Header Ads

KAFULILA AREJESHEWA UBUNGE

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetoa amri ya muda ya kusitisha utekelezwaji wa azimio la kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi, kilichomvua uanachama, David Kafulila (Kigoma Kusini), hivyo kupoteza kiti chake cha ubunge.

Amri hiyo ya muda ilitolewa jana na Jaji Alise Chinguilwe, muda mfupi baada ya kusikiliza ombi lililoletwa chini ya hati ya dharura na Kafulila kupitia kwa wakili wake, Daniel Welwel.

Akitoa uamuzi huo uliomwacha Kafulila akiwa na furaha isiyo kifani, Jaji Chinguilwe alisema, ametoa uamuzi huo baada ya kusikiliza na kuridhishwa na hoja za wakili huyo.

“Nimesikiliza hoja za wakili wa mlalamikaji (Kafulila) na mahakama hii inatoa amri ya kusimamisha utekelezaji wa azimio hilo la NEC ya Chama cha NCCR- Mageuzi ambalo lilimvua uanachama mlalamikaji kwa madai kuwa alikiuka katiba ya chama hicho,” alisema.

Akifafanua juu ya uamuzi huo, jaji huyo alisema kuwa mahakama yake imeona kuwa endapo itaruhusu utekelezwaji wa azimio la NEC ya chama hicho iendelee na uamuzi wake, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), italitangaza jimbo hilo kuwa liko wazi.

“Na ni wazi kuwa NEC ikishatangaza kuwa jimbo hilo liko wazi, itaitisha uchaguzi mdogo wakati kesi ya msingi iliyofunguliwa na Kafulila itakuwa bado haijatolewa uamuzi.

“Hivyo basi, mahakama yangu imezingatia mambo yote hayo, kwa hiyo inakubaliana na ombi la kuzuia utekelezwaji wa azimio la kikao hicho hadi kesi ya msingi iliyofunguliwa na Kafulila mahakamani hapo, itakapo malizika,” alisema Jaji Chinguile.

Kwa amri hiyo ya Mahakama, Kafulila ni Mbunge halali wa Kigoma Kusini hadi hapo mahakama itakapotoa hukumu ya kesi ya msingi iliyofunguliwa na mwanasiasa huyo kijana.

Ijumaa iliyopita Kafulila alifungua kesi ya madai dhidi ya chama hicho na Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, ya kupinga uhalali wa kikao cha NEC ya NCCR–Mageuzi, kilichoketi Desemba 17 mwaka huu, jijiji Dar es Salaam.

Kikao hicho pamoja na mambo mengine, kilimvua uanachama mbunge huyo kwa madai ya utovu wa nidhamu na kukiuka kanuni na taratibu za chama.

Kesi hiyo namba 218/2011, itakuja tena Februari 21mwakani ambapo itakuja kwa ajili ya kutajwa.

Kwa miezi kadhaa sasa, Kafulila amekuwa akiripotiwa na vyombo vya habari kuwa amekuwa akimshinika Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia ajivue gamba kwa madai kuwa ameshindwa kukiongoza chama hicho.

Msimamo huo uliibua makundi ndani ya chama hicho na mwisho wa siku chama hicho kikafikia uamuzi wa kuitisha kikao cha NEC cha dharura, kisha kufanya uamuzi wa kumfukuza uanachama Kafulila.

Mbali ya Kafulila, chama hicho pia kilimvua uanachama kada wake aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais katika uchaguzi uliopita, Hashim Rungwe, kwa madai kama hayo ya Kafulila.

Pia NEC ya chama hicho, ilitoa onyo kali kwa baadhi ya wabunge na wanachama wengine ambao wanadaiwa kuwa ni wafuasi wa kundi la Kafulila.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Desemba 28 mwaka 2011

No comments:

Powered by Blogger.