Header Ads

WANNE UDSM WAENDA JELA KWA KUKOSA DHAMANA

Na Happiness Katabazi

WANAFUNZI wanne kati ya 51 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wanaokabiliwa na kesi ya kufanya mkusanyiko haramu wamepelekwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti ya dhamana waliyopewa.

Waliopelekwa rumande ni Elias Mwambapa, Alphonce Lusako, Moris Denis na Jabir Ndimbo ambao walishindwa kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika na kusaini hati ya dhamana ya Sh 1 milioni kwa kila mshtakiwa.
Hatua hiyo ilikuja baada ya uongozi wa Chuo hicho Kikuu cha Dar es Salaam kujivua udhamini wa wanafunzi 41 kati ya 51, Desemba 20, mwaka jana.

Wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Waliarwande Lema kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Kaganda alidai kuwa jana kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali na kupeleka wadhamini wapya baada ya uondozi wa chuo kujitoa.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, hakimu Lema aliiahirisha kesi hiyo hadi Januari 23, mwaka huu watakaposomewa maelezo ya awali yanayohusiana na kesi yao.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa wa 31, anadaiwa kuwa si mwanafunzi wa chuo hicho, bali ni kibaka aliyetumia jina la mwanafunzi wa chuo hicho la Said John wakati jina lake halisi ni Hassan Suleiman hata hivyo ilibainika kuwa anakabiliwa na kesi nyingine katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni.
Awali, Ambinyiel Maro akiwasilisha barua kutoka kwa uongozi wa chuo hicho mbele ya Hakimu Stewart Sanga alidai kuwa uongozi wa chuo unajivua udhamini kwa wanafunzi 41.

Mahakama hiyo ilipokea maombi hayo, lakini Hakimu Sanga alisema anatoa nafasi mpaka Januari 10, mwaka huu kwa wanafunzi hao 41 kutafuta wadhamini wengine kuliko kuwarudisha rumande.

“Kisheria haitakuwa haki kupokonya udhamini kwa washitakiwa hao kwasababu imekuwa ni ghafla leo hawakujiandaa , hawakujua kama kuna barua hiyo,” alisema Hakimu huyo.

Alitoa tahadhari kwa wanafunzi hao kujiandaa kupeleka wadhamini kwa masharti yale yaliyowekwa awali na ambaye hatayekuwa hana mdhamini atakuwa amevunja masharti ya
dhamana, hivyo ataenda rumande.

Novemba 14, mwaka huu, wanafunzi hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kudaiwa kuwa katika eneo la Mlimani, kwa pamoja walifanya mkusanyiko usio wa halali na kusababisha uvunjifu wa amani katika eneo hilo.

Shitaka jingine walidaiwa kukaidi amri ya askari walipoambiwa watawanyike. Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala wiki iliyopita alifafanua kuwa kati ya wanafunzi 51 waliokuwa wamefikishwa Kisutu, 43 kati yao ndio waliofukuzwa, watatu sio wanafunzi wa chuo
hicho, tisa hawajasikilizwa na Baraza la Chuo hicho na kutolewa mapendekezo.

Alisema matukio yaliyojiri ni mwendelezo wa matukio ya uvunjifu wa amani ambapo kila mara vitendo hivyo vilianzishwa na kikundi kidogo cha wanafunzi na hatimaye kupata wafuasi katika kuvuruga shughuli za chuo.

Alisema madai ya wanafunzi waliokuwa wakiendesha vurugu hizo, yamekuwa yakibadilika kila kukicha ambapo mwanzo walidai mikopo ya wanafunzi waliochaguliwa katika mwaka huu wa masomo na ambao hawakupata mikopo, baadaye dai kubwa likawa ni kuachiwa huru wenzao waliokamatwa na kufunguliwa mashitaka kutokana na kuendesha maandamano kinyume cha sheria na kukaidi amri ya Polisi ya kutawanyika.

Profesa Mukandala alisema katika siku mbili za vurugu madai ya awali yalikuwa kuondolewa kwa adhabu za kinidhamu walizopewa wenzao wachache kwa mujibu wa Kanuni na Sheria za Chuo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Januari 12 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.