Header Ads

NI MGOMO WA MADAKTARI AU?



Na Happiness Katabazi

KWA takribani wiki moja sasa vyombo vya habari vimekuwa vikipambwa na habari za mvutano baina ya serikali na madaktari kuwa wamegoma kufanyakazi kwa kile wanachodai kupandishiwa mishahara, kujengewa nyumba za kuishi na kuongezewa masurufi yao.

Taarifa za mvutano huo binafsi zimekuwa zikinikosesha raha na kunikera mno na kuanza kutamani kuwa na viongozi madikteta.

Nao baadhi ya madaktari walinukuliwa wakisema wameishapita kiwango cha kuongea na waziri wa afya na Ustawi wa Jamii, Dk.Juma Mponda kwani ameshindwa utatua mwenye uwezo wa kuongea nae hivi sasa ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda na kushinikiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Brandina Nyoni, hii ni dharau ya aina yake.

Wakati madaktari hao wakitoa maneno hayo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk.Mponda, Alhamisi ya wiki iliyopita aliifanya mkutano na waandishi wa habari na kutoa tamko la serikali na ufafanuzi kuhusu madai ya madaktari hao na bila kumung’unya maneno alisema serikali haiwezi kuwaongezea mishahara na kufikia shilingi milioni 3.5 kwa kuwa kada hiyo inalipwa vizuri.

Dk.Mponda alisema mishara ya watumishi wa serikali hufuata miundombinu ya watumishi iliyopo ambayo iliboreshwa kwa sekta ya afya na hivi sasa watumishi wa afya wanapata mishahara mikubwa kuliko watumishi wengine serikalini.

Ieleweke kwamba baadhi ya madai ya madaktari ni ya msingi na tayari serikali imesema inayafanyia kazi.

Ila sikubaliani na hatua ya madaktari hao kukiuka viapo vyao walivyoapa kuwa wataakikisha wanahudumia wagonjwa katika mazingira yoyote yale lakikini hivi sasa wameamua kuwatoroka wagonjwa nakwenda kufanya migomo na kufanya deiwaka katika mahospitali binafsi ili waweze kujiongezea kipato.

Na kitendo hicho hakina tofauti na jambazi ambaye anamwelekezea bunduki kichwani mwananchi akimtaka ampatie fedha ama sivyo anamuua au akina tofauti na daktari ambaye anamtibu mgonjwa halafu anamwambia hawezi kukupatia dawa hadi unipatie hongo..

Kwanza nakubaliana na maelezo ya Waziri Mponda kuwa suala la kupandishiwa mishahara na masurufi mingine kwa watumishi wa umma kuna utaratibu wake.Wafanyakazi wa serikali wanaodai kuongezewa mishahara na masurufi mengine wanapaswa kufuata utaratibu mahususi ulianishwa ndani ya Civil Service Negotiation Machinery Act, na kama serikali itashindwa kutekeleza madai yao yaliyofuata utaratibu wa sheria sheria hiyo wanaruhusiwa kugoma.

Sasa tuwaulize hawa madaktari walifuata utaratibu ulioanishwa katika sheria hiyo hadi wafikie uamuzi wa kugoma ?

Na kama hawakufuata utaratibu sheria za nchi zipo wazi ambazo zinawabana wale wote wanaofanyakazi au kutoa ushahidi chini ya kiapo na pindi wanapokiuka viapo vyao wanatakiwa waadhibiwe mara moja.

Maana ni wenyewe walieleza kuwa madai yao waliyafikisha wizarani na waziri Mponda akasema aliupokea ujumbe wa chama cha madaktari na wakajadiliana na serikali ikaueleza ujumbue huo kuwa baadhi ya madai yao serikali inayafanyia kazi.

Na baada ya Dk. Mponda kutoa ufafanuzi huo,hatujakisikia chama hicho cha madaktari kikipinga maelezo ya waziri huyo kwa kutoa ushahidi mbadala matokeo yake tunakisikia chama hicho kikisema kuwa hadhi hayo kwa sasa si ya kuongea na waziri huyo ,hadhi yao hivi sasa ni yakuzungumza na waziri mkuu.

Haya Pinda waliokuwa wakimtaka alikwenda Karimjee kuzungumza na madaktari hao lakini madaktari hao walishindwa kutokea kwa sababu za kijinga ambazo sasa zimetulazimu tuanze kuwamini huu siyo mgomo wa madaktari bali unaajenda mbaya nyuma yake.

Hivi nani kairoga nchi hii?Madaktari ndiyo wenye shida na waziri Mponda ndiyo waziri wao lakini cha kushangaza madaktari hao ambao ndiyo wenye shida wamegeuka kuwa manyapara wa kutoa amri ya wanataka nini na nani wazungemze na nani na cha ajabu hadi sasa serikali inaendelea kuwakumbatia?

Nyie madaktari kwa akili zenu waziri alichokizungumza mnafikiri kabla ya kukizungumza huyo waziri mkuu Pinda alikuwa akijui? Waziri wenu kasema serikali inayafanyiakazi madai yenu hamsikii sasa mnataka nini?

Tuulize ule ujumbe wa madaktari uliokiwenda kuzungumza na Dk.Mponda kuhusu madai yao na akawasikiliza, walikuwa hawajui waziri huyo siyo saizi yao na kwamba hana huwezo wa kuwatatulia kero zao?Mlimfuatia nini ?

Ni lini wamegundua waziri Mponda siyo saizi yao? Je ni baada ya waziri huyo kuwaambia ukweli kuwa haitaweza kuwapandishia mshahara?

Na wewe Pinda aibu uliyoipata jana ulijitakia kwani haiwezekani wewe ndiyo Waziri Mkuu Mawaziri wote wapo chini yako na wanakusaidia katika utendaji kazi wako wa kila siku, madaktari hao wanamtolea maneno ya shombo waziri wa Afya Dk.Mponda na maofisa wake ambao ndiyo wenye dhamana ya sekta hiyo, halafu na wewe unakubaliana na upuuzi na dharau hiyo ya madaktari kwa waziri wako , unakwenda kuwaona , na matokeo yake na wewe wamekudhalilisha umejikuta ukumbini peke yako.

Nchi hii hivi sasa si ngazi ya familia wala nje ya familia, hatuheshimiani tunadharauliana bila sababu za msingi. Hajulikani baba ni nani, mama ni nani, mkubwa ni nani,mtoto ni nani na kiongozi ni nani kila mtu anaongea na kufanya analotaka.Na hali hii isipotokomezwa ipo siku taifa hili litajikuta limetumbukia mtoni.

Kwa akili yenu nyie madaktari mliogoma, hivi hayo madai mnayodai ya kupandishwa mshahara ndiyo mtapandi leo leo? Je hizo nyumba mnazodai mjengewe ndiyo ujenzi wake utakuwa umekamilika ndani ya siku mbili?

Lakini wafanyakazi wengine kwa uhalisia wa fani zao walioajiriwa serikali hawawezi kufanyakazi kazi serikali na sekta binafsi kwa wakati mmoja lakini wafanyakazi wa aina hiyo hatujawasikia wakigoma.

Sasa kama hivyo ndivyo ni kwanini madaktari mnaofanyakazi sehemu mbili na mwisho wa mwezi mnapata mishahara miwili.Mbona kule kwenye hospitali za sekta binafsi mnapofanyiakazi hamuwagomeagi mnakuja kuigomea serikali?

Na kama mnaona serikali iliyowaajiri haiwalipi vizuri si mtafute sehemu nyingine ambako mtalipwa vizuri kuliko kung’ang’ania kufanyakazi sehemu ambayo hulipwi vizuri ambapo mwishoe mtakuja kuwaua makusudi wagonjwa kwa kuwachoma sindano za mikojo ili wafe?

Na kama siyo ubinafsi na unafki ni nini, kipindi hicho mmeongezewa mishara na masulufi hatukuwasikia mkijitokeza adharani kutangaza mmeongezewa mishahara?
Watanzania wanaheshimu haki za binadamu sote tuamke tuupinge mgomo huo kwani mgomo huo ni haramu na umeanza kuleta madhara makubwa kwa wananchi wetu ambao hawana uwezo wa kwenda kutibiwa hospitali binafsi na nje ya nchi.

Ieleweke wazi kuwa ni kweli gharama za maisha zimepanda na ukali huo wa maisha unatuhumiza wote lakini hicho kisiwe kigezo cha madaktari wetu kutoroka wagonjwa mahospitali na kwenda kufanya migomo huku wananchi wasiyo na hatia wakipoteza maisha kwa kukosa huduma.

Minaamini kuwa kila mtu awe na elimu na asiye na elimu ana umuhimu hapa duniani na wote tunategemeana hivyo ni vyema na haki madaktari wakaacha na kingizio kuwa taaluma yao ni muhimu kuliko taaluma zingine.

Mwisho nimalizie kwa kuishauri serikali ijenge utaratibu wa kuyashughulikia mapema malalamiko ya kada yoyote inayoyalalamikia kabla ya kada hizo kuanza kujichukulia sheria mkononi na kugoma kwani mwisho wa siku wanaothirika ni wananchi na taifa linajikuta likipata sifa mbaya kuwa taifa la Tanzania hivi sasa limekuwa ni taifa la migomo.

0716 774494
www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Januari 30 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.