Header Ads

UPELELEZI KESI YA MATTAKA TAYARI

Na Happiness Katabazi


UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kununua magari ya mitumba kinyume na Sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ndege(ATCL), David Mattaka na wenzake umeileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.


Wakili Mwandamizi wa Serikali Oswalid Tibabyemokya alieleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Ritha Tarimo wakati kesi hiyo jana ilipokuja kwaajili ya kutajwa ambapo alieleza kuwa upelelezi huo umekamilika na kwamba wanaiomba mahakama hiyo ipange tarehe kwaajili ya kuja kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.

Kwa upande wake Hakimu Tarimo alisema anaiarisha kesi hiyo hadi Januari 5 kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa na kwamba usikilizwaji wa awali utafanyika Januari 23 mwakani.

Novemba 22 mwaka huu, Mattaka anayetetewa na wakili Peter Swai na Kaimu Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha Elisaph Mathew Ikomba na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Ndani, William Haji anayetetewa na wakili Alex Mgongolwa walifikishwa mahakamabi hapo kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na makosa kushindwa kutunza kumbukumbu za mawasiliano ya manunuzi waliyokuwa wakifanya na mtoa huduma kinyume na kifungu cha 55(3),87(1)(f) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma Na. 21 ya mwaka 2004 na kanuni ya 17(1) ya Sheria ya Manunuzi (Goods,Works,Non-Consultant Services and Disposal of Public Asets by Tender) Regulation,G.N. No.97 of 2005.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa(TAKUKURU) alidai shtaka la pili ambalo linawakabili ni la kushindwa kutimiza matakwa ya vifungu vya Sheria ya Manunuzi ya Umma na Kanuni zake kinyume na kifungu cha 87(1)(f) cha Sheria ya Manunuzi ya umma ya mwaka 2004.

Shtaka la tatu lina mkabili Mattaka peke yake ni matumuzi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa ya mwaka 2007 ambapo Mattaka alitoa idhini ya kununuliwa kwa magari hayo bila ya kuwepo kwa mkataba wa pande zote mbili na bila idhini ya Bodi ya ATCL.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Desemba 6 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.