Header Ads

TUNAPAMBANA KWELI NA DAWA ZA KULEVYA?

Na Happiness Katabazi

SERIKALI  pamoja na wananchi miongoni mwetu tumekuwa tukijinasibu kuwa tunapiga  vita matumizi ya dawa za kulevya ‘unga’  yenye mtandao mkubwa ndani na nje ya nchi.

Hoja ya kupiga vita biashara hii haramu inatokana na bidhaa yenyewe kusababisha madhara ya kiafya kwa watumiaji pamoja na kuichafulia sifa nzuri nchi ya Tanzania inayoonekana ni kitovu cha usafarishaji wa dawa hizo.

Serikali na taasisi mbalimbali za umma zimekuwa zikiibuka pale wanapokamatwa watuhumiwa wa dawa hizo wakiwa na uzito mkubwa au kuwahusisha watu wenye majina makubwa.

Wakati huo ndiyo huonekana mwanasiasa fulani akijinasibu kuwa kinara wa kupinga usafirishaji, uuzaji na utumiaji. Tambo zake huungwa mkono na vyombo vya habari kwa muda baada ya hapo mambo huendelea kwa utaratibu wa kimazoea.

Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kinachoongozwa na Kamanda, Godfrey Nzowa, kimejitahidi katika kupambana na dawa hizo lakini tatizo kubwa ni sheria, nia thabiti na utekelezaji wa wadau mbalimbali.

Licha ya serikali kupambana na biashara hiyo haramu, tujiulize ni kwanini serikali hii tangu Agosti  mosi mwaka jana, hadi leo imeshindwa kumteua Kamishna mpya wa Tume ya Kuzuia na Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini?

Aliyekuwa Kamishna wa tume hiyo, Christopher Shekiondo, amestaafu kazi, Agosti mosi mwaka jana, hadi leo hatujasikia ameteuliwa kamishna mpya.

Tume iliyokuwa ikiongozwa na Shekiondo ilianzishwa kisheria na taratibu za kiuendeshaji zilikuwa zikifuata mkondo huo huo.

Moja ya jukumu la tume hiyo ni kutoa thamani ya dawa za kulevya alizokamatwa nazo  mtuhumiwa katika kesi fulani zilizofunguliwa  Katika mahakama tofauti, ikiwemo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Kesi nyingine za dawa za kulevya zilizofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi  zimefunguliwa kwaajili ya kuandaliwa kisha zihamishiwe Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kwa ajili ya kusikilizwa kwa sababu Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za dawa za kulevya ambazo thamani yake imezidi sh milioni 10.

Hivyo kisheria ni lazima zifunguliwe Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kuandaliwa (committal proceedings) kisha zihamishiwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Nimekuwa nikiandika matukio na mienendo ya kesi mbalimbali zikiwemo kesi za dawa za kulevya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Nimefanya utafiti na nimekuwa nikihudhuria na kuandika kesi mbalimbali ikiwa pamoja na kuzungumza nje ya mahakama na washitakiwa wa kesi hizo, askari, mahakimu na wadau wengine wa mahakama, umeonyesha    mwaka 2012 , Jamhuri ilifungua kesi za dawa za kulevya mahakamani hapo 19.

Mwaka 2013 , Jamhuri ilifungua mahakamani hapo kesi za dawa za kulevya 13 na kuanzia Januari 2 mwaka huu hadi Februari  27 mwaka huu, upande wa jamhuri ulifungua kesi za dawa za kulevya  nane.

Na washitakiwa wa kesi hizo wapo gerezani kwa sababu ya kutokuwapo kwa dhamana kwenye makosa au tuhuma za aina hiyo,  kila zinapokwenda mahakamani hapo upande wa Jamhuri umekuwa ukidai upelelezi wa kesi hizo haujakamilika.

Kesi nyingine zinaongezewa milolongo isiyo na sababu kwakuwa wahusika hukamatwa viwanja vya ndege ama wamebeba au wamemeza dawa husika. Wanaomeza hulazimishwa kuzitoa kwa njia ya haja kubwa.

Watuhumiwa wa aina hii wanahitaji upelelezi wa aina gani? Wapo baadhi yao walishakutwa na vidhibiti eneo la tukio lakini kesi zao zina miaka miwili zikifanyiwa upelelezi.

Upelelezi wa aina hiyo ndio unaolisababishia taifa hasara kubwa ya kuwalisha mahabusu pamoja na kufurika kwa magereza yetu.

Kuchelewa kukamilisha upelelezi kunasababisha mashahidi waliokusudiwa kufariki dunia, ugonjwa, kuacha kazi, kusafiri au sababu zozote zile zinazokwamisha au kufifisha kesi.

Gharama za kuwasafirisha mashahidi wa aina hii ni kubwa sana, sioni sababu kwanini Kesi za dawa za kulevya aina chukua muda mrefu kumalizika wakati serikali inasema ipo Kwenye vita dawa za kulevya? 

Yapaswa tutafakari kwa kina juu ya vita hii na dhamira ya serikali, inakuwaje kesi za dawa za kulevya zichukue muda mrefu ilhali kesi za maandamano kama ile iliyokuwa ikiwakabili wafuasi 52 wa Sheikh Ponda Issa Ponda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilitolewa hukumu haraka?

Kesi hiyo ya maandamano ilifikishwa mahakamani Februari mwaka jana na ikatolewa hukumu Machi  20 mwaka jana, kesi hii ilimalizika ndani ya mwezi mmoja.

Hukumu zinapotolewa mapema watu hupata muda wa kuendelea na masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Kama serikali imedhamiria kutokomeza biashara haramu ya ‘unga’, kwanza imteue Kamishna mpya wa Tume ya Kuzuia Dawa za Kulevya.

Kamishna huyu ni muhimu, kwakuwa ndiye anayetoa thamani za dawa zinazokamatwa kama moja ya kielelezo mahakamani, naamini kuna Watanzania wengi  wana sifa za kushika wadhifa huo.

Kama serikali haipo tayari kutafuta kamishna mwingine, basi wamrudishe Shekiondo na wampe mkataba mwingine. Tangu Agosti mosi mwaka jana hadi leo tume hiyo haina kamishna.

Mungu Ibariki Tanzania.

Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Machi 23 Mwaka 2014

No comments:

Powered by Blogger.