwaka 2010.

Shitaka la tatu ambalo linamkabili mshitakiwa wa pili, Edmund Kapama ‘Dokta’ na mshitakiwa wa tatu, Deogratius Mugassa, ni kudai kuwa wao ni maofisa wa Takukuru kinyume cha kifungu cha 100 B cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, ambacho kinasomwa pamoja na kifungu cha 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya mwaka 2002.

Hakimu Moshi alisema upande wa Jamhuri katika harakati zake za kuthibitisha shitaka la kwanza ilimleta shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri, Michael Wage, ambaye katika ushahidi wake alidai kukutana na washitakiwa hao katika Hoteli ya Sea Cliff Januari 29, mwaka jana, na kielelezo cha tatu ambacho ni picha za kamera ya CCTV ya hoteli hiyo ambayo alidai inaonyesha sura za washitakiwa hao na yeye na kwamba alikuwa akifanya mawasiliano kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu (SMS).

“Sasa mahakama imefikia uamuzi wa kuona ushahidi wa Wage una mapungufu kwani Jamhuri imeshindwa kuleta nakala ya mawasiliano ya ujumbe mfupi ‘print out’ ambazo zingethibitisha Murro alikuwa akiwasiliana na Wage.

“Pia kwa kitendo cha Jamhuri kushindwa kuleta video ya kuona mahakamani, gwaride la utambulisho na nakala halisi ya picha za CCTV zinazoonyesha washitakiwa wote kweli walikutana pamoja na Wage…mahakama hii inatamka wazi kuwa Jamhuri imeshindwa kuthibitisha kosa hili na kwa sababu hiyo inawaachilia huru washitakiwa wote katika kosa hili la kula njama,” alisema Hakimu Moshi.

Akilichambua kosa la pili ambalo ni la kuomba rushwa ambalo pia linawakabili washitakiwa wote watatu, alisema kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri, Wage alidai kuwa mshitakiwa wa pili na wa tatu (Kapama na Muggasa) walijitambulisha kwake kama wao ni maofisa wa Takukuru na wakamtaka awapatie kiasi hicho cha fedha kwakuwa yeye anakabiliwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma ili wasimkamate na kwamba Murro alimwambia ampatie fedha hizo ili asiende kuzirusha tuhuma hizo kwenye kipindi cha Usiku wa Habari kinachorushwa na Televisheni ya TBC1, na kwamba Kapama alipokea kianzio ambacho ni sh 9,000,000 kwa ahadi kuwa kesho yake angekuja kuwamalizia kiasi kilichosalia katika kiwango cha awali walichokuwa wakikitaka kutoka kwake ambacho ni shilingi milioni 10.

Na kwamba Wage alidai Januari 30, mwaka jana alikwenda kutoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi kuwa kuna watu wanamuomba rushwa na kwamba polisi waliweka mtego ambapo waliondoka na shahidi huyo hadi mgahawa wa City Garden uliopo Mtaa wa Mkwepu jijini Dar es Salaam, na Wage akaamuliwa na polisi hao kumpigia simu Murro ili aje kuchukua kiasi cha fedha kilichosalia na kweli baada ya muda mfupi Murro alifika katika eneo la mgahawa huo na kabla ya kushuka kwenye gari alizingirwa na polisi waliokuwa wamemuwekea mtego waliokuwa wakiongozwa na shahidi wa nne, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Issa Chabu.

Hakimu huyo akilichambua shitaka hilo la pili, alisema mahakama imeshindwa kuelewa ni kwanini polisi hao siku hiyo walimkamata Murro kwa haraka kiasi kile na kwamba zile picha za CCTV kamera ambazo zilipokewa na mahakama kama kielelezo cha tatu hazionekani vizuri na kwamba haziusaidii upande wa Jamhuri kuonyesha uhalisia wa washitakiwa hao.

“Mahakama hii imeona Hoteli ya Sea Cliff ni eneo lenye shughuli nyingi sana na linatembelewa na watu wengi na Murro wakati akijitetea alidai kuwa alifika katika hoteli hiyo kwa ajili ya kusaka habari na kwamba kosa hili liliungwa mkono na ushahidi wa Wage na mahakama hii inasema Jamhuri imeshindwa pia kulithibitisha shitaka hili la pili na hivyo mahakama inawaachiria huru washitakiwa wote katika kosa la pili,” alisema Hakimu Moshi.

Kuhusu shitaka la tatu ambalo ni la kujitambulisha kwa Wage kuwa wao ni maofisa wa Takukuru linamkabili Kapama na Mugassa peke yao, hakimu Moshi alisema mahakama imejiuliza umakini wa Wage uko wapi kwani kama ni kweli washitakiwa walijitambulisha kwake kuwa wao ni maofisa wa Takukuru ni kwanini Wage asingeomba washitakiwa hao wampatie vitambulisho vyao?

Aidha, Hakimu Moshi alidai kuwa wakati Kapama na Mugassa wakijetetea waliyakana majina ya Dokta na Kaimu Mkurugenzi wa Takukuru ambayo upande wa Jamhuri ulidai washitakiwa hao walijitambulisha kwa Wage kwa majina hayo na kuongeza kuwa upande wa Jamhuri ulipaswa ufanye uchunguzi mitaani ili kubaini majina hayo na vyeo hivyo kama kweli washitakiwa hao wanavitumia mitaani.

“Mahakama imeonelea shitaka hili la tatu nalo limeacha mashaka makubwa kwani hakuna vielelezo vinavyoonyesha washitakiwa hao Kapama na Mugassa walijiwakilisha kuwa wao ni maofisa wa Takukuru na kwasababu hiyo mahakama hii inawaachiria huru washitakiwa wote kwenye kosa hili la tatu na makosa mengine yote, hivyo kuanzia sasa washitakiwa wote mpo huru na upande wowote kama haujaridhika na hukumu yangu una haki ya kukata rufaa katika mahakama ya juu,” alisema Hakimu Moshi.

Aidha, hakimu huyo alitoa amri kwamba Murro aliyekuwa anatetewa na mawakili wa kujitegemea, Richard Rweyongeza na Pascal Kamala wakati washitakiwa wengine walikuwa wakitetewa na Majura Magafu arejeshewe pingu na bastola yake ambayo ilitolewa mahakamani hapo na upande wa jamhuri kama vielelezo kwasababu vitu hivyo havikubishaniwa mahakamani hapo.

Baada ya kumalizika kusomwa kwa hukumu hiyo umati wa ndugu na jamaa wa washitakiwa hao waliwalaki kwa furaha ndugu zao hao ambao walishinda kesi hiyo nje ya viwanja vya mahakama hiyo huku ndugu mmoja wa Murro ambaye hakuweza kufahamika jina lake mara moja alikwenda kumkabidhi chupa ya mvinyo ambayo Murro aliipokea kwa furaha.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya viwanja vya mahakama hiyo huku akiwa ameambatana na mkewe Jeniffer John, Murro alisema amewasamehe baadhi ya viongozi wa serikali na maofisa wa Jeshi la Polisi ambao walimbambikizia kesi hiyo na kwamba yote ana mwachia Mungu.

“Natoa ushauri wa bure, wanachi wenzangu na maofisa serikali na polisi tuache kutafutana badala yake tufanye kazi kwa masilahi ya taifa letu, matatizo yaliyonikuta mimi yalikuwa ni yakunitafuta mimi lakini leo hii nashukuru nimeweza kuishinda kesi yangu na ninawashukuru wale wote waliokuwa karibu na mimi katika matatizo haya wakawa wananiombea na kwa moyo mmoja natamka rasmi kuwa nimewasamehe wale viongozi wa serikali na jeshi la polisi ambao walibambikia kesi hii,” alisema Murro huku akijifuta machozi na kisha kuondoka mahakamani hapo.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Msaidizi katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Stanslaus Boniface, akizungumza na Tanzania Daima jana mchana alisema Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini inayoongozwa na Dk. Eliezer Feleshi haijaridhika kabisa na hukumu hiyo na kwamba jana hiyo hiyo saa saba mchana walikuwa wameishawasilisha hati ya nia ya kukata rufaa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Februari 5, mwaka 2010, washitakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo wakikabiliwa na mashitaka hayo ya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa Michael Wage, mashitaka ambayo waliyakana na kwa wakati wote huo hadi jana kesi hiyo ilipotolewa hukumu washitakiwa hao walikuwa nje kwa dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Desemba 1 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.