Header Ads

JEETU PATEL ARUHUSIWA KUTOKA NJE YA DSM

Na Happiness Katabazi

IKIWA ni siku sita tangu Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, itengue uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kusimamisha usikilizaji wa kesi ya wizi wa Sh bilioni 7.9 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu (BoT), inayomkabili Mfanyabiashara maarufu Jayantkumar Chandubhai Patel maarufu ‘Jeetu Patel na wenzake wawili, upande wa utetezi umedai unapinga uamuzi huo.


Sambamba na hilo mahakama hiyo imewaruhusu washitakiwa hao kwenda nje ya Dar es Salaam na kukuwataka waakikishe siku ya kesi yao wanafika mahakamani bila kukosa ila mahakama hiyo ikakataa ombi la washitakiwa la kutaka ruhusa ya jumla ya kutoka nje ya mkoa na badala yake imewataka washitakiwa pindi wanapotaka kusafiri wafike mahakamani na kuomba ruhusa kwa mujibu wa sheria.

Mbele ya jopo la mahakimu wakazi Rwaichi Meela, John Kayoza na Grace Mwakipesile,wakili wa utetezi Mabere Marando, Martin Matunda waliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili kutajwa na kutolewa uamuzi lakini upande wa utetezi unawasilisha ombi la kutaka mahakama hiyo itoe amri ya kusitisha usikilizwaji wa kesi hiyo.

Marando alisema wamefikia kuiomba mahakama itoe amri hiyo kwasababu juzi waliwasilisha notisi ya kupinga maelekezo yaliyotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ,Semistocles Kaijage kwa Mahakama ya Kisutu Ijumaa iliyopita, katika Mahakama ya Rufani nchini ili mahakama hiyo iweze kuyapitia maelekezo ya jaji huyo na kuyatolea uamuzi.


Marando alieleza kuwa tayari notisi hiyo imeishapokelewa katika Mahakama ya Rufani na imeishapewa na Na.3 ya mwaka huu,ambapo warufani ni washitakiwa Ketan Chohan ,Devendra Vinodbhai Patel, Amit Nady

“Sisi tunapinga hayo maelekezo ya mahakama kuu kwa mahakama hii na ndiyo maana tumewasilisha ombi katika Mahakama ya Rufani ya kutaka mahakama juu kabisa ifanye mapitio ya maelekezo hayo …hivyo ndiyo maana tunaiomba mahakama hii ya Kisutu itoe amri ya kusitisha usikilizwaji wa kesi hii hadi mahakama ya rufani itakapotolea uamuzi ombi letu”alidai Marando.

Alisema kwenye kesi za masuala ya Kikatiba yanayofikishwa Mahakama Kuu,yanasikilizwa na kutolewa maamuzi na jopo la majaji wa tatu lakini chakushangaza jaji Kaijage ametoa maelekezo hayo peke yake.

Aidha kwa upande wa wakili kiongozi wa serikali Stanslaus Boniface,Fredrick Manyanda walidai kuwa hawana pingamizi na ombi hilo na Hakimu Mkazi Rwaichi Meela aliairisha kesi hiyo Februali 12 mwaka huu, ndipo watakapokuja kutoa uamuzi kuhusu ombi hilo la upande wa utetezi.

Hii ni mara ya pili kwa upande wa utetezi kuwasilisha ombi la kutaka kesi usikilizwaji wa kesi hiyo usitishwe, mara ya kwanza ilikuwa Oktoba 26 mwaka jana , mahakama hiyo ilikubali ombi hilo la kusitisha usikilizwaji wa kesi hiyo kwasababu washitakiwa hao walikuwa wamefungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu.

Hata hivyo Ijumaa iliyopita Mahakama Kuu ilitengua uamuzi huo wa Mahakama ya Kisutu uliokuwa umekubali kesi hiyo isitishwe kwasababu ilibaini maombi waliyowayoyatoa mahakama ya kisutu na kuyaleta Mahakama Kuu na maombi yao katika kesi ya Kikatiba iliyopo mahakama kuu yanafanana.

Novemba 4 mwaka 2008 , ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kati ya Agosti na Desemba 2005 ndani ya jijini la Dar es Salaam, washitakiwa hao waligushi nyaraka mbalimbali na zilizoonyesha kampuni yao ya Bencon International Limited imepewa idhini ya kurithi deni la kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan na kufanikiwa kuiba sh 7,962,978,372.48 mali ya Benki Kuu ya Tanzania.

Juni 4 mwaka jana, Jeetu na wenzake walifungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inayosikilizwa na jopo la majaji watu wanaongozwa na Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu, Geofrey Shahidi na Semistocles Kaijage. inaendelea kusikilizwa ambapo upande wa walalamikaji na wadaiwa wameishawasilisha utetezi wao na imepangwa kuanza kusikilizwa Novemba 2 mwaka huu.

Katika kesi hiyo ya Kikatiba , Jeetu na wenzake wanamshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Reginald Mengi na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwamba kwa nafasi zao walishindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu baada ya mdaiwa wa pili (Mengi) kuwahukumu kupitia vyombo vya habari kabla ya kesi zao nne zilizofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu kutolewa hukumu.

Jeetu na wenzake walifungua kesi hiyo ya kikatiba Na. 30 wakiomba Mahaka ma Kuu itoe tafsiri sahihi ya ibara 13, kifungu 4, 5 na 6 (b) cha Katiba ambacho kinatamka watu wote ni sawa mbele ya sheria na pia itafsiri ibara 13 (6) (b) inayosema mtu yeyote asichukuliwe ana hatia hadi pale mahakama itakapomkuta na hatia.

Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji hao wanadai kuwa wamefikia uamuzi huo wa kuiomba mahakama itoe tafsiri ya ibara hizo za katiba kwa kuwa wanaamini zimevunjwa na Mengi ambaye Aprili 23, mwaka huu, alitumia vyombo vya habari kuwahukumu kwa kuwaita ‘Mafisadi Papa’ wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayosikiliza kesi zao haijatoa hukumu.

Uamuzi wa kusimamaishwa kwa kesi hii iliyofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu , ulikuwa ni uamuzi wa tatu kutolewa katika kipindi cha Oktoba mwaka jana, mahakama hiyo ilitoa amri ya kusimamishwa kuendelea kwa kesi ya wizi wa sh bilioni 9, kesi ya wizi wa sh 3.9 zinazowakabili washitakiwa hao hadi kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na washitakiwa hao itakapotolewa uamuzi.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi nne za wizi wa fedha katika Akaunti ya EPA katika Mahakama ya Kisutu ambazo zilifunguliwa Novemba mwaka juzi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania daima la Alhamisi, Januari 21 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.