Header Ads

SERIKALI YASHAURIWA

Na Happiness Katabazi


SERIKALI imetakiwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 7 cha Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 na Katiba ya nchi kabla ya kuanza uchukua uamuzi wa kuwaondoa kwa nguvu wakazi wanaoishi kwenye makazi hatarishi yaliyoathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha wiki iliyopita.


Ushauri huo wa kisheria umetolewa jana na Mhadhiri toka Kituo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Onesmo Kyauke jana alipofanya mahojiano maalum na gazeti hili jijini Dar es Salaam, ambapo alisema endapo serikali haitazingatia hilo na badala yake ikatumia mabavu, mwisho wa siku itajikuta ikifikishwa mahakamani na wakazi hao na kuwalipa fidia kubwa.

Kyauke alisema kifungu cha 7 cha Sheria ya Ardhi Na.113 ya mwaka 1996, kinatamka watu wanaoishi kwenye makazi hatarishi yakiwemo maeneo ya mabondeni na kwamba kifungu hicho kinawatambua wakazi wanaoshi

“Kwa hiyo endapo serikali inataka kuwaondoa wakazi wanaoishi kwenye maeneo hayo kwanza inapaswa kuzingatia matakwa ya kifungu hicho cha sheria hiyo kwa Waziri mwenye dhamana ya ardhi kwa kuanza kutoa tangazo kwenye gazeti la serikali la kusudio la kulitangaza eneo fulani ni eneo hatarishi na kisha nakala hiyo ya hilo tangazo la waziri huyo linapaswa lipelekwe kwa wakazi wa eneo hilo waweze kulisoma;

“Na wakazi hao wakishalisoma tangazo hilo la waziri na kama hawakubaliani nalo, wakazi hao wa eneo hilo hatari watakuwa na haki ya kwenda kutoa malalamiko yao mbele ya Kamishna wa Ardhi na kamishna wa ardhi atawasilikiza na kuandika ripoti yake na kisha ripoti hiyo kumkabidhi waziri na kumshauri waziri kuwa eneo hilo kweli ni hatarishi;

“Ambapo waziri huyo ataisoma ripoti hiyo na ushauri huo na kama hataridhika na huo utetezi wao, waziri huyo ataipeleka ripoti hiyo kwa rais wa nchi na kisha rais wanchi ndiyo atakaye tangaza kulichukua eneo hilo kwasababu eneo hilo ni hatarishi na eneo hilo linakuwa ni mali ya serikali lakini pia wakazi hao watapaswa walipwe fidia”alisema Kyauke.
Alisema licha ya rais wa nchi kutangaza kulichukua eneo hilo hatarishi kwaajili ya kulibadilisha matumuzi yake ,wakazi hao watakuwa na haki ya kupewa fidia kwanza hata kama wakazi hao walikuwa wakimiliki maeneo hayo kwa kutumia hati za kimila au za wizara.

Kyauke ambaye ni wakili wa kujitegemea pia alisema kwa hiyo agizo lilotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Meck Sadick na Rais Jakaya Kikwete lilowataka wakazi hao wahame halikufuata taratibu hizo za kisheria ambapo mwisho wa siku serikali inaweza kujikuta ikifikishwa mahakamani na wananchi hao na kudaiwa fidia na wakazi hao kwani kifungu cha saba cha sheria ya ardhi kinawatambua wakazi wanaoishi kwenye maeneo hatarishi ambayo yamepimwa na ambayo hayajapimwa.

“Kwa hiyo naiomba serikali yetu ifuate taratibu hizo za kisheria kwani ieleweke wazi Katiba ya nchi ina mpa haki mwananchi ya kumiliki mali na ardhi hivyo, katika kukabiliana na tatizo hilo natoa ushauri kwa serikali ifuate taratibu za kisheria ambazo zipo wazi”alisema Kyauke.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Desemba 28 mwaka 2011

No comments:

Powered by Blogger.