Header Ads

MLIOADHIBIWA UDSM MMEVUNA MLICHPANDA


Na Happiness Katabazi

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Profesa Rwekaza Mukandala ,Januari 10 mwaka huu alitangaza kuwafukuza chuo wanafunzi 13 akiwamo Spika wa Serikali ya Wanafunzi(DARUSO), Peter Arnold na wengine 86 kuwasimamisha miongoni mwao ni Rais wao, Kilawa Simon.


Hatua hiyo ilifikia baada ya hali katika chuo hicho kuwa tete kwa siku tatu mfululizo baada ya wanafunzi wa DARUSO kufukuzwa chuo siku hiyo kwa shinikizo la kuanzisha mgomo wenye nia ya kuwarejesha wenzao 48 na wanne waliosimamishwa Desemba mwaka jana.

Aidha kwa kipindi cha Desemba mwaka jana hadi sasa ni wanafunzi 61 waliofukuzwa na 90 kusimamishwa wakipisha uchunguzi kufanyika na ikigundulika wana makosa watafukuzwa na na watakaoonekana kutokuwa na makosa watarejeshwa kuendelea na masomo.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema maneno yafuatayo kwamba ‘ukweli una tabia moja nzuri sana hauchagui rafiki wala adui’.

Hivyo kwa nukuu hiyo ya Baba wa Taifa kwanza nafahamu wazi mtazamo huu hautawafurahisha wanafunzi waliofukuzwa na kusimamishwa lakini naomba wanivumilie.
Ikumbukwe kuwa Tanzania ni nchi ambayo inajiongoza kwa utawala wa sheria hivyo kila mwananchi na viongozi wetu wanapotenda kazi au kufanya mambo yao lazima wahakikishe wanafuata na kuzingatia taratibu zote za kisheria.

Hivyo basi hata wale wanafunzi vyuoni hasa baadhi ya wanafunzi wa UDSM pindi wanapokuwa na madai yao wanapaswa kufuata taratibu zote za sheria zilizoanzisha vyuo vyao na sheria nyingine za nchi kudai madai yao na siyo kuamua kujichukulia sheria mkononi kwa kuanzisha migomo haramu, kufunga barabara na kuwacharaza bakora wanafunzi wenzao ambao hawawaungi mkono katika hiyo migomo yao haramu .

Labda tuwakumbushe hao wanafunzi wa UDSM kwamba sheria ni msumeno.Na pindi sheria inapoanza kutumiwa dhidi ya wavunja sheria haibagui kuwa huyu ni mwanachuo asishtakiwe mahakamani au kuadhiwa kwa njia yoyote ile au huyu ni maskini.

Pale UDSM kuna wanafunzi ambao wanafahamu vyema kilichowapeleka pale ni masomo na wengine nafikiri hivi sasa wamesahau kilichowapeleka pale na matokeo yake wamekengeuka na kuanza kila kukicha kuanzisha vurugu kwa kisingizio cha hali ngumu ya maisha kwa Bodi ya Mikopo haijawaingia fedha kwenye akaunti mara wale wenzao wanaokabiliwa na kesi ya mkusanyiko haramu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Desemba mwaka jana eti warudishwe chuo wakati wengine wamesimamishwa na wengine kufukuzwa.

Hivi nyie wanachuo mliokuwa mkiendesha huo mgomo haramu wiki iliyopita aliyewaambia UDSM ina mamlaka ya kuwafutia kesi wanafunzi hao nani?Kwanini msingeenda kumvamia Hakimu Waliarwande Lema anayesikiliza kesi hiyo au ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP), Dk.Elizer Feleshi kuwashinikiza wafute hiyo kesi kwani ndiyo hasa wenye mamlaka hayo?Ni kiwaita nyie ni wabaguzi na mnalenu jambo nitakuwa nimekosea?

Wale wanafunzi wanaokabiliwa na kesi si watanzania kama wale watanzania wengine ambao kila kukicha wanafunguliwa kesi mahakamani na wengine wanazeekea magerezani, mbona hatujawahi kuwasikia mkijitokeza kuandaa mgomo kushinikiza nao wafutiwe kesi?Maana kinachotuunganisha sisi Utanzania wetu.

Imeanza kuonekana ni kawaida sasa kusikia kila kukicha wanafunzi wa hasa wale wa UDSM wakigoma bila kufuata taratibu na hakuwa hata mzazi mmoja au wale wanaojiita wanaharakati kujitokeza kukemea vitendo hivyo vya ufunjifu wa amani na utovu wa nidhamu unaofanywa na wanafunzi hao kwa kigezo kuwa wanakabiliwa na matatizo mengi likiwemo la bodi ya mikopo kuwacheleweshea fedha zao.

Ieleweke kwamba ni wanafunzi hawa hawa siku za mbele ndiyo wanaweza kuwa viongozi katika taasisi za serikali,siasa na sekta binafsi sasa inapotokea leo hii wanafunzi hawa leo hii hawajahitimu masomo wala kutwaa madaraka wanaanza kufanya vitendo vya kidikteta vya kuwacharaza bakora wanafunzi wenzao ambao hawataki kugoma,inasikitisha na kutisha sana.
Hapo zamani wanafunzi wa UDSM walikuwa ni wanafunzi ambao walikuwa wakishiriki kwenye midahalo na kutoa fikra zao ambazo zilikuwa zikileta changamoto kwenye jamii, licha kulikuwepo pia migomo licha haikuwa ya mara kwa mara kama hii.

Lakini leo hii hayo hayapo tena kwani kuna taarifa za kuaminika kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakitumiwa na wanasiasa kuanzisha migomo mara kwa mara na bila kufuata taratibu na wanafunzi wengine wanafuata mkumbo na kusahau kuwa kilichowapeleka pale ni kusoma na siyo kutumiwa na wanasiasa na kuanzisha migomo.

Na nyie wanafunzi mnaokubali kutumiwa na wanasiasa mkae mkijua hapo chuoni ulikwenda peke yako na utaondoka peke yako hivyo siku ukifukuzwa chuo hao wanasiasa hawatawasiadia lolote kwani mkae mkijua UDSM ina sheria zake ndogo ndogo ambapo pindi uongozi wa chuo ukiamua kuzitumia ni wazi wale wanafunzi ambao wanashiriki kwenye vitendo vya uvunjifu wa sheria watafukuzwa na hasara wataipata wao na familia zao.
Misioni mankiti
ya wanafunzi hao kila kukicha kuzua migomo, kutoa lugha chafu na kuwachara bakora wenzao na kuwatoa madarasani kwa kigezo kuwa wanashinikiza bodi iwaingizie fedha kwenye akaunti kwa muda wanaoutaka wao wakati wanafunzi hao hao wengine wanawazazi ambao wanauwezo wa kuwalipia ada lakini hawawalipii ada lakini wanafunzi hao hatujawasikia wakiwaletea vurugu au kuwapiga baba zao kwa kigezo cha kushindwa kuwalipia ada.

Tujiulize leo hii ni wanafunzi wangapi ambao wamekosa fursa ya kulipiwa ada ya vyuo vikuu na bodi ya mikopo lakini wanafunzi hao wanasoma katika mazingira magumu sana na wamegeuka kuwa matonya wa kuomba ada huku na kule kwenda kulipa vyuoni lakini hata siku moja hatujawasikia wanafunzi hao wakifanya vurugu?

Ni baadhi ya wanafunzi hawa hawa wa UDSM mwishoni mwa mwaka jana siku ile ya Sherehe ya miaka 50 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Uganda Yoweli Mseveni walikuwepo kwenye sherehe hizo lakini wanafunzi hawa kwa kukosa nidhamu walimzomea kwa mabango rais Kikwete.

Rais Kikwete alivumilia hali hiyo na aliendelea na maadhimisho hayo na ilipofika wakati wa kutoa hotuba yake alisoma hotuba yake ambayo ilionekana kutoa matumaini mapya ya maendeleo kwa chuo hicho kwani ndani ya hotuba hiyo alisema serikali yake itatenga fedha kwaajili ya upanuzi wa ujenzi wa majengo wa chuo hicho hali iliyosababisha wale wale waliokuwa wakimzoea nao kuanza kumpigia makofi.

Katika mila na desturi za Afrika na jamii iliyostaarabika ni lazima mtoto awe na heshima kwa mkubwa wake , lakini kwa kile kitendo kilichofanywa na baadhi ya wanafunzi wale kumzoea rais wan chi Kikwete siku hiyo ni dhahiri kwa watu tunaotazama mbali, kitendo kile kilituthibitishia kuwa wale wanafunzi waliofanya kitendo kile ni wahuni,wasiyoheshimu wakubwa na viongozi na kuwa uenda hata majumbani kwao hawawaheshimu wazazi wao.

Ifike mahala sasa uongozi wa Chuo Kikuu chini ya Profesa Mukandara uamke na kuanza kurejesha na kutetea heshima ya UDSM kwa kuwashughulikia bila huruma wanafunzi wote wanajihusisha na vitendo vya uvunjifu wa sheria chuoni hapo kwa madai kuwa wanakabiliwa na maisha magumu kwani hakuna ubishi kwamba chuo hicho hivi sasa ndani ya nchi za Afrika Mashariki kimeanza kuwa na sifa mbaya ya wanafunzi wake kuanzisha migomo kila kukicha badala ya kuingia madarasani kusoma.

Chuo KIkuu cha Dar es Salaam, kina historia ndefu na kimezalisha wasomi wengi na wazuri ambao hivi sasa wanatamba katika nchi nyingi duniani, sasa serikali na Profesa Mukandara msikubali sifa hiyo ya kitaaluma iliyokuwa nacho chuo hicho ipotee kwaajili ya wanafunzi wachache ambao wana hulka za kihuni ambao wanapoteza muda mwingi wa kuandaa maandamano badala ya kujisomea.

Ni kweli chuo hicho kinakabiliwa na changamoto kadhaa kama uchache wa mabweni, miundombinu ya majitaka,madara na mengineyo lakini changamoto hizo zisiwe kigezo cha wanafunzi hao kudai kwanjia ya uvunjifu wa sheria kutatuliwa kwa changamoto hizo.
Nawataka nyie wanafunzi ambao mnadai mnadai haki zenu kwa njia ya migomo haramu mtambue kuwa hata sisi tunaofanyakazi maofisi tena tunafamilia zinatutegemea pia na sisi tunakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo zinatakiwa zitatuliwe na wamiliki au viongozi wa maofisi tunayofanyia kazi, lakini sisi wafanyakazi tumekuwa tukifuata taratibu na njia za amani kufikisha vilio vyetu vya kutaka changamoto hizo zitatuliwe na kweli wakati mwingine zinatatuliwa na nyingine hazitatuliwi kwa muda tunautaka sisi na tunavumilia.

Nimalizie kwa kuwaasa kuwa kumbukeni kuwa nyie baadhi ya wanafunzi mnaoshiliki kwenye migomo kila kukicha pale UDSM ni kusoma na siyo kutumiwa na wanasiasa au kudai haki zenu kwanjia ya uvunjifu wa sheria za nchi mkae mkijua mwisho wa siku mtaangua kwenye mikono ya dola na mtashughulikuwa kama wanashughulikiwa watuhumiwa wengine ambao si wanafunzi.

Kwani inasikitisha sana kuona mzazi kwa moyo mweupe anamruhusu mtoto wake aende kusoma UDSM halafu mtoto huyo anafika chuoni hapo anasahau kilichompeleka pale na dhiki za nyumbani kwao anaanza kujiingiza kwenye makundi ya wanafunzi wapuuzi ambao wanachowaza ni migomo kuliko kusoma mwisho wa siku mzazi anasikia mtoto wake amekamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa makosa ya mkusanyiko usiyo halali au kusimamishwa shule au kufukuzwa chuo kabisa.Kwa kweli inaumiza sana.

Na ndiyo maana katika makala yangu ninawaasa wazazi,vyombo vya habari ambao si tu wana watoto wanaosoma pale UDSM kuanza kuwakemea wanafunzi wanaoshiriki kufanya uhuni huo kuliko kila kitu kuuachia uongozi wa chuo na serikali kuwakemea wanafunzi wanaotenda vitendo hivyo kwani kushindwa kufanya hivyo ndiyo kunasababisha wakati mwingine wanafunzi hao kuwa na jeuri ya kuendelea kutenda vitendo hivyo kwani hakuna watu wa kuwakemea.

Leo hii kuna baadhi ya wazazi au wafanyakazi waliojaliwa kuwa na kipato kikubwa wameamua kutotaka watoto wao wakasome UDSM kutokana na uhuni huo ambao ni wazi na taratibu unaanza kuporomosha heshima ya chuo mbele ya jamii jambo ambalo ni hatari kwa chuo kama hicho ambacho kinamilikiwa na serikali yetu.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne,Januari 17 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.