Header Ads

RAIA WA BURUNDI KORTINI KWAKUKUTWA NA RISASI 682

Na Happiness Katabazi

RAIA wa Burundi, Ismail Stefano (39) jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka ya kukutwa na silaha mbili aina ya SMG na risasi 682.

Mbele ya Hakimu Mkazi Ritha Tarimo Wakili wa Serikali Cecilia Mkononga alidai kuwa Januari 5, mwaka huu katika stendi ya mabasi yaendayo mikoani ya Ubungo, mshtakiwa huyo alikamatwa akiwa na SMG mbili pamoja na risasi 682 kinyume na kifungu cha 4(1) na 34(1),(2) cha sheria ya Umiliki wa silaha sura ya 223 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Mkononga alidai kuwa silaha hizo alizokamatwa nazo mshtakiwa akizimiliki bila ya kuwa na leseni inayomruhusu kufanya kumiliki , na zilikuwa na namba UC-99611998 na nyingine namba 1992-AET 3837.

Alidai kuwa siku hiyo aliyokamatwa , mshtakiwa huyo pia alikutwa akimiliki risasi hizo 682 wakati akiwa hana kibali kinachomruhusu kuzimiliki.
Hata hivyo mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamalika hivyo wanaiomba mahakama ipange tarehe ya kutajwa.

Akitoa masharti ya dhamana Hakimu Tarimo alimhoji mshtakiwa huyo kuwa ni mwenyeji wa wapi ambapo mshtakiwa huyo alijibu kuwa yeye ni mzaliwa wa Mkoa wa Kigoma na wazazi wake kabila lao ni Wahutu na wakimbizi toka nchini Burundi waliongia nchini mwaka 1972 na kwamba wakati wanaingia nchini mama yake alikuwa na ujauzito wake hivyo yeye amezaliwa mkoani Kigoma.

Aliendelea kudai kuwa licha ya yeye kuzaliwa mkoani Kigoma pia ana uraia wa Tanzania lakini vinashikiliwa na jeshi la polisi na kusisitiza kuwa yeye ni raia wa Tanzania.

Hakimu huyo aliendelea kumuuliza mshtakiwa huyo kuwa anakaa wapi , ambapo alijibu Katumba Mpanda na kuongeza kuwa alikuja Jijini Dar es Salaam na lengo lake ni kufikia nyumba ya kulala wageni.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Wakili Mkononga aliiomba mahakama wakati inapotoa masharti ya dhamana izingatie kuwa mshtakiwa huyo haelewi uraia wake kama ni mtanzania au la.

Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Ritha alimtaka mshtakiwa huyo awe na wadhami watatu wanaominika , wanaoishi Dar es Salaam, mmoja wao awe mfanyakazi wa serikali lakini asiwe mwalimu.

Hata hivyo mshtakiwa huyo alishindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana na hakimu akaamuru apelekwe gerezani hadi Januari 24 mwaka huu kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 11 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.