Header Ads

LIYUMBA AOMBA AFUTIWA KESI

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi ya kukutwa na simu akiwa katika gereza la Ukonga, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, iifute kesi hiyo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza.

Kesi hiyo ambayo inasikilizwa na Hakimu Mkazi, Stewart Sanga, jana ilikuja kwa ajili ya kusikiliza pingamizi lililowasilishwa na wakili wa Liyumba, Majura Magafu, kwa ajili ya kuwasilisha pingamizi ambalo linataka mteja wake afutiwe kesi hiyo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kwa sababu taratibu za awali za sheria ya Magereza ya mwaka 2002 hazikufuatwa.

Wakili Magafu alidai kwa mujibu wa sheria ya magereza ya mwaka 2002 inataka mshtakiwa anayeishi mahabusu kabla hajaletwa mahakamani asomewe mashtaka na ofisa wa magereza hukohuko gerezani na endapo atapatikana na hatia atapewa adhabu na aendapo mshtakiwa huyo ataonekana amekuwa mtendaji sugu wa makosa akiwa gerezani ndipo italazimika afunguliwe mashtaka katika mahakama za uraiani.

Akipangua hoja za upande wa utetezi Wakili wa Serikali Eliezabeth Kaganda alianza kwa kusema kuwa kesi ya aina hiyo inayomkabili Liyumba siyo ya kwanza kufunguliwa katika mahakama za hapa nchini.

Kaganda aliitaja kesi ya jinai Na. 472/2009 iliyokuwa ikimkabili Juma Matonya katika Mahakama ya wilaya ya Temeke ambapo hakimu Mzava alimhukumu kifungo cha miezi sita jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukutwa na simu gerezani.

Na kesi nyingine mbili za aina hiyo hiyo, ambazo washtakiwa walitiwa hatiani moja akitakiwa alipe faini ya shilingi 20,000 na nyingine kwenda jela miezi sita.

“Kwa kesi hizo ambazo ni mifano hai, upande wa jamhuri unapinga hoja ya wakili ya utetezi inayotaka sisi tulete vielelezo kuonyesha hatua zilizofanyika kwa kuwa kuna mashahidi wa upande wa mashtaka watakaokuja kueleza kila kitu,” alidai wakili Kaganda.

Wakili Kaganda alieleza kuwa kabla hawajamfikisha Liyumba mahakamani hapo Jeshi la Magereza lilikuwa na mamlaka ya kushughulikia tuhuma zilizokuwa zikimkabili mshtakiwa na kwamba mkurugenzi wa mashtaka, na maofisa wa magereza walikuwa wameishaamua kuifungua kesi hiyo mahakamani hapo, kwa sababu hiyo haikuwa mara ya kwanza kukutwa na simu gerezani na alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa shinikizo la damu hivyo haikuwa rahisi kumpa adhabu akiwa gerezani.

Aidha akijibu hoja za Kaganda, wakili Magafu alieleza kwa kudai kuwa kwanza anamshukuru wakili huyo kukubali hoja yake ya maofisa wa magereza kuwa alikuwa na mamlaka ya kushughulikia tuhuma zilizokuwa zikimkabili mshtakiwa.

Magafu aliipinga hoja ya wakili huyo wa serikali kuwa mshtakiwa alipokuwa gerezani alikuwa ni mtendaji sugu wa makosa hayo ya kukutwa na simu gerezani lakini eti magereza ilishindwa kumwadhibu kwa sababu alikuwa anaugua ugonjwa wa shinikizo la damu kwa sababu haina ushahidi wowote kwani hata kama ni kweli alikuwa akiyatenda makosa hayo hakuna ushahidi unaonyesha alishawahi kufikishwa mbele ya maofisa wa magereza na kuchukuliwa hatua.

Akizungumzia kuhusu kesi zile tatu zilizotolewa hukumu na mahakama ya Temeke, wakili Magafu alidai kuwa upande wa utetezi haufahamu kesi hizo zilifunguliwa katika mazingira gani hivyo Kaganda alipaswa alete nakala za hukumu hizo ili waweze kuzisoma.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Stewart Sanga alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili na kwamba atakuja kutoa uamuzi wake Januari 27 mwaka huu.

Septemba 8 mwaka jana, kwa mara nyingine tena Liyumba alifikishwa mbele ya hakimu Sanga akikabiliwa na kosa la kukutwa na kitu kilichokatazwa gerezani chini ya kifungu cha 86 (1,2) cha sheria ya Magereza kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Wakili Kaganda alidai kuwa Liyumba ambaye wakati huo alikuwa ni mfungwa mwenye Na.303/2010, Julai mwaka jana, ndani ya gereza la Ukonga, alikutwa na simu ya Nokia Na.1280 nyeusi iliyokuwa na laini yenye Na. 0653-004662 na IMEI Na. 356273/04/276170/3 ambayo alikuwa akiitumia kufanyia mawasiliano binafsi wakati ni kinyume cha sheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Januari 14 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.