Header Ads

KIKWETE AZULIWA JAMBO

• ADAIWA KUMTAKA MTIKILA KWENYE MTANDAO WAKE

Na Happiness Katabazi

MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila ambaye ametupwa lupango baada ya kufutiwa dhamana kwa kosa la kushindwa kujiheshimu, amedai hatua hiyo imetokana na msimamo wake wa kukataa kuingizwa kwenye mtandao wa kumsaidia Rais Jakaya Kikwete ashinde.


Tayari hivi sasa kuna madai ya kuwapo kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani ambao wako katika mtandao unaojulikana kama ‘Saidia Jakaya Kikwete Ashinde’.

Baadhi ya viongozi wanaotajwa na ambao siku za hivi karibuni wamekuwa wakitoa kauli za kuwashambulia wanaompinga Rais Kikwete, ni pamoja na Rais wa Chama cha TADEA, Lifa Chipaka, Mwenyekiti wa UPDP, Fahmir Dovutwa na Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema.

Mtikila alitoa madai hayo mazito ya kukataa kuingizwa kwenye mtandao huo wa Rais Kikwete juzi, muda mfupi kabla ya kuwekwa mahabusu kwa kosa la kutojiheshimu na kuruka dhamana.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa njia simu, Mchungaji Mtikila ambaye ana historia ya kukabiliana na kesi za kashfa dhidi ya viongozi wa juu serikalini, alisema Jumatano ya wiki iliyopita, aliitwa na Katibu wa Rais Kikwete, Kassim Mtawa katika Hoteli ya Kempinski ya jijini Dar es Salaam na kuwa na mazungumzo ya faragha.

Mtikila ambaye amepata kuhukumiwa kwenda jela mwaka mmoja kwa kosa la kumkashifu Mwalimu Nyerere, alidai kuwa alipofika hotelini hapo alikutana na Mtawa na kuelezwa kuwa lengo la kikao chao ni kutaka ajiunge kwenye mtandao wa Saidia Kikwete Ashinde katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

“Mtawa alinipa majukumu matatu; moja ni la kuitisha mkutano na vyombo vya habari na kutoa kauli ya kuwalaani wote waliomshambulia Rais Kikwete kwenye mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, pili alinitaka niitishe mkutano na wanahabari ili niweze kuunga mkono utabiri wa Sheikh Yahya Hussein na tatu, niwachafue wote wanaotaka kujitokeza kumpinga Rais Kikwete ndani ya CCM.

“Mimi nilikataa katakata kufanya kazi hiyo kwani kwangu mimi huo ni udhalimu kwa sababu ninamuogopa Mungu na kuheshimu katiba ya nchi na suala la kugombea nafasi yoyote ni haki ya kila mtu kikatiba,” alisema Mtikila kwa sauti ya upole.

Aliendelea kudai kuwa katika mazungumzo yao, Mtawa alimuahidi kuwa endapo angekubali kufanya mambo hayo matatu, angepewa fedha nyingi za kuendeleza familia yake.

Hata hivyo Mtikila alipoulizwa kama katika mazungumzo hayo hakuchukua kiasi chochote cha fedha, alisema alizikataa kwani alikataa kuingizwa kwenye mtandao huo.

Akizungumzia madai hayo dhidi ya Rais Kikwete kwa njia ya simu, Katibu wa Rais, Mtawa alikanusha na kuyaita ni ya uongo na uzushi wa hali ya juu.

“Jamani huo ni uongo wa hali ya juu. Mimi sijakutana na Mtikila kama anavyodai. Kwanza mimi si niliyemshitaki. Mtu anapofutiwa dhamana maana yake amevunja masharti ya dhamana, ameyakiuka mwenyewe, ndiyo maana mahakama imemfutia dhamana.

“Tena mimi si Msajili wa Mahakama, sasa nashangaa anavyotaka kuniingiza kwenye mambo yasiyo na msingi… Huyo Mtikila ni muungo, tena nashukuru sana umenipa nafasi ya kujieleza,” alisema Mtawa.

Juzi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, ilimfutia dhamana Mtikila kwa madai ya kushindwa kujiheshimu.

Amri hiyo ya kumfutia dhamana ilitolewa na Hakimu Mkazi Waliarwande Lema baada ya kusikiliza utetezi wa mshitakiwa ambaye alifika katika viwanja vya mahakama hiyo saa tano asubuhi akiwa amechelewa na ghafla alijikuta akikamatwa na askari polisi wa mahakamani hapo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Mtikila alipaswa kufika mahakamani hapo majira ya saa tatu asubuhi wakati kesi hiyo ilipotajwa, lakini hakuwepo, ndipo Wakili wa Serikali, Beatrice Mpangala aliomba hati ya kukamatwa kwa mshitakiwa.

Kabla ya Mtikila kukamatwa, aliiambia mahakama kwamba alidamka mapema na kumtafuta daktari wake aliyemtaja kwa jina moja la Katembo, ambaye alimfanyia upasuaji baada ya kugongwa na nyoka aina ya kobra wakati alipokuwa katika shughuli za kidini nchini Zimbabwe mwaka jana.

Alisema alijitahidi kuwatafuta wadhamini wake ili wafike mahakamani kwa niaba yake, lakini hakuweza kuwapata, ndiyo maana alikuja mwenyewe mahakamani hapo akiwa na maumivu makali mwilini mwake.

Hata hivyo hakimu Lema alieleza kutoridhishwa na utetezi huo na kuamuru Mtikila atupwe rumande hadi Januari 25 kesi yake itakapotajwa tena.

Hii ni mara ya pili kwa Mchungaji Mtikila kushindwa kufika mahakamani wala wadhamini wake. Mara ya kwanza ilikuwa Oktoba 22, mwaka jana.

Mchungaji Mtikila anakabiliwa na kesi ya uchochezi namba 1767/2007.

Ilidaiwa kuwa alitoa maneno ya uchochezi na kashfa dhidi ya Rais Kikwete kwa kumuita gaidi kwa madai kuwa serikali anayoiongoza inataka kuanzisha Mahakama ya Kadhi, jambo ambalo ni kinyume na katiba ya nchi.

Chanzo:Gazeti la Jumatano ,Januari 13 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.