JOHN VICENT MATTAKA
Abuni njia rahisi ya kufahamu hisabati
*Agundua tatizo ni njia za ufundishaji
*Aja na njia yake mpya, aiita ni mkombozi
Na Happiness Katabazi
KILIO cha wanafunzi wengi hapa nchini hususan katika shule za msingi na sekondari ni kutolipenda somo la hisabati. Na hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa wanafunzi walio wengi kwa miaka mingi hapa nchini.
Ufaulu wa masomo ya lazima katika matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka uliopita unaonyesha kuwa somo la Kiswahili linaongoza likiwa na asilimia 81.59 ya ufaulu, likifuatiwa na Kiingereza (63.23). Somo la siasa likishika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 62.09, likifuatiwa na jiografia (58.97) na la mwisho ni hisabati ambapo ufaulu ni asilimia 24.
Si sekondari pekee, adha hii ya matokeo mabaya katika somo la hisabati imekuwa ikiwakumba pia wahitimu wa shule za msingi kila mwaka.
Sababu zinazotolewa na wanafunzi hao ni kwamba somo hilo ni gumu na hawawezi kulimudu, hali iliyosababisha wanafunzi wengi kukimbia na kukimbilia kuchukua masomo ya michepuo mingine ambayo wamekuwa wakidai ni nafuu kwao.
Jambo ambalo serikali na wadau wa sekta ya elimu wasipolitafutia umbuzi wa tatizo hilo, mwisho wa siku taifa litajikuta lina wataalamu wachache wa hisabati na biashara.
Katika makala hii mwandishi wa gazeti hili amefanya mahojiano na mgunduzi wa njia rahisi za kufahamu na kulielewa somo la hisabati kupitia ugunduzi wa utafiti unaojulikana kama PEACEFUL START, Mtanzania John Vincent Mattaka (43) ambaye anaanza kwa kusema:
“Falsafa ya Peaceful Start inafanana sana na falsafa ya taasisi za tiba. Ubora wa taasisi ya tiba unadhihirika pale unapomsaidia yule ambaye ni mgonjwa zaidi kupata ahueni, au kupona kabisa. “Vivyo hivyo kwa Peaceful Start ina wigo mpana wa ubora wa kitaaluma unaochochea fikra za ubunifu, usiowaacha kando hata wale wanaodaiwa kuwa na uelewa mdogo, wale wanaosuasua darasani na kuonekana mzigo kwa wanaowafundisha.
“Hawa wakinolewa kifikra na vionjo vya Modeli-bunifu ya Peaceful Start, wanabadilika haraka na pengine hata kuwazidi wale ambao kabla ya hapo walikuwa wanawapita kwa uelewa.”
Mattaka anabainisha kuwa mwaka 1989 Chama cha Hisabati (CHAHITA) kilimteua kuwa miongoni mwa watu waliokwenda kushiriki katika Olimpiki ya Hisabati iliyoandaliwa na Muungano wa Vyama vya Hisabati vya nchi za Afrika (The African Mathematical Union ) huko Ibadan - Nigeria.
Anasema akiwa Ibadan alipata changamoto iliyomsukuma kujikita katika utafiti ulioleta ugunduzi huo. Changamoto hiyo iliyomgusa ilikuwa ya kuambiwa kuwa Bara la Afrika halimo kabisa katika ramani ya ulimwengu wa hisabati.
Anasema alipohitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1993, aliamua kutoajiriwa. Badala yake alijikita katika utafiti wa hisabati kwa lengo mahususi la kujibu ile changamoto kwa kupata ujuzi mpya utakaolistahilisha Bara la Afrika katika ramani ya wachangiaji mahiri wa somo la hisabati duniani.
Alitaka kuwafunulia Watanzania, Waafrika na wengineo kuhusu fikra za uoni wa ndani wa sifuri hadi tisa ambao yeye anauona kuwa ni wa msingi sana katika kulielewa somo la hisabati kwa wanaofundisha na wanaojifunza.
Hata hivyo, baada ya kuukamilisha utafiti kwa kupata njia bunifu, rahisi na mbadala ya kufundisha na kujifunza hisabati, bado aliona wanafunzi wengi hawaelewi hisabati haraka na kwa kiwango alichotarajia. Akagundua kuwa lugha nayo ilikuwa ni kikwazo kinachochangia ugumu wa somo hilo.
Hivyo aliamua kuzama na kujikita tena katika utafiti kwa nia ya kupata njia bunifu, rahisi na mbadala za kufundisha na kujifunza Kiingereza na Kiswahili na akafanikiwa kupata njia inayojulikana kama ‘SuVerbA ya kujifunza Kiingereza na ya ‘Abadafaga’ kwa somo la Kiswahili.
“Kutokana na ugunduzi huo tunawatangazia kwamba tatizo linaloonekana kuwa ni sugu la ugumu wa hisabati na Kiingereza limeshapata ufumbuzi kupitia ugunduzi huu wa Peaceful Start. Hivyo wanafunzi wanaodaiwa kuwa na uelewa mdogo katika kujifunza, wakiwekwa chini ya mfumo wa Modeli-bunifu ya Peaceful Start wanabadilika haraka,” anasema.
Anasema walengwa wao wakuu ni wanafunzi wa ngazi ya shule ya msingi. kujijengea upekee wa kueleweka kama wataalamu waliobobea katika ujenzi wa misingi imara ya usomaji na ufundishaji. Hivyo wanafunzi wa shule za msingi ndio walengwa wetu wa kwanza na kuongeza kuwa kulegalega kwa ubora wa elimu kwa ngazi za sekondari na vyuo kunaashiria makosa yalilofanyika kwenye ngazi ya elimu ya msingi.
Anahoji kwani Kiingereza ni kigumu kiasi gani hadi mtu afike chuo kikuu hajakijua, nako huko wahangaike kumfundisha? Hata hisabati si ngumu kiasi hicho kinachovumishwa.
Walengwa wao wakuu kama alivyotangulia kusema ni wanafunzi wa ngazi ya shule ya msingi. Kama jina lao lilivyo PEACEFUL START ina azima ya kujijengea upekee wa kueleweka kama wataalamu waliobobea katika ujenzi wa misingi imara ya usomaji na ufundishaji wa somo la hisabati.
Anasema licha ya yeye kuwa mtafiti wa taasisi hiyo pia taasisi hiyo ina Katibu Mkuu wake ambaye ni Brigedia Jenerali Mstaafu Gerald Kiswaga, ambaye ndiye anajishughulisha na shughuli za utendaji wa taasisi hiyo.
Taasisi hiyo ya kiraia ilisajiliwa kisheria mwaka (2005), ili kuwezesha matokeo ya utafiti uliofanywa kwa njia bunifu, rahisi na mbadala za kufundisha na kujifunza hisabati, Kiingereza na Kiswahili kutumiwa na walengwa waliomo katika sekta ya elimu na mafunzo na utafiti aliufanya kwa miaka 15.
Anasema katika dunia ya leo ushiriki wa wananchi wake kwenye biashara ya mtandao wa kompyuta (e-commerce) ni miongoni mwa vigezo muhimu vinaovyoonyesha kukomaa kwa uchumi wa nchi husika.
Katika hilo, mtafiti huyo anasema kuwa hatuwezi kuingia kwenye ushiriki wa namna hii ya biashara ya kisasa iwapo bado tuko nyuma kwenye umahiri wa masomo ya sayansi na tekonolojia ambayo moja kwa moja yanahusisha somo la hisabati.
“Kwa hiyo sayansi na tekonolojia haiwezekani iwapo umahiri wetu wa kujifunza na kufundisha hisabati na lugha utazidi kuwa ni huu usioridhisha hata kidogo.
Anasema yawapasa wajizatiti vilivyo, vinavyogunduliwa hapa kwetu tuvilinde kwa hatimiliki husika na tuvitangaze kwa nguvu zote na hatimaye tuviuze ili nasi tupate fedha za kigeni kupitia hivyo.
“Tumefikia wakati somo la hisabati limekuwa kama janga la taifa. Hivyo ni vema tukampa nafasi yeyote atakayedai kuwa na ufumbuzi juu ya suala hili, akasikilizwa.
“Kwa hali ilivyo sasa ki-hisabati, kesho yetu, haina matumaini hata kidogo. Hivi tutawapataje wataalamu wa fani mbalimbali kama vile za ualimu, udaktari, uhasibu, urubani, kilimo, ulinzi na usalama, kompyuta, biashara, uchumi, na wengineo?” anasema.
Kwa mantiki hiyo, anasema taasisi hiyo ni hazina yenye rasilimali kubwa na muhimu , lakini baya zaidi ipo tu bila kujua hatima ya itakavyotumika na kutusaidia.
Anasema iwapo watapata ushirikiano wanaotarajia kutoka kwa wadau mbalimbali wataweza kuusimika mfumo wa utoaji elimu bora na endelevu.
Ni matumaini yao kuwa katika muda mfupi wataweza kuboresha maendeleo ya sekta ya elimu na mafunzo hapa nchini, Afrika na hata dunia nzima.
Mtafiti huyo anasema kuwa, ugunduzi na utaalamu huu ukianza kutumika na kusambaa nje ya nchi utachangia kwa kiwango kikubwa suala zima la ajira na pato la fedha za kigeni.
Mattaka ni baba wa watoto watatu. Mwaka 1975-1981 alisoma Shule ya Msingi Mwongozo, wilayani Newala. Mwaka 1986-1988 akajiunga na Shule ya Sekondari ya Tosamaganga, Iringa na mwaka 1982-1985 alisoma Shule ya wavulana ya Songea.
0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Januari 21 mwaka 2010
No comments:
Post a Comment