Header Ads

KESI YA HAMAD RASHID KUSIKILIZWA JANUARI 19

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Dar es Salam imepanga kusikiliza maombi ya Mbunge wa Wawi Zanzibar Hamadi Rashid na wenzake 10 waliofukuzwa uanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), juma lijalo.

Rashid na wenzake juzi waliwasilisha maombi mahakamani hapo wakiiomba mahakama hiyo iwamuru waitwe mahakamani wajieleze ni kwa nini wasitiwe hatiani na kufungwa kwa kupuuza amri ya mahakama.

Pia anaiomba mahakama ibatilishe uamuzi wa Baraza Kuu la Chama hicho wa kuwafukuza uanachama na itamke kuwa wao bado ni wanachama halali wa chama hicho.
Habari zilizolifikia Tanzania Daima jana na kuthibitishwa na Wakili wa kina Rashid Agustine Kusalika zinasema kuwa maombi hayo yamepangwa kusukilizwa Alhamisi ijayo Januari 19, 2012 na kwamba maombi hayo yatasikilizwa na Jaji Augustine Shangwa anayesikiliza kesi ya msingi .

Januari 4 Jaji Shangwa wa Mahakama Kuu Dar es Salaam iliagiza Baraza Kuu la CUF lisitishe mchakato wa kuwasimamisha au kuwafukuza uanachama Rashid na wenzake wala kuendelea kuwajadili wakati wa mkutano wake wa Januari 4 uliofanyika Zanzibar.

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya Rashid na wenzake kuwasilisha maombi Januari 3, 2012 wakiiomba mahakama hiyo iamuru mkutano huo ambao ulikuwa na lengo la kuwafukuza uanachama usitishwe hadi kesi yao ya msingi itakapomalizika.
Katika kesi yao hiyo ya msingi namba 1 ya mwaka 2012, Rashidi na wenzake wanahoji uhalali wa Kamati ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho na uteuzi wa wajumbe wake.
Kamati hiyo ndio iliyowahoji Rashid na wenzake na kisha kupendekeza kwa Baraza Kuu wafukuzwe uanachama.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya kuwasilisha maombi hayo madogo, Rashid alisema CUF wamevunja Katiba ya Nchi kwa kuidharau amri ya Mahakama pamoja na Katiba ya chama chao.

Alisema Ibara ya 4 ya katiba ya chama hicho inasema kuwa mahakama ndio itakayoamua mambo yote yakiwemo yahusuyo migogoro baina ya wanachama bila kuingiliwa isipokuwa kwa kukata rufaa tu na kwamba Ibara ya 5 inasisitiza kuwa juu ya utawala wa Sheria.
Alisema kutokana na chama hicho kukiuka amri halali ya mahakama basi yeye bado ni mbunge halali wa Wawi na kwamba hata kwenye vikao vya kamati za Bunge vitakavyoanza Januari 15 atashiriki.

Alisisitiza kuwa tayari ameshawalisha taarifa na vielelezo kwa Spika Anne Majkinda na kwamba kwa mujibu wa kanuni za bunge kama jambo liko mahakamani haliwezi kuchukua hatua yoyote hadi mahakama itakapokuwa imetoa uamuzi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamsi, Januari 12 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.