Header Ads

UGUMU WA MAISHA UTATUANGAMIZA


Na Happiness Katabazi

KARIBU kila pembe ya nchini hii wimbo wa gharama za kupanda kwa maisha na mfumuko wa bei umezidi kushika chati katika mawazo na midomoni mwa wananchi wengi.


Wananchi tulio wengi hususani sisi wenye maisha ya hali ya chini tumekuwa tukisurubika na hali hiyo huku tukiona hakuna jitihada za mara moja zinazofanywa na serikali au wamiliki wa makampuni ya sekta binafsi wakikabiliana na hali hiyo.

Matokeo yake wafanyakazi wanaofanya kazi katika serikali, sekta binafsi na wale wasio na ajira za uhakika na wamekuwa wakiimba wimbo huo wa kukabiliwa na hali ngumu ya maisha .

Kwa sisi wanawake ambao mara kwa mara ndiyo tunakwenda kununua bidhaa katika masoko na madukani ndiyo tumekuwa tukishuhudia moja kwa moja upandaji wa bei za nafaka katika kipindi kifupi tu na ukimuuliza muuzaji ni kwanini wiki iliyopita nimekuja kununua mchele au maharage kwa bei ile na leo umepandisha bei kiasi hiki.

Muuzaji anaishia kukupa jibu la mkato kwamba gharama za maisha zimepanda na kwamba kama unataka kununua bidhaa zake nunua hutaki nenda katika masoko mengi.

Mtu unakuwa huna jinsi inabidi ununue bidhaa hiyo kwa huku ukinung’unika moyoni.
Tumewasikia viongozi wa serikali wakitoa bei ya sukari kwa wauzaji kuwa washushe bei hiyo toka shilingi 2500 kwa kilo moja na waizue kwa shilingi 1,700.Lakini maagizo hayo yameshindwa kutekelezeka na wauzaji hao matokeo yake bei ya kilomoja ya sukari inauzwa sh 2500.
Lakini kwa kuwa shida ni mwalimu sisi malofa hivi sasa tunakimbila maduka ya Shoprite kununua sukari kwasababu bei yake ina unafuu.Katika maduka hayo kilo moja ya sukari ni shilingi 1,900.
Kwa maoni yangu serikali kupitia wachumi wake kama hawatakaa kitako na kuweka mikakati ya taifa lake kukabiliana na hali hii, basi ijiandae kuona baadhi ya nguvu kazi yake kubwa mwisho wa siku ikishindwa kuzalisha kutokana na sababu mbalimbali.
Ikiwemo maradhi ya kuambukiza kama ukimwi, magonjwa ya moyo na wananchi wake kuamua kujitumbukiza kwenye vitendo haramu kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya mkato na mwisho wa siku wakajikuta wakiangukia kwenye mkono wa dola.
Hivi sasa huko mitaani kuna vijana ambao hawana elimu na wengine wenye elimu tena wengine wapo vyuoni, nao wamekuwa wakilalamikia hali hilo hali inayowasababisha wengine kushindwa kujizuia na kuamua kujitumbukiza kwenye kufanya ngono zembe ili waweze kupata fedha za kuendeshea maisha yao.
Na siyo kundi hilo pia kuna baadhi ya wake za watu nao bila haya wamekuwa wakisaliti ndoa zao na kwenda kufanya mapenzi na wanaume wengi ili waweze kupata fedha za kuendeshea maisha yao kwa kisingizio kuwa waume zao fedha wanazowapatia ni ndogo.
Pia kuna wa mama watu wazima nao wamekuwa wakitumia fedha zao kuwarubuni vijana wadogo wa kiume kufanya nao mapenzi kwa kuwahonga fedha ili waweze kuwatimizia haja zao za kimapenzi.

Licha tabia hizi chafu hazikuanza leo zimeanza siku nyingi lakini hivi sasa zimeshika kasi na zinafanyika kwa uwazi bila kificho kwa kila mmoja wao kutumia udhaifu wa mwenzie uwe wa kimapenzi au kifedha.

Tukiachana na hilo hivi sasa mitaani kutokana na baadhi ya vijana kutaka kujipatia fedha kwa njia za mkato na kukata tamaa,miongoni mwao mitaani wamekuwa wakiishi maisha ya kifahari kuliko hali halisi zinazowazunguka na wengine wamekuwa wakinyoshewa vidole kuwa wanajiusisha na kufanyabiashara haramu kama kuuza unga kwa kigezo cha kujifanya wao ni wafanyabiashara wa kwenda kununua bidhaa kama nguo nje ya nchi na kuzileta hapa nchini.

Ni rai yangu pia kwa waendeshaji wa maofisi ya sekta binafsi nao wabadilike hivi sasa wasiangalie faida tu wanayoingiza tu makampuni na viwanda vyao pia wakae chini watafakari ni jinsi gani wanaboresha maisha ya wafanyakazi wao kwani hakuna ubishi mfumuko wa bei pia unawaathiri hata wafanyakazi wa sekta binafsi.

Pia na serikali nayo iweke utaratibu sasa huko mbele ya safari wa kuweza kuwabana wauzaji wa bidhaa mbalimbali ambao kila kukicha wanapandisha bei kwani hiki kisingizio cha serikali cha soko huria ndiyo maana inashindwa kuwabana ipo siku watu watachoka kukisikia.

Na pia serikali iendelee kupanua wigo wa ajira za uhakika kwa vijana ili waweze kuondoka vitendo hivyo haramu ambavyo mwisho wa siku vitafupisha maisha yao.

Tunaamini serikali yoyote makini ina uthubutu na ina mkono mrefu na inapoamua jambo lake lifanyike na litekelezwe, linatekelezwa sasa ni sisi wenyewe tumeridhia serikali yetu ituongoze hivyo serikali hii haina budi sasa kuakikisha inaweka taratibu za kuweza kukabiliana na hali hii ya wananchi wengi kuimba wimbo huu wa ukali wa maisha.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Januari 10 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.