DECI WAKWAMA TENA KISUTU
Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imekataa kurudia kutoa uamuzi wa dhamana wa kesi ya vigogo wa Taasisi ya Entrepreneurship for Community Initiative (DECI) kwa sababu tayari Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Addy Lyamula alishaitolea uamuzi.
Hayo yalisemwa jana na Hakimu Mkazi, Mteite, muda mfupi tu baada ya mawakili wa utetezi kuwasilisha ombi la kutaka mahakama hiyo iziondoe sababu zilizosababisha DPP-Eliezer Feleshi, Juni 17 mwaka huu, kutoa hati ya kuzuia dhamana ya washitakiwa, kwa madai sababu hizo hivi sasa hazipo tena.
Kitululu alidai sababu hizo hazipo tena kwani awali shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa kwa mara ya kwanza, na upande wa mashitaka ukawa umejengewa uwoga, hivyo DPP akafikia uamuzi wa kutoa hati hiyo ya kuzuia dhamana, ili kulinda usalama wa washitakiwa na maslahi ya Jamhuri.
“Siku hiyo kulikuwa na Maaskari wengi hapa Mahakamani hata wale wa kutuliza ghasia, ni ni dhahiri leo pia hawapo (jana), jambo ambalo limedhihirisha kuwa upande wa serikali umeridhika na hakuna wasiwasi wa kiusalama dhidi ya wateja wetu;
“Na kwa misingi hii tunaomba upande wa mashitaka uiondoe hati hiyo ya DPP ya kuzuia dhamana kwa washitakiwa ili wateja wetu waweze kupata dhamana kwani shitaka linalowakabili linadhamiwa” alisema Kitululu.
Akipangua hoja hizo wakili wa serikali, Biswalo Mganga, alianza kwa kusema yeye ana majibu mafupi kwamba upelelezi huo bado haujakamilika.
Mganga alidai kesi hiyo ilipokuja kwa mara ya pili Juni 17, mwaka huu, pamoja na mambo mengine yote, Hakimu Mkazi Lyamuya alitoa uamuzi kuhusu dhamana ya washitakiwa, uamuzi ambao alidai umemfunga mikono hata Hakimu Mteite na mahakama hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kutengua hati ya DPP.
Mganga akipangua hoja hizo huku akionyesha kujiamini, alidai hati hiyo ni ya DPP na bado DPP hajawasilisha taarifa ya kuiondoa.
Kuhusu hoja ya sababu za kiusalama baina ya washitakiwa na jamhuri , alidai sababu hizo zilitolewa na DPP na wala siyo Kitululu hivyo ni vema DPP mwenyewe akatoa taarifa ya kuiondoa hati hiyo.
Kuhusu hoja kwamba FFU na wanausalama kutokuwepo kwa wingi jana mahakamani hapo, alisema
“Hivi wale nyuma ni Mgambo?si maofisa wa polisi na wakili huyo asitake kuvifundisha kazi vyombo vya ulinzi na usalama kazi kwani vyenyewe vinajua ni jinsi gani vinavyofanyakazi” alidai Mganga na kusababisha watu kuangua kicheko.
Akitoa uamuzi wake, Hakimu Mkazi Mteite, alisema kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa tu na kwamba amesikiliza hoja za pande zote mbili na kueleza kuwa kuhusu hoja za upande wa utetezi kutaka wateja wake wapatiwe dhamana, hawezi kutolea maamuzi ombi hilo kwa mara ya pili kwani Hakimu Lyamuya alishalitolea uamuzi .
Lakini Mteite aliutaka upande wa mashitaka uangalie kama zile sababu zilizoainishwa kwenye hati ya DPP kama hivi sasa hazina nguvu tena, basi waziondee ili washitakiwa waweze kupatiwa dhamana na akaiahirisha kesi hiyo hadi Julai 10 mwaka huu.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Jackson Mtares Dominic Kisendi, Timotheo ole Loitgimnye, Samwel Mtares, Arbogast Kipilimba na Samwel Mtalis ambao wote wanaendelea kusota rumande.
Juni 12 mwaka huu, Wakili Kiongozi wa Serikali Justus Mlokozi alidai washitakiwa wote wanakabiliwa na mashitaka mawili, shitaka la kwanza ni kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu 111A(1)(3)cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu , na shitaka la pili ni kupokea amana za umma bila leseni kinyume na kifungu cha 6(1,2) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Kifedha Na.5 ya 2006.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Julai mosi, 2009
No comments:
Post a Comment