KIFO CHA DK.SENGONDO MVUNGI KIMENIUMA
Na Happiness Katabazi
NOVEMBA 12 mwaka 2013, saa 10 jioni nikiwa darasani katika Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UB) nasubiri mwalimu wa somo la Criminal Law aingie kufundisha , mwanafunzi mwenzangu wa sheria ambaye ni Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Marco Mochiwa alinifuata na kuniuliza mbona watoto wa mwalimu wetu Dk.Sengondo Adrian Mvungi yaani Dk.Natujwa na Nakundwa wamekuja kuchukuliwa ghafla na kurudishwa nyumbani.
Nilishtuka na kumwambia misijaona na nikamweleza Mochiwa kuwa taarifa hizo alizonipa ni mbaya sana kwangu na licha sina ushahidi nazo natoka darasani naenda ofisi ya walimu ilinikajue ni kwanini wamechukuliwa hivyo kwani saa saba mchana nilionana na Dk.Natujwa chuoni hapo na kuzungumza nae akasema kuwa baba yake hivi sasa anaitaji maombi kila wakati na tuliongea mambo mengi sana ambayo siwezi kuyaandika katika makala hii.Dk.Mvungi umeniuma sana.
Wakati nikishuka ngazi ghafla nikapokea simu toka kwa Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Mtanzania, Ester Mbusi akinipa pole ya msiba wa ‘mume wangu’ Dk.Mvungi.Niisii kuchanganyikiwa na kushuka ngazi pole pole huku nikienda kwenye ofisi za walimu nikakuta zimefungwa na kwenda kweny ofisi ya Meneja wa chuo,Innocent Mahedi na kumuuliza ni kweli Dk.Mvungi kafariki na nikweli
Dk.Natujwa kaondoshwa haraka chuoni hapo?
Mahedi alikatalia kata kata na kusema kuwa hana uhakika wa taarifa za kifo hicho , nilimuuliza zaidi ya mara saba huku nikilia na kumuliza iweje kama Dk.Mvungi ni mzima watoto wake wachukuliwe kwa dharula chuoni hapo?Iweje kama taarifa hizo ni za uongo, waandishi wa habari wengi wanipigie simu za kunipa pole zakuondokewa na ‘Rais Mdhurumiwa’?
Mahedi alijikausha ila niliwambia ukweli kuwa anafahamu ila ananificha.Kutokana na mazingira hayo nilimpigia simu Dk.Natujwa alipokea na kusema hana ushahidi na hilo ila wanaelekea Mwenge lakini nikasikia pembeni yake kwenye simu analia sana anasema baba yake amefariki.
Siyo siri nilijikuta nikilia kwa sauti ya juu kwenye viunga vya chuo na kukaa chini , namshukuru sana mwanafunzi mwenzangu wa sheria ambaye ni mwandishi wa habari wa gazeti la The Citzen,Bernad James ndiye aliyenisubiri nimalize kulia,na kuniinua kwenye mchanga nilipokuwa nimekaa na kunibebea mkoba na kunishika mkono kuelekea kituoni ambapo ni mwendo wa kama dakika 15 tukapanda wote Bajaji nanikamwambia kwakuwa nimeambiwa wakina Dk.Natujwa wamepelekwa Mwenge nyumbani kwa marehemu kaka yake Dk.Mvungi nilianza safari ya kwenda hadi hapo Mwenge vijijini saa 12 jioni na nilipokelewa na wako wapi Dk.Natujwa wakanithibitishia ni kweli Dk.Mvungi amefariki na watoto wake wamepelekwa Kibamba nyumbani kwa Dk.Mvungi alikokuwa akiishi na mke wake Anna na msiba utakuwa Kibamba.Nikapanda kwenye bajaji nalia sana hadi niliporudi nyumbani Sinza saa moja usiku ndipo kidogo nilianza kukubali hali halisi kuwa ni kweli ‘Rais Mdhulumiwa’ amefariki dunia, na kuanza kuandika makala hii.
Dk.Mvungi alijeruhiwa usiku wa kuamkia Novemba 3 mwaka huu kwa mapanga kichwani na usoni na kusababisha kupoteza fahamu tangu siku hiyo na Novemba 7 mwaka huu, alitolewa MOI na kusafirishwa kwenda Hospitali ya Milpark nchini Afrika Kusini kwaajili ya matibabu zaidi lakini Novemba 12 mwaka huu, alifariki dunia.Dk.Mvungi umeniuma sana.
Dk.Mvungi ‘Rais Mdhurumiwa’ ambaye aliwahi kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na hatimaye kufikia nafasi ya kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo UDSM,ni miongoni mwa waasisi Chuo Kikuu cha Bagamoyo(UB) ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katika na Rais Jakaya Kikwete, alikuwa ndiye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo.
Kabla sijafika mbali napenda kutamka wazi kuwa kifo na ukatili aliofanyiwa na wahuni ‘majini watu’, Dk.Mvungi yaliniumiza sana na yanaendelea kuniumiza sana hasa ukizingatia Dk.Mvungi licha kilikuwa ni chanzo changu cha habari ambaye alikuwa akinipa habari ambazo nyingine nilikuwa naziandika kwenye gazeti na nyingine nilikuwa siziandiki kwenye gazeaati alikuwa ni kama baba yangu wa kunizaa kwani aliniweka karibu mno na familia yake,alikuwa akinishauri mambo mengi likiwemo la kujiendeleza kielimu kwenda kusoma sheria, kifamilia, kazi yangu ya uandishi wa habari hasa ukizingatia Dk.Mvungi aliwahi kuwa mwandishi wa habari wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo licha hakuwai kusomea chuo chochote kozi ya Uandishi wa habari.
Sitamsahau Dk.Mvungi katika hili ambapo mwaka 2009 niliomba kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kusoma kozi ya Cheti cha Sheria nikakosa nafasi, nilivyokosa nafasi nilimfuata ofisini katika Shule ya Sheria UDSM, na kumueleza hilo ambapo Dk.Mvungi alinitaka nimfuate anakokwenda ili aende akawauleze ni kwanini mimi nimekosa nafasi ya masomo na fomu zangu zilikuwa na dosari gani, tuliingia katika ofisi ya mhadhiri mmoja anaitwa Semu Thomas ambaye alimsikiliza Dk.Mvungi na akamtaka Dk.Mvungi arudi ofisini akakae na kwamba yeye Semu atabeba jukumu hilo na alinipeleka hadi kwa Mkurugenzi wa Kozi ya Cheti cha Sheria Tairo, ambaye alisikiliza na kulitatua tatizo langu na akanitaka nijaze fomu upya, na kweli nilijaza fomu upya na zikagongwa mhuhuri wa uwakili na Dk.Mvungi na hatimaye nikakubaliwa kujiunga na kozi hiyo.Dk.Mvungi umeniuma sana.
Ndimara Tigambwage ndiye aliyemuingiza Dk.Mvungi katika fani ya uandishi wa habari kwani Dk.Mvungi alikuwa akinielezaga kuwa hapa duniani kuna watu anaweza kuwapinga adharani kupitia vyombo vya habari na siyo Ndimara Tigambwage au Balozi Costa Ricky Mahalu.
Kwani alipokuwa amemaliza elimu ya kidato nne alikuwa akiishi kwa marehe kaka yake Mwenge jijini Dar es Salaam, na wakati huo alikuwa akiandika mashahiri na kuyatuma kwenye gazeti la Mzalendo na kuuza duka.Ndimara ndiye aliyefika nyumbani kwa kaka yake Mvungi , Mwenge na kumshika mkono Dk.Mvungi na kumpeleka katika gazeti la Mzalendo na kuwaomba wahariri wampatie kazi ya uandishi wa habari ambapo alipatiwa kazi na alifanyakazi katika gazeti hilo akiwa na rafiki yake ambaye naye ni mjumbe wa Tume ya Mabadilko ya Katiba, Profesa Paramaganda Kabudi ambaye naye pia hakuwai kusomea uandishi wa habari lakini alikuwa ni mwandishi wa habari na mwisho wa siku Profesa Kabudi na Dk.Mvungi waliamua kwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kusoma sheria na mwisho wa siku walifaulu vizuri uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ukawapatia ajira ya kuwa waadhiri wa sheria wa chuo hicho hadi miaka ya karibu Dk.Mvungi alipostaafu utumishi wa serikali.
Dk.Mvungi pia alikuwa akinieleza kuwa hawezi kumpinga adharani Balozi Mahalu kwani balozi Mahalu akiwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ndiyo aliidhinisha Dk.Mvungi na wenzake waende kuongeza shahada nyingine ya sheria nchini Ujerumani.Nakusema anawaheshimu sana.
Kweli maneno yanaumba.Mara zote Dk.Mvungi alikuwa akimweleza mwanae mkubwa ambae ni Mkuu wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Bagamoyo(UB), Dk.Natujwa Mvungi siku akifariki ,mkewe mdogo yaani mimi Happiness Katabazi ambaye mara zote alikuwa akipenda kuniita ‘First Lady’ nitaandika makala ambayo itamuelezea yeye alikuwa ni mtu wa aina gani katika dunia hii na tulikuwa tukicheka Dk.Mvungi akisema hivyo na mimi nikawa ninamwambia ata akifariki ghafla tayari nina picha zake nyingi tulizopiga pamoja kwahiyo sitapata shida ya kutafuta picha zake hizo na kweli limetimia.
Tangu nianze kuwa karibu na Dk.Mvungi kama mzee wangu mwaka 2000- 2013 ,pamoja na mambo mengi alikuwa akinieleza kuwa enzi zaDk. Eliuther Kapinga, mwaka 2002.
Kapinga aliuawa kikatili kwa kunyongwa shingo na kupigwa nondo kichwani nyumbani kwake, Mbezi Beach.
Katika ujana wake Dk.Mvungi alikuwa akinieleza kuwa alikuwa akipenda sana kucheza mchezo wa ngumi na hadi hivi sasa Dk.Mvungi alikuwa akifanya sana mazoezi ya viungo na muongozaji mzuri tu shughuli katika sherehe na misiba. Na hata harusi ya Profesa Kabudi na mkewe ,ni Dk.Mvungi ndiye alikuwa MC wa harusi hiyo.
Si hivyo tu hata Chuo Kikuu cha Bagamoyo ambacho kinatarajia kufanya mahafali yake ya kwanza tangu kilipoanzishwa rasmi mwaka 2011, kilikuwa kimepanga Dk.Mvungi ndio awe MC wa mahafali hayo lakini kwa bahati mbaya akakutwa na mkasa huo uliosababisha afariki dunia.Dk.Mvungi ameniuma sana jamani.
Itakumbukwa kuwa katika kampeni za uchaguzi mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005.Dk.Mvungi alikuwa ni miongoni mwa wagombea urais.Itakumbukwa kuwa uchaguzi wa mwaka 2005 ulisogezwa mbele kwasababu aliyekuwa mgombea mwenza wa Chadema, alifariki dunia.Katika raundi ya kwanza ya kampeni, aliyekuwa mhariri wangu wa Gazeti la Mtanzania , Gabriel Athuman alinipanga niongozane na Augustine Mrema (TLP)katika kampeni zake ambapo nilizunguka na Mrema katika mikoa 15 kama mwandishi wa habari wa mgombea urais kwa tiketi ya TLP.
Tume ya ya Uchaguzi ikasimamisha kampeni kwaajili ya kifo hicho, ilipokuja awamu ya pili ya kampeni, Mhariri wangu Gabriel Athuman ambaye kwasasa anafanyakazi katika Ofisi ndogo za CCM, Lumumba Dar es Salaam,aliniondoa kwenye timu ya Mrema ambaye naye Mrema na mkewe Rose walikuwa wakiniita mimi ni First Lady wa Mrema, na kunipeleka kujiunga kwenye timu ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi ambaye ni Dk.Mvungi.
Kweli nilikuwa ni mwandishi wa habari wa kike peke yangu katika timu ya waandishi wa habari zaidi watano wanaume na tulifanyakazi yetu vizuri na Dk.Mvungi akawa anajigamba mbele ya Mrema kuwa amemwibia mke yaani mimi enzi hizo nikiitwa ‘First Lady wa Mrema’, na kwamba hivi sasa Happiness ndiye mke wa Dk.Mvungi kwasababu tu mhariri wangu amenipanga mwandishi wa kik kwenye msafara wake na jina hilo la First Lady liliasisiwa na Dk.Mvungi na mkewe Anna katika msafara wake ambao tulizunguka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar akiomba kura kwa wananchi ili awe rais wa Tanzania.
Lakini kura hazikutosha kwa upande wake , kura zilitosha kwa mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ambaye alitangazwa kuwa rais. Dk.Mvungi hakuwa na kinyongo na Rais Kikwete kushinda naninakumbuka baada ya Dk.Mvungi kumaliza kampeni aliathirika sana kiuchumi , sikumtupa nilikuwa naye katika shida na raha kwani nilipokuwa nafika ofisini kwake mimi ndiyo niligeuka kuwa mhudumu , karani mpokeaji wageni wake kwa kipindi hicho chote ninachokuwa ofisini wake.
Ilipofika katika kampeni za uchaguzi mkuu wa wa Urais mwaka 2010, Dk.Mvungi hakugombea na mimi nikiwa Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Tanzania Daima, aliyekuwa Mgombea Mwenza wa CCM, Dk.Mohammed Gharib Bilal aliiomba ofisi yangu iniruhusu niingie kwenye timu yake ya kuripoti mikutano yake ya kampeni ambapo tulizunguka nae mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar , na nilikuwa mwandishi wa kike peke yangu na wanaume watatu.
Kampeni hiyo ya Dk.Bilal ambaye kwa sasa ndiye Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilisababisha kwa miezi mitatu niwe mbali na Dk.Mvungi hali iliyosababisha Dk.Mvungi kuwa ananipigia simu ya kunitania huku akilalamika kuwa Dk.Bilal ametumia madaraka yake vibaya amempora ‘First Lady wake‘ ‘Happiness), yaani mimi na kwamba anakusudia kumfungulia kesi madai Dk.Bilal kwa kumpora mkewe.
Baada ya kampeni za 2010 kumalizika nikarejea mtaani na nikawa naona mara kwa mara na Dk.Mvungi na kumpatia ‘umbeya’ unaondelea mitaani nay eye ananipatia taarifa za hali ya kisiasa nchini na huko mikoani walikokuwa wanazunguka wamepata maoni gani ya wananchi.
Lakini ghafla nikamsikia mtu ambaye mimi na Dk.Mvungi tumekuwa tukimuita kwa utani kuwa ni mwizi wa kura za Dk.Mvungi mwaka 2005 na kwamba Dk.Mvungi ndiye alishinda kiti hicho cha urais ila kura zake ziliibwa, yaani Rais Jakaya Kikwete kamteua Dk.Mvungi kuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Sote vijana wake tulifurahia uteuzi huo na kumtakia kila la kheri katika majukumu hayo mapya na mara kwa mara nimekuwa nikienda kumtembelea katika ofisi hizo za Tume.
Mara baada ya kuteuliwa tukawa hatuonani mara kwa mara kama zamani kwani alikuwa akizunguka mikoni kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya.
Nilikuwa nikimtania kuwa namimi nakusudia kumshitakiwa Rais Kikwete kwasababu amesababisha ndoa yangu na yeye isambaratike kwasababu tangu apewe ofisi eneo la Posta Mpya karibu na Ikulu, sisi watu wa karibu naye tumekuwa hatumuoni mara kwa mara kwani amekuwa amaliza muda mwingi kwenye vikao vya tume na kusafiri mikoani kukusanya maoni.Tunacheka baada ya kutaniana hivyo kishatunaendelea na majadiliano yetu.Dk.Mvungi ameniuma.
Kwa wanaomfahamu Dk.Mvungi watakubaliana na mimi kuwa kama Taifa tumepoteza mtu aliyekuwa na mchango mkubwa sana hakika wasomi wa kozi ya sheria na kozi ya Uongozi na Utawala ambao walikuwa wakifundishwa na Dk.Mvungi,wale waliokuwa wakitetewa bure kesi zao mahakamani na Dk.Mvungi watakubaliana namimi kuwa wahuni wale wamemuua kikatiri na kinyama mpenzi wetu ambaye bado tulikuwa tukimuitaji.
Baada ya uchaguzi mkuu wa 2006, Dk.Mvungi alikuwa ananiambia ametikisika kiuchumi hivyo ‘First Lady wake nisirubuniwe na mafisadi nikamtelekeza.Na alikuwa akiniambia kuwa nimepata mume mwenye kichwa kikubwa ambacho kina akili na kinafikiri sawa sawa.
Alivyorudi kufundisha UDSM kufundisha na nilipokuwa naenda ofisini nakaa nae hadi wakati mwingine saa tano usiku na kisha dereva wake Emma anamrejesha Dk.Mvungi nyumbani kwake Chuo tunamuamsha mke wake Anna anamfungulia mlango na kisha anamwamuru dereva wake anirejeshe nyumbani, nilikuwa nikimshuhudia Dk.Mvungi pamoja na kazi nyingine alikuwa akiniambia anakiunda Chuo Kikuu cha Bagamoyo , kwani anautaalamu huo na kweli alikuwa akiandaa chuo hicho akishirikiana na Balozi Mahalu mimi nikiwa shahidi wa mchakato huo kwani wazo la kuanzishwa chuo hicho ni la Mahalu na Dk.Mvungi na kweli walifanikiwa hadi chuo kikaanza kufanyakazi.
Kwa ufupi Dk.Mvungi muda wake mwingi alikuwa akiumalizia kazini, kujisomea, kutoa ushauri wa kisheria kwa vyama vya siasa,wananchi waliokuwa wakiito huduma hiyo na wengine walikuwa hawana fedha za kumlipa alikuwa akiwatetea bure mahakamani,alikuwa ni mtu mwenye fikra za kimageuzi,hakupenda madaraka yeye alikuwa akinieleza kuwa anapenda kuwasaidia watu kupanga mikakati safi ili watu hao waweze kupata madaraka,aliweka mbele maslahi ya wanyonge na hakuwa mtu mwenye kuwa na tamaa ya fedha na siku zote alikuwa akisema yeye hatembei wala kushika fedha,fedha zake kidogo alizokuwa nazo zinashikwa na mkewe Anna.
Oktoba 29 mwaka huu,ndiyo ilikuwa ni siku yangu ya mwisho kukutana na kuzungumza kwa zaidi ya saa tatu na Dk.Mvungi ofisini kwake Tume ya Mabadiliko ya Katiba na tulipiga picha za kumbukumbu ya yeye kuwa katika ofisi hiyo mpya, nilipomtembelea ambapo nilifuatana na mdogo wangu Michael Machali alisema yeye yupo kwenye Tume hiyo kwaajili ya kukakikisha watanzania wanapata Katiba bora, na kwamba atatumia taaluma yake ya Sheria ya Katiba kuiwezesha Tume ya Jaji Joseph Warioba kufanikiwa na licha anaishi Kibamba ila anafika ofisini hapo saa 12 asubuhi na kuondoka jioni .
Kumbe ndiyo ilikuwa ni siku yangu ya mwanzo na mwisho ya kumuona na kumsikia hapa duniani Dk.Mvungi.Dk.Mvungi umeniuma sana.
Dk.Mvungi siku hiyo alitueleza na mdogo wangu kuwa siyo kwamba hapendi kuchukua muda mrefu kukaa na familia yake, bali dhamira yake imekuwa ikimtuma kutumia muda mwingi kwenda ofisini kuwatumikia watanzania na mara zote alikuwa akimsifu na kumheshimu Mwalimu Julias Nyerere kuwa Mungu alikuwa amewaletea watanzania kiongozi mwenye maono. Dk.Mvungi umeniuma.
Dk.Mvungi hakuwa mtu anayependa makuu licha alikuwa ni mtu aliyependa haki,kuwafundisha watu , ukweli na kusimamia kile anachokiamini bila woga na unafki.
Katika miaka ya karibu Dk.Mvungi alikuwa akilalamika taaluma ya habari imekumbwa na mmomonyoko wa maadili hapa nchini, kwani baadhi ya waandishi wa habari na wahariri wao wamekuwa wakiandika habari ambazo azisaidii sana maendeleo ya nchi isipokuwa kuandika habari zinazojadili tuhuma ambazo wakati mwingine ni za uzushi tu kuhusu ufisadi wa kiongozi fulani na kwamba hivi sasa baadhi ya waandishi wa habari za ufisadi wamezigeuza kama ndiyo dini yao na mara zote akawa ananiasa na kunifundisha jinsi ya kujiingiza kwenye uandishi wa aina hiyo.
Nafahamu kuna wanasiasa na mawakili leo hii watakuwa wanalia na kusaga meno kwasababu ya kifo hiki , kwasababu tulipokuwa wakiitaji kuandikiwa hotuba zao za kisiasa na kufundishwa jinsi ya kujenga hoja katika mijadala mbalimbali , kuwasilisha hoja mahakamani walikuwa wakimfuata Dk.Mvungi hata usiku wa manane na Dk.mvungi alikuwa akiwasaidia na hadi leo wanasiasa hao wamekuwa na majina makubwa sana hapa nchini ila sitawataja majina.Dk.Mvungi umeniuma.
Kwa wale waasisi wa mageuzi wa nchi hii ambao hivi sasa ni wazee, hawawezi kumtaja Dk.Mvungi enzi hizo akiwa ni kijana mdogo ambaye alikuwa akishiriki kikamilifu kupitia taaluma yake ya sheria katika kuakisha Tanzania inaiingia katika mfumo wa vyama vingi.
Mzee James Maparara, Mabere Marando, Dk.Ringo Tengo na wengine wanajua hilo kipindi kile wanaanzisha Taasisi ya TANLET, pia nimiongoni mwa waasisi waliokisuka Kituo cha Kutetetea Haki za Binadamu(LHCR) na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kupitia taaluma yake ya sheria.Dk.Mvungi umeniuma.
Nalipongeza jeshi la polisi kwa hatua yake ya kuwakamata watu waliodai kuwa ndiyo waliomsababishia kwa makusudi kifo ‘Rais Mdhurumiwa’.Naomba jeshi la polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi kufanya kazi yao ya upelelezi ,kukusanya ushahidi thabidi na kuandaa mashitaka kwa uweledi na kisha kuwafikisha mahakamani kwani endapo watakurupuka katika kuiandaa kesi hiyo ni wazi mwisho wa siku washitakiwa hao watakuja kuachiriwa huru na mahakama.
Dk.Mvungi ni mwanasheria wa kwanza kuuwawa kinyama
Hapa nchini ni Dk. Eliuther Kapinga, mwaka 2002.
Kapinga aliuawa kikatili kwa kupigwa nondo kichwani nyumbani kwake, Mbezi Beach. Lakini mwisho wa siku polisi na ofisi ya DPP walifanyakazi yao vizuri ambayo ilimshawishi Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ,Juxson Mlai kuwahukumu adhabu ya kifo.Nilipata fursa ya kuudhuria kesi hii mwanzo hadi mwisho wake.Ilikuwa ni majozi wakati washitakiwa hao wakijitetea kwani walikuwa wakieleza jinsi walivyoitoa roho ya Kapinga.
Mwanasheria mwengine ambaye pia alikuwa Mhadhiri wa sheria Mwandamizi wa UDSM ni Profesa Juani Mwaikusya ,Julai 14 mwaka 2010 naye alifariki kikatiri kwa kupigwa risasi akiingia nyumbani kwake eneo laSalasala, na hatimaye polisi ilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa na kesi hiyo ilifunguliwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Nimalizie kwa kusema kuwa Watanzania kama taifa hivi sasa miongoni mwetu wenye roho katiri na ambao mnafikiri mungu haoni ukatiri na madhira mnaowafanyia waja wake,mbadilike.
Acheni hiyo tabia kwani mnatuweka roho juu wenzenu na kuanza kuishi kwa wasiwasi .Kubalini kuwa mungu yupo, tena hajazeeka wala kupofuka macho na mungu wa siku hizi ni kijana anatembea na IPAD ameiunganisha na Wireles na anafanya mambo yake kisasa na analipa malipo hapa hapa dunia tena haraka sana, na nyie ipo siku atawaadhibu pamoja na vizazi vyenu.Laiti mngetambua umuhimu wa Dk.Mvungi hapa duniani aliokuwa nao msingethubutu kumtendea unyama ule.Mmemuuzia na kumuua Dk.Mvungi lakini nataka mtambue kuwa mtasababisha watu wengi waliokuwa wakimtegemea kutokana na mchango wa kazi yake waathirike zaidi na wengine waondoe kesi zao mahakamani kwasababu wamekosa wakili wakuwawakilisha mahakamani bure.
Nchi hii hivi sasa badala ya watu kuumiza vichwa kubuni mambo ya maendeleo kama kuanzisha viwanda vya kutengeneza magari, ndege,Laptop sisi ndiyo tumekuwa vinara wa kubuni mipango mkakati na endelevu ya kufanyiana vitendo vya kikatili vya kutupia majini kwa bei nafuu, kumwagiana tindikali, kutekana na kujeruhiana kwa mapanga, kuzulia uongo, fitna. Tabia hizi ni mbaya sana na zinatisha kwani wahalifu hawa siku hizi wala hawakusubiri njiani wanakufuata nyumbani wanakufanyia unyama.
Mmekatisha kikatiri maisha ya Dk.Mvungi ambaye alikuwa anategemewa na familia yake ikiwa ni pamoja na kuwalipia ada za shule watoto wake, kumtunza mkewe Anna na kuwapa mwongozo wanae.Dk.Mvungi ameniuma.
Dk. Mvungi ameacha mke na watoto watano. Alizaliwa Novemba mosi 1952. Mwaka 1994 alitunukiwa Shahada yake ya Udaktari katika fani ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Hamburg, Ujerumani.
Mwaka 1987 alipata Shahada ya Uzamili ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM); mwaka 1981 alipata Shahada ya Kwanza ya Sheria UDSM.
Dk. Mvungi hadi mauti yanamkuta alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu (LHRC).
Mmwaka 1995 hadi 2008 alikuwa Mtetezi na Mtafiti Mkuu wa Sheria na Haki za Binadamu katika Mradi wa Kituo cha Kutetea Haki za Wafugaji.
Aliwahi kuwa wakili kutoka LHRC katika kesi ya Kikatiba ya kutetea wananchi wa Kijiji cha Nyamuma.
Mwaka 2000 hadi 2003 alikuwa Mkaguzi wa Kitivo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda na mwaka 2003 alishika wadhifa wa kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria UDSM.
Daima Dk.Mvungi nitakukumbuka kwa mambo mengi likiwemo pia vazi lako la suti kwani nitofauti sana na aina ya suti zinazovaliwa na wanaume wengi, ni wanaume wachache sana wanaovaa aina ya mtindo wa suti alizokuwa anavaa Dk.Mvung na aina ya maisha uliyokuwa ukiishi.Vijana wako umetufundisha mengi mazuri tutayafuata na mabaya tuyaacha.
0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 14 mwaka huu.
0716 774494: www.katabazihappy.blogspot.com
No comments:
Post a Comment