Header Ads

DK.HOSEAH, KWA HILI HAPANA

Happiness Katabazi

MKURUGENZI wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah, hivi karibuni amekaririwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa mhimili wa mahakama nchini unachelewesha maamuzi ya kesi mbalimbali za rushwa zilizofunguliwa na taasisi yake.


Dk. Hoseah alisema TAKUKURU hukamilisha upelelezi katika kesi zake mbalimbali za rushwa, lakini mahakama zimekuwa zikishindwa kutoa uamuzi kwa wakati na kusababisha ushahidi uliokusanywa kuharibika na watuhumiwa kuachiwa huru, huku lawama zikienda kwa taasisi yake kuwa haifanyi kazi ipasavyo.

Aidha, msomi huyo aliendelea kujinasibu kwa kusema kuwa taasisi anayoiongoza inapofungua kesi, huwa na ushahidi wa kutosha na endapo mahakama zingeendesha kesi hizo bila urasimu, hukumu za kesi hizo za rushwa na ufisadi zingeweza kumalizika ndani ya wiki mbili.

Kimsingi tukubaliane kwamba kesi za rushwa ni kesi za jinai kama kesi nyingine, kwa hiyo, kuchelewa kutolewa hukumu kwa kesi hizo si kitu cha ajabu. Si tunaona kesi za mauji na rushwa ambazo kimsingi ni za jinai zinavyoendeshwa na kuchukua muda?

Binafsi sioni umaarufu wa kesi za rushwa ukilinganishwa na kesi za mauaji. Falsafa ya sheria inatuambia kuwa haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyonyimwa (justice delayed, justice denied). Sasa kama hiyo ni falsafa ya sheria tuangalie ni sababu zipi zinazozifanya kesi zichelewe kuamuliwa.

Kwa mfano, sheria imeweka vipengele vya kiufundi na visipotekelezwa haki haiwi imetimia kwa hiyo, huwezi kuwalaumu mahakimu au majaji ambao wamekuwa wakivifuata la sivyo wafanye kinyume chake, jambo ambalo si sahihi na litaunyima haki upande mmoja.

Sheria ambayo imeandaliwa vibaya inaweza kusababisha kesi kuchelewa pale isipotosheleza, mfano kama sheria inaweka kosa la jinai halafu waendesha mashitaka wakashindwa kuumba kesi kulingana na sheria iliyopo, basi mahakama ina mamlaka ya kumwachia huru mshitakiwa.

Si kwa sababu mshitakiwa huyo hajatenda kosa, bali ni kwa kuwa hati ya mashitaka imekosewa au imebuniwa kinyume na matakwa ya sheria, kesho yake au siku hiyo hiyo mshitakiwa anaweza kukamatwa na kufunguliwa kesi ile ile kama ilivyotokea Mei 27, mwaka huu, katika kesi ya Jinai Na. 27 ya mwaka huu, iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba, na Meneja Mradi, Deogratius Kweka, ambapo Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Waliarwande Lema, aliwaachia washitakiwa hao baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa na dosari za kisheria.

Sababu nyingine inayochelewesha kesi ni mahakimu, majaji, waendesha mashitaka, mawakili wa kujitegema, mashahidi wakiugua ni sababu tosha ya kesi kuahirishwa na hiyo sababu haipingiki kwa sababu binadamu hatuna uwezo nalo.

Lakini sababu nyingine ni upande wa mashitaka kushindwa kukamilisha upelelezi, hali inayosababisha kesi kupigwa kalenda. Tatizo hili tumekuwa tukiliona kila kukicha katika mahakama zetu katika kesi mbalimbali, waendesha mashitaka kutoka ofisi ya TAKUKURU, DPP wamekuwa wakiiambia mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika na wakati wakitoa sababu hiyo unakuta kesi husika iliyofunguliwa mahakama fulani ina zaidi ya miezi minane.

Lakini pia siku hizi umezuka mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya mawakili wa kujitegemea, wa kuwasilisha mapingamizi, kukata rufaa, kuomba mapitio katika mahakama za juu kwenye kesi zinazowakabili wateja wao wanapoona ushahidi wa upande wa mashitaka katika kesi husika umewabana wateja wao.

Hili linafanyika mchana kweupe. Kwa bahati nzuri sisi waandishi wa habari tunapokuwa tukizungumza na baadhi ya mawakili wa kujitegemea nje ya mahakama, hutueleza mbinu hiyo chafu ya kisheria ambayo wanajua fika mapingamizi na rufaa hizo hawatashinda.

Mbinu hiyo chafu si kuwa ni kosa au inavunja sheria, bali huwasaidia kupata muda mrefu zaidi wa kujipanga dhidi ya kesi wanazoziendesha pamoja na kuwapatia fursa wateja wao kuendelea kufanya shughuli zao wakiwa nje kwa dhamana.

Nafikiri Dk. Hoseah mbinu hii ambayo hivi sasa inaendelea kushamiri katika mahakama zetu hujaibaini. Mbinu hii hivi sasa ndiyo inayoonekana kushika hatamu na kupendwa na mawakili wengi zaidi. Ni jambo la kawaida kabisa kila kukicha kusikia au kuona kesi nyingi zikifunguliwa mahakamani lakini imekuwa ni nadra kusikia au kuona hukumu zikitolewa.

Kwa sababu kama hizo chache sioni sababu ya Dk. Hoseah kuilaumu mahakama kuwa inachelewa kutoa uamuzi katika kesi mbalimbali zinazopelekwa na taasisi yake. TAKUKURU ni miongoni mwa taasisi zinazolaumiwa na baadhi ya waendesha mashitaka na mawakili wa kujitegemea, kwamba kesi za rushwa zinazopelelezwa nayo zinashindwa kumalizika kwa wakati kwa sababu ya upelelezi kutokamilika kwa wakati pamoja na kutoletwa kwa mashahidi.

Hivyo, suala maamuzi ya kesi kuchelewa kutolewa si la kulaumiana, bali linapaswa liangaliwe mfumo mzima wa haki. Lakini tukianza kutupiana lawama mahakama inachelewesha kesi ina maana Dk. Hoseah anawashitaki mahakimu na majaji kuwa ama wanahongwa, wana maslahi binafsi au ni wavivu.

Hivyo, madai hayo ya Dk. Hosea hayapaswi kupewa nafasi mbele ya jamii ya kistaarabu, jamii ikifikia hatua hiyo ya kuamini maneno ya kushutumiana yatolewayo na viongozi wa taasisi nyeti hukosa imani kwa chombo husika jambo ambalo huleta dharau na kupunguza imani dhidi ya chombo hicho.

Lakini pia kauli kama hizo ni sawa na kushitakiana au upande fulani kutaka upate sifa ya kuwa unafanya kazi nzuri kuliko mwingine mbele ya Rais Jakaya Kikwete na jamii.

Ni vizuri ikakumbukwa kwamba Hoseah huyu alishawahi kuwa hakimu na kufanya kazi katika mahakama mbalimbali na anajua vilivyo matatizo mbalimbali wanayokumbana nayo, imekuwaje ameyasahau na kufikia hatua ya kutoa shutuma kama hizi?

Pia tumuulize Dk. Hoseah ni kwanini aliondoka kwenye kazi ya uhakimu? Na je wakati akiwa hakimu, aliwahi kumaliza kesi za rushwa au kesi nyingine ndani ya wiki mbili? Nauliza swali hilo kwa sababu kesi za rushwa hazikuanza jana wala juzi, bali ni za kipindi kirefu ingawa hazikuwa zikisikika kwenye vyombo vya habari kama zilivyo za hivi sasa.

La msingi kwetu Watanzania si viongozi kunyoosheana vidole, tujaribu kuona jinsi ya kuboresha mfumo wa kutoa haki kwa kubadilisha sheria ziwe rahisi zaidi kueleweka kwa watendaji na wananchi na ikiwezekana vipengele vyote vyenye kuleta na kuchangia ucheleweshwaji wa utoaji wa haki vinaondolewa.

Lakini pia tutoe mafunzo kwa mahakimu na waendesha mashitaka ili wawe na uwezo mkubwa zaidi wa kuziendesha kesi zote. Tuboreshe maslahi yao hao watendaji, bila shaka watakuwa na motisha ya kufanya kazi zaidi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

No comments:

Powered by Blogger.