Header Ads

MEJA JWTZ KORTINI KWA UTAPELI

Na Happiness Katabazi


MEJA wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kikosi cha 511 cha Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, Muhsini Kombo (39) na Devotha Soko (33), jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa tuhuma ya kujipatia sh milioni 100 kwa njia ya danganyifu.



Mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema, wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya, alidai katika shitaka la kwanza kuwa Kombo pamoja na Devotha Soko walikula njama na kughushi kati ya Januari-Machi mwaka 2008.

Wakili Komanya alidai shitaka la pili ni kwamba Machi 25 mwaka 2008 kwa nia ya udanganyifu washitakiwa walighushi mhutasari wa kikao cha Machi 25 mwaka 2008 na kujaribu kuonesha kuwa familia ya marehemu Awadhi Shoo imemteua Devotha Soko kuwa msimamizi wa mirathi.

Katika shitaka la tatu inadaiwa kuwa Aprili 23 mwaka 2008 , Devotha alitoa nyaraka za uongo katika Mahakama ya Mwanzo Sinza jijiini Dar es Salaam, kwa lengo la udanganyifu na akajaribu kuonyesha ameteuliwa kusimamia mirathi ya familia ya marehemu Awadhi Shoo.

Katika shitaka la tano, inadaiwa kuwa Mei 15 mwaka 2008 katika Mahakama ya Mwanzo Sinza , Devotha alimpatia hakimu wa mahakama hiyo taarifa hizo ambazo si za kweli, kuwa marehemu Awadhi Shoo alifariki dunia mwaka 1986 akiacha watoto wawili, Juma na Asha na kwamba mshitakiwa huyo wa pili amesimamia mirathi hiyo huku akijua si kweli.

Imeelezwa kuwa Januari 21 mwaka 2011 kwa nia ya udanganyifu, washitakiwa wote wawili walijipatia sh milioni 100 kutoka kwa Rukia Zidadu baada ya kumuuzia nyumba iliyopo kitalu Na. 281 Block 46 huko Kijitonyama. Washitakiwa wamekana mashitaka na upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Hakimu Lema alikubali dhamana ya fedha taslimu sh milioni 25 au kuwasilisha hati ya mali yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo, Devotha alitimiza masharti hayo ya dhamana lakini Meja Kombo alishindwa kutimiza masharti hayo na amepelekwa rumande hadi Desemba 19 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Desemba 6 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.