Header Ads

CHONDE CHONDE JAJI MKUU

Happiness Katabazi

DESEMBA 15, mwaka jana, Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani, alisema anakusudia kuzungumza na baadhi ya waliokuwa majaji wa Mahakama Kuu (wastaafu) ili wasaidie kupunguza wingi wa kesi zilizoko mahakamani hivi sasa.


Endapo hilo litakubalika, majaji hao wastaafu hawatalipwa mshahara bali watapata malipo kwa kadiri ya idadi ya kesi watakazoziamua. Jaji Mkuu alitoa kauli hiyo siku hiyo wakati wa hafla ya kuwapokea na kuwasajili mawakili wapya wa kujitegemea 20, hafla iliyofanyika katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

“Ninakusudia kuongea na baadhi ya ya majaji wa Mahakama Kuu waliostaafu tukubaliane malipo kwa kesi inayomalizwa. Kama inawezekana nitafikiri kuongea na rais ili ateue mahakimu wakazi waandamizi waliostaafu wawe makaimu jaji ambao hawatalipwa mishahara bali kwa kesi watakazoamua,” alisema Jaji Mkuu Ramadhan.

Alisema kutokana na wingi wa kesi Mahakama Kuu, kuanzia Desemba mosi mwaka jana, aliwateua Majaji wa Mahakama Kuu wote kuwa majaji katika Kitengo cha Ardhi kwa lengo la kuondoa ukiritimba kwa eneo hilo kusikiliza kesi zote.

Akizungumza hilo, Jaji Ramadhani alisema kwamba yanayosubiriwa kwa sasa ni marekebisho ya Sheria ya Ardhi katika sura ile ya 216 kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002 ili utekelezaji huo uanze.

Jaji Mkuu huyo ambaye ni Brigedia Jenerali Mstaafu wa JWTZ pamoja na kuwataka mawakili hao kufuata miiko ya kazi yao kwa kuwajali wananchi maskini na mikoani, alizungumzia suala la mlundikano wa kesi na kuahidi kupitia kanuni mpya ya Mahakama ya Rufaa (Court of Appeal Rules, 2009) itakayotumika mwaka huu ili kupunguza tatizo hilo.

Kwanza kabisa napenda nipongeze uamuzi wa Jaji Mkuu wa kuwateua majaji wote wa Mahakama Kuu kuwa Majaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kwani hakuna ubishi kwamba wananchi wengi waliofungua au waliofunguliwa mashauri katika kitengo hicho wamekuwa wakilalamika ucheleweshwaji wa kutolewa maamuzi kwa mashauri na sababu moja wapo ni uhaba wa majaji wa kuzisikiliza kesi hizo.

Ndiyo maana nikaanza kwa kupongeza hatua hiyo kwani inatasaidia kwa kiasi fulani mrundikano wa kesi.

Lakini pia naomba nitofautiane na kusudio la Jaji Ramadhani la kuzungumza na baadhi ya waliokuwa majaji wa Mahakama Kuu (wastaafu) ili wasaidie kupunguza wingi wa kesi zilizoko mahakamani hivi sasa.

Tujiulize ni majaji na mahakimu wakazi wa aina gani anaotaka kuwarejesha? Na atatumia chujio lipi kuwachuja majaji na mahakimu wasafi na wazalendo kuwarejesha? Kwani si miongoni mwao mahakimu na majaji ndiyo walishindwa kuzimaliza baadhi ya hizo kesi ambazo leo tunazilalamikia kuwa kuna mlundikanao wa kesi mahakamani?

Kuna baadhi ya mahakimu walivyostaafu, baadhi ya wananchi na watumishi wa mahakama walishukuru na kufanya sherehe na kugonganisha bilauri kwani mahakimu hao walikuwa hawazingatii maadili ya taaluma. Ila kwa sababu tu mhimili wetu wa Mahakama hapa nchini haupendi kuwafukuza kazi watumishi wake licha ya kuwa baadhi yao ni wachafu.

Sisi Watanzania tuna haki ya kuletewa watendaji wenye damu inayochemka, wachapakazi na wanaoweza kukabiliana na mikikimikiki. Kuna vijana wengi wamesoma diploma na shahada za sheria wanaweza kuwa mahakimu wazuri tu.

Kwa nini Jaji Mkuu anatafuta njia ya mkato ya kuwatumia wastaafu badala ya mpango endelevu ambao akiutumia ipasavyo mlundikano wa kesi mahakamani utakuwa ni historia?

Kwa nini asione haja ya kuiomba serikali iongeze fedha kwenye mhimili anaouongoza ili kwa kipindi cha masomo cha mwaka ujao, mahakama iweze kupeleka wanafunzi wengi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), mkoani Tanga, ili waweze kuhudhuria kozi ya uhakimu na wakitoka hapo wapewe ajira ya uhakimu kwenye mahakama zetu?

Jaji Mkuu na watendaji wake hawana njia, bali kuikaba koo serikali iweze kuwaongezea fungu ili mwaka ujao wa fedha , mahakama iweze kuongeza idadi kubwa zaidi ya mahakimu wakazi wengi ukilinganisha na miaka iliyopita.

Binafsi naona itakuwa ni vyema kama uongozi wa mahakama ungetumia mkakati wa muda mrefu ambao utakuwa ni endelevu kwa kufuata njia hizo mbili ambazo naamini mwisho wa siku msongamano wa kesi mahakamani utapungua kwa kiasi kikubwa.

Kwani ni uongozi huu wa mahakama kila kukicha umekuwa ukilia kwamba vyumba vya kuendeshea kesi ni vichache na wakati mwingine unakuta mahakimu wakazi wawili wanatumia ofisi moja na hali siyo tu ipo mikoani, hata pale Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu tunaishuhudia kila kukicha.

Sasa tumuulize Jaji Mkuu, hao wastaafu anaokusudia kuwakodisha ili waje kumaliza mlundikano wa kesi, watakuwa wanakaa kwenye vyumba vipi? Au wataandaliwa vyumba maalumu vya kuendeshea kesi hizo?

Ni kweli baadhi ya majaji na mahakimu wastaafu wamekuwa wakiujua muundo wa mhimili wa mahakama vizuri na ni wazalendo, lakini hatuoni kwamba wakati umefika sasa wa kuwaacha wazee wetu hao wapumzike na badala yake wabaki kuwa washauri wa mahakimu na majaji wa sasa ?

Nchi ni yetu sote mambo yatakapoharibika ni wote tunaharibikiwa, hivyo ni vyema tukawa na mipango ya muda mrefu ili mwisho wa siku iwe endelevu na suluhisho la matatizo fulani fulani. Naelewa wazi Jaji amefikia uamuzi huo kwa moyo wa uzalendo kwa taifa lake lakini nimalizie kwa kumweleza kwamba Watanzania tunahitaji mipango endelevu na itakayomaliza matatizo hayo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Januari 3 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.