Header Ads

KESI YA KAFULILA,NCCR-MAGEUZI-MAWAKILI WATUNISHIANA MISULI

Na Happiness Katabazi

CHAMA cha NCCR-Mageuzi nchini kimedai vyombo vya habari vilivyochapisha na kutangaza habari jana kuhusu amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam katika kesi ndogo Na.218/2011 iliyofunguliwa mahakamani hapo na Mbunge wa Kigoma Kusini kupitia chama hicho David Kafulila na wenzie saba.


Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Idara ya Katiba na Sheria wa chama hicho, Dk.Sengondo Mvungi katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jana katika makao makuu ya chama hicho ambapo alisema lengo la mkutano huo ni kutoa ufafanuzi zaidi wa kilichoamriwa na Jaji Alise Chinguile juzi jioni.

“Nyie vyombo vya habari hivi mmefikia hatua sasa ya kuchakachua hata amri za mahakama?Kumbukeni hata vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyotokea Rwanda, waandishi wa habari walishiriki kuleta machafuko yale sasa nataka niwaeleze jambo moja mfahamu kuwa hii Tanzania ni yetu sote na kamwe mimi na chama changu hatuwezi kuona nyie waandishi wa habari mnachakachua hata amri za mahakama halafu tunanyamaze kimya”alisema Dk.Mvungi kwa sauti ya ukali.

Dk.Mvungi akitolea ufafanuzi wa kilichoamliwa na mahakama ni kuhusiana na yale waliyoyaomba ambapo hakuna hati yoyote inayoonyesha maombi ya kubatilisha maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho yaliyotolewa Desemba 17 mwaka huu na kwamba suala la kuamuru upande katika kesi usifanye jambo zaidi ni katika mamlaka ya mahakama ambalo chama hakina tatizo na suala hilo.

“Ni vyema ieleweke wazi kwamba hakuna amri yoyote ya mahakama iliyotolewa ya kuwabakiza waliovuliwa uanachama katika chama.Wala hakuna amri ya kuwafutia adhabu yoyote waliyopewa wale waliodhibiwa . Hivyo maamuzi ya NEC yababaki kuwa sahihi na halali kwa mujibu wa sheria za nchi mpaka pale ambako mahakama itaamua vinginevyo.

“Msimamo wa chama chetu kwa sasa ni kwamba maamuzi yake ya NEC ambayo yalimvua uanachama Kafulila bado hayajatenguliwa wala kujadiliwa na mahakama yoyote ile.Isipokuwa kwa sasa tumepokea amri ya Mahakama Kuu ikizuia chama kisiendelee na hatua zaidi dhidi ya Kafulila na wenzake walioshirikiana kushitaki chama kwenye kesi Na.218/2011 mpaka shauri la msingi litakapoamriwa”alisema Dk.Mvungi.

Alisema msimamo wa chama chake ni kwamba hautaipinga amri hiyo ya mahakama licha amri hiyo imetolewa bila wadaiwa ambao ni Chama cha NCCR-Mageuzi na Mwenyekiti wake James Mbatia bila kujulishwa wala kupewa wito wa mahakama kuwa Kafulila amewafungulia kesi mahakamani hapo na kwamba wameshangazwa na hatua hiyo ya mahakama ya kusikiliza ombi hilo bila ya kutoa wito wa kuitwa kwa wadaiwa ili waje kujitetea na kwamba chama hicho kimeamua kitaenda kuudhulia kwenye kesi kubwa ambayo itatajwa Februali 21 mwaka huu.

Vyombo vya habari vingi jana viriripoti habari ambazo zilimkariri wakili wa Kafulila, Daniel Welwel kuwa mahakama imetoa amri ya kuzuia utekelezwaji wa uamuzi wa NEC ya chama hicho wakati amri ya mahakama haikusema hivyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Desemba 29 mwaka 2011.
mwisho

No comments:

Powered by Blogger.