Header Ads

MCHINA AHUKUMIWA, AKAMATWA TENA

Na Happiness Katabazi



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilimhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya sh 100, 000 raia wa China Xuxiab We Ng (26) baada ya mshtakiwa kukiri kutenda kosa la kumzuia ofisa wa Idara ya Uhamiaji asifanye kazi yake.


Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Aloyce Katemana, muda mfupi baada ya Mwanasheria wa Idara ya Uhamiaji Patrick Ngayomela, kumsomea shtaka linalomkabili mshtakiwa ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea, Yassin Memba, na kisha mshtakiwa jana alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza kukiri kutenda kosa hilo.

Hakimu Katemana alisema kwa kuwa mshtakiwa amekiri kosa linalomkabili mahakama hiyo inamtia hatiani kwa kosa hilo ambalo ni kinyume na kifungu cha 31(1)(f) na (2) cha Sheria ya Uhamiaji, hata hivyo mshtakiwa huyo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Teng Da Foot Wear Co Ltd, alilipa faini hiyo na kuachiliwa huru.

Dakika kumi baada ya raia huyo wa China kulipa faini, alijikuta akikamatwa na askari wa polisi wa mahakamani hapo na kisha kupelekwa kikuo kikuu cha Polisi Kati, kwa ajili ya kufunguliwa kesi mpya ya shambulio la kudhuru mwili.

Awali wakili wa Idara ya Uhamiaji, Ngayomela, akimsomea shtaka lake, alidai kuwa Novemba 30, mwaka huu, huko Kariakoo mshtakiwa huyo alimzuia Ofisa Uhamiaji Koplo Mussa Abdallah Mkubwa, kufanya kazi yake kwa kumshambulia na kumsababishia maumivu makali yaliyompelekea kulazwa hospitali akiwa hajitambui.

Na kwamba baada ya kumpiga mshtakiwa huyo alikamatwa na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Kati na kuchukuliwa maelezo na alikiri kosa na iliamuriwa afikishwe mahakamani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Desemba 3 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.