Header Ads

MAHAKAMA KUU YATENGUA UAMUZI KESI YA JEETU PATEL

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kusimamisha usikilizaji wa kesi ya wizi wa Sh bilioni 7.9 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu, inayomkabili Mfanyabiashara maarufu Jayantkumar Chandubhai Patel maarufu ‘Jeetu Patel na wenzake wawili.


Uamuzi huo ulisomwa jana Katika Mahakama ya Hakimu MKazi Kisutu na Kiongozi wa Jopo la Mahakimu Wakazi Rwaichi Meela anayesaidiana na John Khayoza na Grace Mwakipesile ambapo kabla ya kuusoma uamuzi huo alisema uamuzi huo ni maelekezo yaliyopewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Semistocles Kaijage.

Rwaichi alisema maelekezo hayo ya Mahakama Kuu kwa jopo lake,alisema yamefikiwa baada ya mahakama kuu kupitia maombi ya washitakiwa yalitoka Kisutu na kufikishwa hapo na Kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa mahakamani hapo na washitakiwa hao na akabaini kuwa maombi yote yanafanana.

Jeetu na wenzake mwishoni mwa mwaka jana waliwasilisha katika Mahakama ya Kisutu ombi la kutaka usikilizwaji wa kesi yao katika Mahakama ya Kisutu usimamishwe na jarada la kesi hiyo lipelekwe Mahakama Kuu kwaajili ya kutumika katika kesi ya Kikatiba waliyoifungua dhidi ya serikali, ombi ambalo Oktoba 26 mwaka jana, lilikubaliwa na jopo la mahakimu wakazi hao ambao walisimamisha usikilizwaji kesi hiyo hadi kesi ya Kikatiba itakapotolewa uamuzi.

“Natengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu uliosimamisha usikilizaji wa washutakia kwasababu korti kuu imebaini kwamba maombi hayo yanafanana na yale waliyoyawasilisha kwenye kesi yao ya Kikatiba ambayo yapo katika Mahakama Kuu”alisema Rwaichi kwaniaba ya Jaji Kaijage.

Baada ya kusomwa kwa maelekezo hayo, wakili wa utetezi Gabriel Mnyere aliomba kesi hiyo ije kwaajili ya kutajwa ili wapate nafasi ya kutafakari maelekezo hayo na pia akaiomba mahakama hiyo iwaruhusu washitakiwa waweze kutembelea ofisi zao katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Pwani, Morogoro,Tabora,Arusha,Mtwara na Zanzibar kwaajili ya kuzungukia kampuni zao kwani bila ya hivyo kampuni hizo zitakufa na zikifa Watanzania walioajiriwa katika kampuni hizo wanazoziongoza watapoteza ajira na kwamba wapo tayari kuripoti kwa Wakuu wa Upelelezi kila watakapokuwa wakifika katika mikoa hiyo.

Hata hivyo Wakili Mwandamizi wa Serikali,Fredrick Manyanda na Oswald Tibabyekoma walipinga vikali hoja ya upande wa utetezi yakutaka kesi hiyo ije kwaajili ya kutajwa tu kwa kile alichodai kuwa ombi hilo si la msingi na kuongeza kuwa kesi hiyo ni ya muda mrefu kwani ilifunguliwa tangu Novemba 4 mwaka 2008 na upelelezi ulishakamika na upande wa mashitaka upo tayari kwaajili ya kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao.

Aidha wakili wa serikali Tibabyekoma alipinga tena ombi la washitakiwa wasipewe ruhusa ya kusafiri nje ya Dar es Salaam,kwasababu ombi hilo limeletwa kwa kiapo na siyo ombi kama inavyopaswa iwe kisheria na kufafanua kuwa hati ya kiapo kisheria ni ushahidi wa kwamba ombi husika limeletwa au linatarajiwa kuletwa mahakamani.
Hata hivyo Hakimu Mkazi Rwaichi alisema amesikiliza maombi ya pande zote mbili na akaairisha kesi hiyo Januari 20 mwaka huu, ambapo siku hiyo ndiyo jopo hilo litakuja kwaajili ya kutoa uamuzi wa maombi hayo.

Mbali na Jeetu washitakiwa wengine ni Devendra Patel na Amin Nandy wanaotetewa na Mabere Marando.

Novemba 4 mwaka 2008 , ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kati ya Agosti na Desemba 2005 ndani ya jijini la Dar es Salaam, washitakiwa hao waligushi nyaraka mbalimbali na zilizoonyesha kampuni yao ya Bencon International Limited imepewa idhini ya kurithi deni la kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan na kufanikiwa kuiba sh 7,962,978,372.48 mali ya Benki Kuu ya Tanzania.

Juni 4 mwaka jana, Jeetu na wenzake walifungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inayosikilizwa na jopo la majaji watu wanaongozwa na Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu, Geofrey Shahidi na Semistocles Kaijage. inaendelea kusikilizwa ambapo upande wa walalamikaji na wadaiwa wameishawasilisha utetezi wao na imepangwa kuanza kusikilizwa Novemba 2 mwaka huu.

Katika kesi hiyo, Jeetu na wenzake wanamshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Reginald Mengi na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwamba kwa nafasi zao walishindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu baada ya mdaiwa wa pili (Mengi) kuwahukumu kupitia vyombo vya habari kabla ya kesi zao nne zilizofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu kutolewa hukumu.

Jeetu na wenzake walifungua kesi hiyo ya kikatiba Na. 30 wakiomba Mahaka ma Kuu itoe tafsiri sahihi ya ibara 13, kifungu 4, 5 na 6 (b) cha Katiba ambacho kinatamka watu wote ni sawa mbele ya sheria na pia itafsiri ibara 13 (6) (b) inayosema mtu yeyote asichukuliwe ana hatia hadi pale mahakama itakapomkuta na hatia.

Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji hao wanadai kuwa wamefikia uamuzi huo wa kuiomba mahakama itoe tafsiri ya ibara hizo za katiba kwa kuwa wanaamini zimevunjwa na Mengi ambaye Aprili 23, mwaka huu, alitumia vyombo vya habari kuwahukumu kwa kuwaita ‘Mafisadi Papa’ wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayosikiliza kesi zao haijatoa hukumu.

Uamuzi wa kusimamaishwa kwa kesi hii iliyofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu , ulikuwa ni uamuzi wa tatu kutolewa katika kipindi cha Oktoba mwaka jana, mahakama hiyo ilitoa amri ya kusimamishwa kuendelea kwa kesi ya wizi wa sh bilioni 9, kesi ya wizi wa sh 3.9 zinazowakabili washitakiwa hao hadi kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na washitakiwa hao itakapotolewa uamuzi.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi nne za wizi wa fedha katika Akaunti ya EPA katika Mahakama ya Kisutu ambazo zilifunguliwa Novemba mwaka juzi. Mbali na Jeetu, washitakiwa wengine ni Devendra Vinodbhai Patel, Amit Nady na Ketan Chohan

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Januari 16 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.