Header Ads

HATIMA YA LIYUMBA APRILI 9

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imesema kuwa Aprili 9, mwaka huu, itatoa uamuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), anayekabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, iwapo ana kesi ya kujibu au la.
Sambamba na hilo, hatimaye jana upande wa Jamhuri ulitangaza rasmi kuifunga kesi hiyo.

Kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Edson Mkasimongwa, anayesaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa, alitoa amri hiyo baada ya kusikiliza malumbano ya kisheria yaliyotolewa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Juma Mzarau na Ben Lincoln na wakili wa utetezi, Majura Magafu, aliyekuwa akisaidiwa na Jaji Hillary Mkate, Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke.

Hakimu Mkazi Mkasimongwa alisema kuwa anakubaliana na maombi ya pande zote yaliyohusu mahakama kuwapatia fursa ya kuwasilisha majumuisho yao ya kumuona mshitakiwa ana kesi ya kujibu na kuongeza kuwa jopo lake limefikia uamuzi wa kuzitaka pande zote mbili kuwasilisha majumuisho hayo kwa njia ya maandishi.

“Hivyo natoa amri kwamba upande wa utetezi uwasilishe majumuisho yake kwa njia ya maandishi mahakamani Machi 22 na upande wa mashitaka uwasilishe majumuisho yake mahakamani Machi 29 na kwamba kesi hii itakuja kutajwa Machi 26 na mahakama hii itatoa uamuzi wa mshitakiwa kama ana kesi ya kujibu au la Aprili 9, mwaka huu,” alisema Mkasimongwa.

Awali kabla ya uamuzi huo kutolewa, wakili Mzarau aliikumbusha mahakama kuwa shauri hilo lilikuwa limepangwa jana kuendelea na mashahidi wa upande wa mashitaka, lakini baada ya wao kupitia kwa kina nakala ya mwenendo wa kesi hiyo ulionyesha ni mashahidi wanane waliotoa ushahidi na vielelezo 13 vilitolewa mahakamani hapo na wamefikia hatua muafaka ya kuifunga kesi yao kwa mujibu wa kifungu cha 231 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

Baada ya Mzarau kutoa maelezo hayo, wakili wa utetezi Magafu aliinuka na kuomba mahakama iwaruhusu jana hiyo hiyo waweze kuwasilisha majumuisho yao kwa njia ya mdomo, ya kwamba mteja wake (Liyumba) hana kesi ya kujibu.

Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa na wakili Mzarau, kwa madai kuwa wanahitaji wapate muda wa kujiandaa na kwamba wanaiomba mahakama majumuisho hayo ya mshitakiwa kama ana kesi ya kujibu au la, wao na upande wa utetezi wawasilishe majumuisho hayo kwa njia ya maandishi ili waweze kuisaidia mahakama kufikia maamuzi sahihi.

Kabla ya uamuzi huo wa jana wa upande wa mashitaka kuifunga kesi hiyo, wakati wakimsomea maelezo ya awali Liyumba, waliiambia mahakama kuwa wanakusudia kuleta mashahidi kumi na ilipofika hatua ya mshitakiwa wa tatu wakati anatoa ushahidi wake, upande wa mashitaka uliongeza idadi ya mashahidi na kufikia mashahidi 15.
Kwa idadi hiyo, hadi kufikia jana upande wa mashitaka umeweza kuleta jumla ya mashahidi wanane tu.

Januari 27, mwaka jana, Liyumba na Meneja Mradi wa Benki Kuu, Deogratius Kweka, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashitaka hayo ya kuidhinisha mradi wa majengp ya minara pacha bila idhini ya bodi ya wakurugenzi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Mei 27 mwaka jana, mahakama hiyo iliwafutia kesi, lakini muda mfupi baada ya kuachiliwa walikamatwa tena mahakamani hapo na Mei 28 mwaka jana Liyumba peke yake ndiye aliyerudishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka hayo na Kweka akawa ameachiliwa huru.

Tangu kipindi hicho hadi sasa Liyumba anaendelea kusota rumande, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ambapo mahakama ilimtaka atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh bilioni 111.


Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne,Machi 16 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.