Header Ads

MTIKILA ATUPWA RUMANDE

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemtupa rumande Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila baada ya kumfutia dhamana kwa kukiuka masharti.


Amri ya kumfutia dhamana na kutupwa rumande ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, baada ya kusikiliza utetezi wa Mtikila aliyechelewa kuhudhuria kesi ya uchochezi inayomkabili mahakamani hapo.

Mtikila alipofika mahakamani hapo majira ya mchana alikamatwa na askari polisi waliokuwa na hati ya kukamatwa kwake baada ya kutoonekana mahakamani hapo jana asubuhi wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Hati ya kukamatwa kwa Mtikila ilitolewa baada ya ombi la Wakili wa Serikali, Beatrice Mpangala aliyekuwa tayari kusikiliza kesi hiyo, lakini mshitakiwa huyo kutoonekana mahakamani bila kuwapo kwa sababu za msingi.

“Sababu ulizotoa za kushindwa kufika mahakamani leo asubuhi zimeshindwa kuishawishi mahakama na hii ni mara ya pili kwa wewe kushindwa kufika mahakamani wala wadhamini wako.

“Mara ya kwanza ilikuwa Oktoba 22 mwaka jana, ulichelewa pia kuja mahakamani. Ili tabia hii ikome mahakama inakufutia dhamana yako kwa sababu umeshindwa kujiheshimu,” alisema Hakimu Lema.

Alisema Mtikila atakaa rumande hadi Januari 25, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya upande wa mashitaka kumsomea maelezo ya awali.

Kabla ya kutoa amri hiyo, hakimu huyo alimhoji Mtikila alikuwa wapi wakati kesi yake inatajwa mahakamani, naye kujibu kwamba alikwenda kwa daktari wake aliyemfanyia upasuaji alipogongwa na nyoka nchini Zimbabwe.

Mtikila aliendelea kujitetea kuwa asubuhi alijitahidi kuwatafuta wadhamini wake ili wamuwakilishe mahakamani lakini hakuwapata.

“Mheshimiwa Hakimu asubuhi nilijitahidi kuwasiliana na wadhamini wangu, lakini sijafanikiwa, ndiyo maana mimi nimekuja mchana,” alidai Mtikila.

Hata hivyo, hakimu Lema alisema kuwa sababu hizo si za msingi, hivyo ameshindwa kuishawishi mahakama isimfutie dhamana.

Katika kesi hiyo ya uchochezi Mtikila anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi ya kumkashfu Rais Jakaya Kikwete kwa kumuita gaidi kwa sababu serikali anayoingoza inataka kuanzisha Mahakama ya Kadhi, jambo ambalo linapingana na katiba ya nchi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Januari 12 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.