Header Ads

MIAKA MITANO YA SERIKALI YA AWAMU YA NNE:


*TUMFUNDE NINI RAIS JAKAYA KIKWETE?

Na Happiness Katabazi

UONGOZI wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, umebakisha takriban miezi tisa kabla haujamaliza kipindi chake cha miaka mitano ambacho kimeainishwa katika Katiba ya nchi.


Moja kati ya mambo aliyokuwa ameahidi Kikwete pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye kampeni za kuwania kiti cha urais ni kuwaletea Watanzania maisha bora pasi na kuainisha njia za kutekelezea ahadi hiyo ambayo sasa inaonekana ni kitendawili kikubwa kilichokosa mteguaji.

Ni ukweli usiopingika kuwa ahadi hiyo na kauli mbiu ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya vilivyochangia kumpa ushindi wa kishindo alioupata mwaka 2005 na kuwabwaga washindani wake kutoka vyama vya upinzani.

Ushindi huo haukupatikana kwa uraisi kutokana na kukabiliwa na upinzani mkali ndani na nje ya CCM, kundi la wanamtandao lililokuwa likiratibiwa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, ambao wanasemekana kuwa ‘maswahiba’ wa Rais Kikwete ambao ndio waliokuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha mtandao wao unamuingiza mgombea wao Ikulu iwe kwa mbinu chafu au safi.

Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye kwa wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa CCM, alilazimika kumpigia kampeni Rais Kikwete hata kama alikuwa hajui ni mbinu gani zingetumika kutimiza ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania; ahadi hizi za kwenye kampeni hizo ziligubikwa na mizengwe ya kila aina.

Baada ya Kikwete kuingia madarakani wanamtandao waliofanikisha safari yake ya kuingia Ikulu walijikuta kila mmoja wao akizawadiwa kulingana na nafasi yake kwenye mtandao. Waliochangia fedha nyingi nafasi zao zilikuwa kubwa (uwaziri), waliouunganisha mtandao na kuufanya ufanikiwe wakaambulia vyeo serikalini, kuanzia ukatibu mkuu hadi ukuu wa wilaya.

Waliokuwa kwenye jamii wakatupiwa mfupa wa kutafuna ulioitwa ‘mabilioni ya JK’.

Hayo ndiyo yaliyokuwa matokeo ya maisha bora kwa kila Mtanzania. Aliyepata alipata na aliyekosa alikosa. Sandakalawe…amina!

Leo CCM imeparaganyika siyo tena chama kile kilichomteua Kikwete akitetee kipate ushindi wa Tsunami, kuna makundi yanayowania nafasi ya urais wa nchi kwa udi na uvumba tena kwa kauli za kushtua na za kuulaumu utawala wa sasa kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo pamoja na kuwalea baadhi ya wanachama wenzao wanaodaiwa kuwa ni mafisadi.

Si jambo la ajabu kwa makundi hayo kuibuka kwa kasi kipindi hiki na kudai nchi imekosa uongozi imara kwa kuwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Kikwete katika kipindi hiki cha miaka mitano kashindwa kuvunja makundi na kukiunganisha chama kwani bado kuna CCM mtandao ile ya wasio wanamtandao.

Jambo jingine ni kushindwa kukiondoa chama na watu walio karibu naye katika kashfa mbalimbali za ubadhirifu wa fedha (ufisadi) unaoonekana kuwa wa kitaasisi zaidi kuliko ilivyofikiriwa mwanzoni kuwa ni utashi wa baadhi ya watu wenye tamaa za kuchuma mali kwa njia zisizo halali.

Chama hivi sasa kinaonekana kukumbatiwa na baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni matajiri ambao kila wanachokisema ndicho kinachofuatwa hali ambayo imekifanya kipoteze sifa ile kilichojizolea siku nyingi kuwa ni chama cha wakulima na wafanyakazi ambao walihenya kukiimarisha chini ya utawala wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Lakini kubwa zaidi ambalo watu wamekuwa wakililalamikia ni kuwa serikali yao imegeuka kuwa ya kidhalimu; isiyojali wananchi wake hasa kwa kutekeleza sera ya ubinafsishaji, kubomoa bomoa nyumba, unyang’anyaji wa mali za watu bila fidia inayostahili.

Cha kusikitisha zaidi hata zile ahadi tamu tamu walizokuwa wakipewa huku wakigaiwa fulana, kofia na khanga za kuisifu CCM, karibu zote zote hazijatekelezwa ipasavyo ikiwemo elimu bure kwa vijana hadi chuo kikuu, nyumba za serikali zilizouzwa kurejeshwa mikononi mwa serikali pamoja na maboresho makubwa ya sekta ya afya.

Leo hii wale waliokuwa mstari wa mbele kusema kuwa ahadi hizo zingetekelezwa wamekuwa wakitembea vichwa chini kwa aibu kila wanapopita na kushuhudia umaskini unavyozidi kushamiri kadiri siku zinavyosonga mbele, elimu inavyozidi kushuka, nchi inavyozidi kutegemea misaada kutoka nje na mambo mengi ambayo kimsingi yanaondoa dhana nzima ya taifa kuwa huru.

Utawala wa sasa unaweza kujivunia mafanikio ya kujenga na kuanzisha mahusiano mazuri na nchi nyingi duniani, baadhi ya sekta angalau naweza kusema zimeweza kupiga hatua za kimaendeleo, uhuru wa kutoa maoni kwa wananchi ambao umeainishwa kwenye Ibara ya 18(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, umepanuka kwa kiasi kikubwa chini ya uongozi wa Rais Kikwete kulinganisha na awamu zilizopita.

Rais Kikwete, bado amezingirwa na kundi kubwa la wapambe wanaodai wanampenda na wanamshauri vizuri. Hawa baadhi yao leo nalazimika kuwaita ni ‘mbwa mwitu’ waliovaa ngozi ya kondoo, kwa sababu wakati mwingine Rais anashindwa kuona uborongaji wa mambo unaofanywa na watendaji walio chini yake lakini wapambe hawa wanashindwa kumueleza ukweli badala yake wanabaki wakimsifia kwa kuteua watendaji wachapa kazi na makini ilhali wajua wanampaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

Aina hii ya wapambe haijaanza kwa Rais Kikwete pekee kwani ilianza katika Awamu ya Mwalimu Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.

Viongozi ama kwa kujua au kutokujua wamejikuta wakikubaliana na maelezo wanayopewa kila mara na wapambe hao ambapo wamekuwa wakijitahidi kujenga ukuta mkubwa kati ya viongozi na wananchi kwa hofu kuwa fursa hiyo ikipatikana wananchi wataeleza kila kitu kuhusu matatizo yao pamoja na utendaji usioridhisha.

Nina hakika wapambe hawa hawataishia hapa hata kura zako (Kikwete) zitakapotosha katika kipindi chako cha pili cha kuliongoza taifa kwa miaka mitano mingine (2010-2015), ndipo utaanza kuona rangi halisi za wapambe na wale uliowapa madarakani kwa kuwa wanajua huwezi tena kuwania kiti hicho kulingana na matakwa ya Katiba.

Wengi wao watajitenga nawe, licha ya baadhi yao hivi sasa kutokubaliana nawe; bali wanafanya hivyo kwa woga na unafiki hasa kutokana na nguvu uliyonayo katika kiti cha ukuu wa nchi, hawa watakusaliti na watakupaka matope na kila aina ya uchafu kiasi cha kufanya uchukiwe na jamii kama anavyoonekana Rais mstaafu, Benjami Mkapa.

Najua wakati huo hutakuwa na nguvu ya kuwadhibiti kama ilivyo hivi sasa. Leo wanakuchekea na kukupamba kwa kuwa uko madarakani, lakini kesho watakukimbia na kukucheka huku wakikuzomea kwa yale waliyokushauri vibaya na ukayafuata.

Ni vyema Kikwete ungesikia wosia huu ukabadilika kwa kuamua kuwa rais wa Watanzania wote . Kumbuka Watanzania walikuchagua uwaongoze siyo ugeuze urais kuwa ni kikundi cha watu wachache.

Ni vyema pia rais wetu na serikali unayoingoza mngesikia wosia huu na kuamua kuwa watenda haki mkasimamia haki za wanyonge wa nchi hii badala ya hao mafisadi na matajiri wanaodaiwa kuwa na ushawishi mkubwa kwako. Hivi kweli utakapoondoka Ikulu hizo kampuni za madini ambazo serikali inaonekana kuzitetea na kuzilinda kwa gharama kubwa zitayaenzi yale yote uliyozifanyia?

Ni vyema Kikwete ukayatafakari yanayoendelea kumpata mtangulizi wako Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye wakati anakaribia kustaafu na alivyostaafu alijikuta anakabiliwa na wimbi kubwa la kashfa dhidi ya serikali yake na familia yake ambazo ziliibuliwa na kuenezwa na kukuzwa na vyombo vya habari na wale waliokuwa baadhi ya wapambe wake wa karibu ambao aliwaamini na kuwapenda.

Wapambe hao wengine walikuwa ni wataalamu wa fani mbalimbali; walimshauri baadhi ya sera ikiwemo ile ya uuzwaji wa nyumba za serikali, ubinafsishaji; Rais Mkapa bila kujua alikuwa akitegwa na mbwa mwitu hao aliidhinisha sera hizo zitumike lakini mwisho wa siku walimgeuka na kuanza kumcheka na kumpakazia kwamba ameuza nchi na nyumba za serikali.

Na hata wewe Rais Kikwete ambaye wakati Mkapa akiwa madarakani, ulikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, sera hizo wakati zinapitishwa ulikuwa ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri, ulizikubali. Na bado ningali nikikumbuka mwaka 2005 ulivyokuwa ukiomba kura uliwaahadi wananchi kuwa wakikuchagua utazirejesha nyumba hizo serikalini lakini hadi sasa bado ahadi hiyo inaonekana mwiba kwako na kwa watendaji wako.

Na kwa tafsiri ya ahadi hiyo, wewe ulikuwa ukiikosoa kinyumenyume sera hiyo ya uuzwaji wa nyumba za serikali kwa watumishi wake iliyoasisiwa na serikali ya Mkapa hali iliyopelekea wananchi wakuone wewe ni shujaa na Mkapa akaonekana ni kiongozi asiye mzalendo kwa taifa lake na fisadi wa kupindukia.

Baadhi ya wananchi wasiotaka kutafuta ukweli na kuchambua mambo kwa kina wanaendelea kumchukia Mkapa, utafikiri hakuwahi kufanya jema hata moja katika utawala wake.

Jambo hilo ni hatari kwa usalama wa taifa letu siku za usoni kwani mtindo huu wa wanasiasa uchwara wasiotaka kutumia nguvu ya hoja kupinga maamuzi yaliyochukuliwa na wanasiasa wenzao matokeo yake wanaamua kutumia uzushi na majungu kwa kushirikiana na baadhi ya waandishi ‘wachumia tumbo’ na kuanza kuchapisha baadhi ya habari za uongo dhidi ya viongozi tena wakubwa wa nchi hii, tukae tukijua ipo siku hao wanaochafuliwa kwa uzushi uvumilivu utawashinda kwani nao ni binadamu hawajatolewa nyongo, nao watajitokeza hadharani kuanika wanachokijua, ni wazi nchi haitakalika.Tusifike huko.

Mwisho ni vyema Rais Kikwete ujue kwamba Tanzania haina uongozi wa kichifu au usultani inapotokea watoto wa rais kwa kipindi kifupi tu wanatumia jina la rais kupewa madaraka kwenye chama kinachoongozwa na baba yao, tabia kama hiyo ni chanzo cha udhaifu mkubwa kwa rais mwenyewe na ishara ya kutokuwa makini.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Januari 17 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.