Header Ads

JWTZ KIWE CHOMBO CHA ULINZI NA MAENDELEO YA WANANCHI


Happiness Katabazi

KUNA msemo usemao ‘Wanajeshi/askari ni mbwa wa Mfalme’.

Kama msemo huu ni kweli au sikweli si hoja ya makala hii. Makala hii inalenga Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), ni chombo chenye nidhamu na kikitumika vizuri kinaweza kuliletea taifa letu neema kubwa.


Jukumu mojawapo la msingi la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wa amani, ni kusaidia mamlaka za kiraia kulinda usalama wa wananchi na mali zao,mipaka ya nchi na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kutoa misaada ya uokoaji wakati wa majanga na kukarabati miundombinu inapoharibika.

Katika kusaidia shughuli za kijamii, JWTZ kwa muda wote wa uhai wake, imeweza kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa na kujipatia sifa kemkem kutokana na mchango wake, hasa katika uokoaji na urejeshaji miundombinu ya barabara na madaraja wakati wa mafuriko.

Jukumu hilo limekuwa likifanywa na wanajeshi wote, wakiongozwa na wahandisi wa medani wa JWTZ wenye makao makuu yao eneo la Sangasanga mkoani Morogoro, ambao wamebobea katika fani hiyo.

Wahandisi wa medani ndio watalaamu ambao wakati wa vita huwezesha vikosi kusonga mbele kwa kuonyesha njia, kwa kufanya doria na kuchagua sehemu nzuri ya kupitisha vikosi, zana na vifaa. Wao pia husafisha njia kwa kutegua mabomu, kujenga barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Kwa misingi hiyo basi, naona kuna umuhimu kwa taifa letu kuanzisha utaratibu wa kuwatumia wahandisi,mabwana shamba wa JWTZ wakati wa amani ili taifa liweze kupiga hatua ya maendeleo katika sekta ya miundombinu, kilimo na ujenzi.
Jeshi letu hivi sasa lina hazina ya wataalam wa kila fani, lakini baadhi yao taaluma zao hawazitumii ipasavyo kutokana na serikali yetu kutowapa fursa ya kutumia ujuzi wao wakati wa amani.

Sote ni mashaidi kwamba inapotekea maafa na mfano mzuri ni yale yaliyotokea Kilosa,Same na kwingineko wahandisi wa JWTZ wamekuwa wakisukumizwa kutengeneza barabara, kuokoa majeruhi nk., lakini hali hiyo ya pilikapilika hawaipati wakati wa amani.

Pamoja na kuwa na fani ya uhandisi, lakini wanajeshi wote wamefundishwa ukakamavu na kazi zao huzifanya ndani ya muda unaotakiwa.

Ni barabara, madaraja mengi tunayashuhudia yamejengwa na raia wa kawaida, tena kwa gharama kubwa, lakini yamekuwa yakichukua muda mrefu kukamilika,au yakikamilika yanaaribika ndani ya kipindi kifupi na mara nyingine tunaambiwa serikali ndiyo imekuwa ikichelewesha fedha za kuwalipa makandarasi na wakati mwingine tunaambiwa makandarasi hao ni wazembe.

Hakika habari kama hizi hazipendezi kusikiwa maskioni mwa mwananchi yeyote mpenda maendeleo, kwani sote tunafahamu taifa lisilo na miundombinu ya uhakika ni wazi litakuwa linajirudisha nyuma kimaendeleo kwani shughuli za uzalishaji zitakwama kwa kuwa mazao au mawasiliano hayasafirishwi kwa wakati muafaka, hivyo kufanya pato la wananchi na taifa kwa ujumla kukosekana na bidhaa kukosekana sokoni.

JWTZ litumike wakati wa amani katika kudhibiti mipaka na katika udhibitio huo ni pamoja na kuweka uzio wa kiulinzi katika maeneo ambayo yanapenyeka kwa urahisi na maadui wanaoweza kuja kuhuju nchi yetu mfano mzuri wezi wa ng’ombe kule Tarime kwani mpaka huo umekuwa na matatizo kila mara kwa mara.Na hiyo ni kazi ya Jeshi wakati wa amani na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kila mwaka ionyeshe jinsi ambavyo wameimalisha ulinzi.

Serikali iwaijengee uwezo JWTZ iweze kufanyakazi za ujenzi katika maeneo ya vijijini ambayo yanatakiwa yafikike.Maeneo hayo yanaitaji barabara,visima.JWTZ watakapopewa miradi hiyo watatengeneza hizo barabara,watachimba visima kisha watawafundisha wanakijiji hao jinsi ya kutumia miundombinu hiyo na jinsi ya kuzifanyia ukarabati pindi zitakapoaribika kisha wanawakabidhi wanakijiji mradi huo.

Pia wanajeshi wetu waweze kupewa miradi mikubwa ya kilimo , waende huko vijijini kuwasaidia wananchi wenzetu kuwajengea miundombinu ya mashamba makubwa ya kilimo .Kisha wanawakabidhi miradi hiyo wananchi.Na Hapo ndipo tunaweza kusema Kilimo Kwanza kitafanikiwa kwasababu ikumbukwe kinaitaji ujezni wa miundombinu ya umwagiliaji kabla ya kilimo chenyewe.

Katika maeneo mengine wahandishi wa JWTZ wanaweza kwenda vijijini kuwafundisha wananchi jinsi ya kujenga nyumba za kisasa.Hii ni teknolojia ambayo wananchi wanatakiwa wafundishwe,Jeshi likishamaliza kuwafundisha ,idadi kubwa ya wanakijiji itakuwa ikijua kwa vitendo ujenzi wa kisasa.Haya ndiyo mambo ambayo serikali makini kote duniani inafanya kama kweli inataka wananchi wake wapate maendeleo.

JWTZ isitumike tu kwenye kupendezesha magwaride katika sherehe za kitaifa ,mazishi ya viongozi,maafa na kuswagwa kwenda kuimarisha ulinzi kule Pemba nyakati za uchaguzi mkuu.

Huu ni wakati wa zama za maendeleo ya sayansi na teknolojia na hivyo vinapaswa kulikumba jeshi pia na njia mojawapo ya kulifanya liende sambamba na maendeleo hayo, ni kupanua wigo wa utendaji wake na ninafikiri njia mojawapo ni kwa kujishughulisha katika ujenzi wa taifa kwa kutumia rasilimali watu iliyonayo.

Hizi si zama za wanajeshi wetu kutembea na silaha wakati wote, au kulewa pombe muda mrefu pale Upanga Messi,Sabasaba Messi,Muungano Messi-Tabora, kunyang’anyana mabibi mitaani na raia bali kubadilika ili liwe jeshi la ujenzi wa taifa, huku likihakikisha amani na usalama wa mipaka ya nchi yetu.

Tujiulize kipi bora, kuendelea kuwatumia makandarasi toka nje ya nchi kwa gharama kubwa ambao wakimaliza kazi wanaondoka na vifaa vyao au taifa lijinyime na kununua vifaa vyake na kutumia wahandisi wake katika ujenzi wa miundombinu ya taifa letu?

Lengo langu si kupiga vita makandarasi wa nje ili wasipewe tenda, la hasha! Ila kwa kuwa serikali kila kukicha imekuwa ikilia kuwa haina fedha za kutosha kutokana na bajeti ya taifa kuwa tegemezi kwa wafadhili, sasa kwanini hicho kidogo tulichonacho kisizunguke humu ndani ili wananchi na taasisi nyingine za serikali ziweze kufaidika nacho?Tunachokiona fedha nyingi zimeelekezwa kwenye siasa.

Kwani hivi sasa serikali inatumia fedha nyingi kuleta makandarasi toka nje ya nchi kwa ajili ya ujenzi wa barabara wakati jeshi lina wahandisi wengi tu wasiotumiwa ipasavyo.Matokeo yake wanajeshi endapo serikali itakubali kuwatumia wahandisi medani, ni wazi kwamba serikali itatumia fedha kidogo kwa ajili ya kulipa gharama za huduma hiyo.

Nitoe pia changamoto kwa JWTZ kwamba, kama kweli nayo ina nia njema na taifa hili na inapenda kuona miundombinu ya taifa lao ikiimarika, pia nayo ina jukumu la kuikomaria serikali iiwezeshe na kisha iwaruhusu kufanya kazi za kuboresha miundombinu wakati wa amani.

Naamini fedha za kununulia vifaa vya ujenzi wa miundombinu kote nchini tukiwa na nia ya dhati tunaweza kuzipata, kwani nchi yetu ina utajiri mwingi wa rasilimali, ambao tukiutumia vizuri, unaweza kutupatia haraka fedha hizo.

Yawezekana wakawapo watakaosema kuwa jeshi halina vifaa vya kutosha vya kuweza kufanya shughuli hiyo, sawa, lakini hatuoni sababu ya JWTZ kutowezeshwa ili waweze kununua vifaa hivyo ambavyo vitakuwa ni mali yetu ya kudumu na tutakuwa tukivitumia muda wowote tunapovihitaji kuliko hali ilivyo hivi sasa ambako tunatoa tenda kwa wahandisi wa nje ambao huongeza gharama kwa kuingiza vifaa vya ujenzi na bado hujinufaisha kwa kuviuza mara wanapomaliza kazi zao.

Naona wakati umefika kwa serikali ya awamu ya nne ambayo kwa bahati nzuri inaongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye kabla ya kuingia kwenye ulingo wa siasa alikuwa ni ofisa wa jeshi hili, na wakati akiomba kura kwa wapiga kura aliahidi kuwa atayatupa majeshi yote, aketi kitako kwa kushirikiana na Wizara ya Miundombinu ione jinsi ya kuwashirikisha wahandishi wa jeshi kwenye ujenzi wa miundombinu ya taifa hata wakati wa amani.

Na endapo hilo litafanyika basi litakuwa limesaidia sana wanajeshi wetu kuondokana na ile dhana ya utani wanayaoitumia wawapo mafunzoni au kwenye messi zao wakipata ‘moja moto moja baridi’ ya “3WWWs’.Tafrsi yake ni War,Women and Wine’,yaani mwanajeshi lazima atekeleze kwa vitendo vitu hivyo vitatu ,yaani vita, wanawake na mvinyo.

Ikumbukwe endapo wanajeshi wetu akiwamua kuitekeleza kikamilifu utani huo kwa vitendo ni wazi kabisa wanajeshi wetu wengi watateketea kwa gonjwa la ukimwi.

Rais Kikwete haitoshi kuona ukiteua baadhi ya maofisa wa JWTZ kuwa wakuu wa mikoa na wilaya. Kama ulivyoweza kuteua maofisa hao kuja uraiani kufanya kazi, vivyo hivyo tunataka kuona wahandisi medani wa jeshi hilo wakitumiwa na serikali yako katika shughuli za ujenzi ,ukarabati na ujenzi wa miundombinu ili taifa lipate maendeleo kwa kukimbia kama sote tunavyotamani.

Wanajeshi madaktari na fani nyingine ndani ya jeshi hilo, tunaona hivi sasa wamekuwa wakitumia fani zao vizuri kwa sababu kuna hospitali zinazoeleweka ndani ya jeshi hilo ambazo zimekuwa zikitoa huduma bora za matibabu tena kwa nidhamu hata kwa raia. Na mfano halisi ni kile kikosi cha 521KJ cha Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo Dar es Salaam, kinachoongozwa na Meja Jenerali Salim Salim.

Ni vyema tukumbuke kuwa, mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe, hivyo basi Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe na si wageni. Sote kwa pamoja tujifunge mkanda bila kubaguana katika kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa taifa na naamini tutafanikiwa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Januari 10 mwaka 2010

1 comment:

Anonymous said...

Wazo ni zuri sana,pia itakuwa ni wakati wa watu wenye elimu zao kuzitumia.Kwani nchi za huku Ulaya wanatumia Jeshi katika mambo mengi kuliko makampuni.Jeshi linatakiwa kuwa na wasomi ambao ni walinzi wa Taifa,Ambao elimu yao inatumika katika maendeleo ya taifa.Nimeipenda sana hii article kwani kufanya vitu wenyewe sio ubishi bali ni ufanisi,kila siku hakuna kazi barabara mbovu na siasa zisizo na maendeleo,Tanzania tunakwenda wapi.Natumaini hili litafanyiwa kazi japo sidhani kwa sasa na hawa mafisiwenye Asidi.

Powered by Blogger.