Header Ads

KORTI YAWANG'ANG'ANIA MAOFISA WA BoT

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la upande wa utetezi katika kesi ya wizi wa sh milioni 207 katika Benki Kuu(BoT) lilokuwa likitaka washitakiwa watatu katika kesi hiyo ambao ni maofisa wa benki hiyo wafutiwe mashitaka kwa sababu wanakinga ya kutoshitakiwa wakati wakitetekeleza majukumu yao ya kikazi.


Washitakiwa katika kesi hiyo ni Kada wa CCM,Rajab Maranda, Farijara Hussein na maofisa watatu wa BoT, ambao ni Ester Komu, Iman Mwakosya na Bosco Kimela wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Mabere Marando,Majura Magafu na Mpare Mpoki.

Uamuzi huo ulitolewa jana na kiongozi wa jopo la Mahakimu Wakazi Ignas Kitusi anayesaidiana na Eva Nkya na John Utamwa kufuatia juzi wakili wa utetezi Mpare Mpoki kuwasilisha ombi hilo ambapo alisema kwa mujibu wa kifungu cha 65 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 inakata mfanyakazi au mjumbe wa bodi wa benki hiyo asishitakiwe kwa makosa aliyoyatenda wakati akitimiza majukumu ya kikazi na hivyo DPP kabla ya kuwashitaki alipaswa awaondolee kinga , hoja ambayo ilipingwa vikali na Wakili Kiongozi wa Serikali Stanslaus Boniface.

Akisoma uamuzi huo Kitusi alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, jopo hilo limebaini tatizo lipo kwenye tafsiri ya kifungu hicho cha sheria ambapo alisema ni kweli kifungu hicho kinatoa kinga kwa wafanyakazi na wajumbe wa bodi ila kwasababu washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya wizi,kula njama,kughushi makosa ambayo si moja ya majukumu yakazi ya washitakiwa hao.

“Baada ya kusema hayo tunakubalina na wakili Mkuu wa Serikali Boniface kwamba ni kweli wafanyakazi na wajumbe wa bodi ya BoT wanakinga lakini makosa yanayowakabili siyo moja ya majukumu yao yakazi…hivyo tunatupilia mbali pingamizi ombi la utetezi na washitakiwa ambao ni maofisa wa BoT wataendelea kubaki kwenye kesi hii kama ilivyokuwa awali”alisema Ignas Kitusi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis, Januari 21 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.