Header Ads

MGOMBEA URAIS WA UPINZANI BURUNDI,AFIKISHWA KISUTU

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA mgombea urais wa chama kimoja cha upinzani nchini Burundi, Alex Sinduhnje, jana alifikishwa katika mahabusu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, lakini hata hivyo hakuweza kupandishwa kizimbani.

Sinduhnje ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea, Hurbet Nyange, alifikishwa majira ya saa tatu asubuhi, katika eneo la mahakama hiyo na makachero wa polisi tayari kwa ajili ya kusubiri kupandishwa kizimbani lakini hata hivyo haikuweza kufahamika angefunguliwa mashtaka gani.

Gazeti hili lilipofika saa 6:47 mchana liliwashuhudia makachero wa Jeshi la Polisi wakimuondoa mtuhumiwa mahakamani hapo na kumpeleka polisi kwa kutumia gari aina ya Discovery lenye namba za usajili 280 AEN.

Baada ya hali hiyo kutokea waandishi wa habari za mahakamani walimfuata Mwendesha Mashtaka Kiongozi wa Mahakama hiyo, Elizabeth Kaganda, ili kupata ufafanuzi ni kwa nini hajapandishwa kizimbani, na kusema kuwa baadhi ya taratibu za kisheria zilikuwa hazijakamilika.

“Kwa kuwa taratibu za kisheria kuhusu tuhuma zinazomkabili Sinduhnje hazijakamilika ofisi yangu imeliagiza Jeshi la Polisi kwenda kufanyia marekebisho hayo na kuondoka na mtuhumiwa huyo na kwenda kumhifadhi katika mikono yao na pindi taratibu hizo zitakapokamilika hatua nyingine zitafuata,” alisema Kaganda.

Kufikishwa kwa Sinduhnje mahakamani hapo, kulimfanya Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila, kufika kwa ajili ya kumsaidia, lakini alidai kuwa makachero wa polisi walimkataza asiende kuzungumza na mtuhumiwa huyo hali iliyomfanya Mtikila kukaa kwenye chumba cha mawakili kwa ajili ya kusubiri taratibu zilizokuwa zikiendelea dhidi ya mshtakiwa huyo.

“Huyu Sinduhnje ni mpinzani ambaye amemsumbua sana Rais wa Burundi, Pier Nkurunzinza, katika uchaguzi uliopita na nimepata taarifa kuwa serikali ya Tanzania inataka imrudishe Burundi na mimi maoni yangu sitaki arudishwe kwao kwani akirudishwa kule anaenda kukatwa kichwa,” alisema Mtikila.

Mtikila alisema kwa taarifa alizonazo ni kwamba serikali ya Burundi inamtaka mtuhumiwa huyo arudishwe Burundi ili akakabiliane na kesi za kubambikwa za mauji kwani uchaguzi ulipomalizika alikimbilia Ulaya akakaa huko na ndiyo hivi karibuni kaingia hapa nchini na kukamatwa, haelewi kama mtuhumiwa huyo aliua kwa kutumia simu au intaneti.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Januari 14 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.