MNALENU JAMBO,SIO BEI MPYA YA KIVUKO
Na Happiness Katabazi
MWISHONI mwa wiki iliyopita Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alitangaza kupanda kwa nauli za vivuko hususan vivuko vya serikali vya Kigamboni.
Alisema kuanzia siku hiyo abiria wangeanza kulipa nauli ya sh 200 badala ya sh 100 ya zamani.
Hata hivyo tangazo hilo lilionekana kuwakera baadhi ya watumiaji wa huduma hiyo na wengine kufikia hatua ya kumtolea maneno yasiyofaa na kupinga wakati abiria wengine wakitekeleza agizo hilo kwa vitendo kwa kuanza kutumia huduma hiyo kwa nauli mpya.
Baada ya baadhi ya wananchi kulipinga tangazo hilo, Magufuli aliwapasha wananchi hao kwamba asiyetaka kulipa nauli mpya ajifunze kupiga mbizi au asitumie kivuko hicho na badala yake azungukie Kongowe.
Aidha juzi tulishuhudia baadhi ya wabunge wa Dar es Salaam wakinukuliwa na vyombo vya habari wakiishutumu kauli ya Magufuli na kudai kwamba upandaji wa nauli utawaumiza abiria na kuomba uongozi wa juu wa nchi kumuonya waziri kutokana na maamuzi ya kupandisha nauli.
Binafsi naunga mkono tangazo la Waziri Mafuguli la kupandisha nauli na ushauri alioutoa kwa abiria wanaopinga ongezeko hilo la nauli kwamba kama hawataweza kulipa basi wajifunze kupiga mbizi au wazungukie Kongowe.
Nimelazimika kuunga mkono agizo hilo kwa sababu Watanzania wengi tunapenda kuambiwa uongo na viongozi wetu, hivyo anapotokea kiongozi anayetuambia ukweli ili tujiandae kukabiliana na utekelezwaji wa ukweli huo, huwa tunamuona ni mbaya na hafai.
Kutokana na tabia hii ambayo imejengeka akilini mwetu, ndio maana nyakati za uchaguzi, wagombea wengi wa ubunge, urais na udiwani toka vyama vya siasa wamekuwa wakitumia uongo kunadi sera zao na hatimaye wananchi wanaopenda kudanganywa huona wanasiasa hao wanafaa na kuwapa kura za ndiyo.
Nina uzoefu na hilo nililolisema kwani nimezunguka nchi nzima mara tatu na wagombea wa urais toka vyama mbalimbali na baadhi ya ahadi walizokuwa wakizitoa kwenye majukwaa zilikuwa hata hazimo kwenye ilani za vyama vyao.
Nakumbuka kampeni za urais mwaka 2005, ahadi mbalimbali zilitolewa na viongozi wa kisiasa kama vile kila kata kungejengwa chuo kikuu; maisha bora kwa kila mmoja; milo mitatu kwa kila mtu; pamoja na wananchi kusoma bure hadi chuo kikuu.
Wakati viongozi hao tofauti wakitoa ahadi hizo kwenye mikutano ya hadhara tulikuwa tukiwashangilia sana lakini leo hii tumegeuka na kuanza kuwashambulia kwa ahadi hizo.
Sasa kwa muktadha huo nawataka wananchi tunaotumia kivuko cha Kigamboni tujiulize hivi katika akili zetu siku zote za maisha tulikuwa tukifikiri ile nauli ya sh 100 ya kivuko haitapanda?
Ni nyie abiria mliokuwa mkilia usiku na mchana kuhusu ubovu wa kivuko cha zamani na hatimaye alipoingia madarakani Rais Jakaya Kikwete na serikali yake wakafanya jitihada hadi wakawaletea kivuko kipya cha Mv. Magogoni; leo hii mnavuka usiku na mchana na kwa usalama zaidi kwa sababu kivuko hicho kipya ni cha uhakika.
Lakini hamjiulizi serikali ilipataje fedha hadi ikawaletea kivuko hicho hapo Kigambo?
Inashangaza kwa ongezeko hilo la nauli ambayo kwa sasa ni sh 200 hadi mnataka kuandamana wakati bidhaa na huduma mbalimbali zimepanda bei kama nafaka, dawa, kondomu, matibabu, vinywaji, nauli za kwenda mikoani, ada na vifaa vya shule.
Wabunge wa Dar es Salaam mnaoingilia kati jambo hili, napenda kutoa ushauri wa bure kwenu kwamba tekelezeni ile dhana ya uwajibikaji wa pamoja na achaneni na porojo za kisiasa.
Naamini Magufuli sio chizi kwa kutoa agizo lile, hivyo ni vema na mna haki, wabunge kwenda ofisini kwa Magufuli kimya kimya ili awaeleze sababu zilizosababisha yeye kufikia uamuzi huo na sio kujitokeza hadharani na kuanza kumhukumu kuwa anatumia madaraka yake vibaya kupandisha nauli.
Sote tunafahu waziri ana mamlaka ya kutunga sheria ndogondogo muda wowote anapoona inafaa.
Serikali kupitia Magufuli haijawalazimisha mtumie kivuko hicho, hivyo wale wanaopenda kutumia kivuko hicho kwa nauli mpya watumie na wasiotaka watafute njia nyingine.
Magufuli aliposema kama hamtaki kulipa bei mpya basi mjifunze kupiga mbizi au kuzungukia Kongowe sio lugha ya kuudhi, bali ametoa ushauri mzuri tu.
Kwa nini Watanzania hatupendi mtu anayeliita jembe ni jembe? Kwa nini tunawapenda watu wanaotudanganya kwa kanga, pilau na kofia wakati wa uchaguzi wakati tunajua ni waongo?
Magufuli tafadhali kaza uzi! Na nyie wanasiasa wa Dar es Salaam acha unafiki na uzandiki.
Kama hili la kupanda bei limewakera andikeni michanganuo kwa hao wafadhili wenu wanaowachangieni hela za kampeni kisirisiri ili muweze kununua kivuko binafsi ili wananchi waweze kupanda bure kama mtaweza!
Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
0716 774494 www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 4 mwaka 2011.
1 comment:
una lako jambo
Post a Comment