Header Ads

MAWAKILI WA LIYUMBA WAKWAMISHA KESI

Na Happiness Katabazi


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilijikuta ikishindwa kuanza kusikiliza pingamizi la awali lililotarajiwa kuwasilishwa na mawakili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba (63), anayekabiliwa na kesi ya kukutwa na simu gerezani kwa sababu ya mawakili hao kutokuwepo mahakamani bila kutoa taarifa rasmi.



Liyumba anayetetewa na mawakili wa kujitegemea Majura Magafu na Hudson Ndusyepo, alifika mahakamani na kudai kuwa Magafu amemweleza kuwa yuko Mahakama Kuu kwenye kesi nyingine na Ndusyepo kampeleka hospitalini baba yake mzazi kwani ni mgonjwa.

Hoja hiyo ilionekana kumkera wakili wa serikali Elizabeth Kaganda, ambaye alidai upande wa jamhuri ulikuwa tayari kwa ajili ya kuanza kusikiliza pingamizi la upande wa utetezi na kwamba anasikitishwa na kitendo cha mawakili hao kutofika mahakamani bila kutoa taarifa za udhuru kwa utaratibu unaostahili.

Kwa upande wake, Hakimu Stewart Sanga, alimweleza mshtakiwa huyo kuwa mawakili wake walipaswa kutoa taarifa mahsusi kama kweli wako Mahakama Kuu na kwa ajili gani kwani wakili kwenda kuhudhuria kesi Mahakama Kuu si jambo la kushtukiza.

Alisema anaiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 21, mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kusikiliza pingamizi la awali ambalo litawasilishwa na mawakili wa utetezi.

Septemba 8, mwaka huu, Liyumba alifikishwa mahakamani akikabiliwa na kesi ya kukutwa na simu gerezani kinyume na sheria za Magereza chini ya kifungu cha 86 (1,2) kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Desemba 3 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.