Header Ads

RITES IWE MWANZO,TUMULIKE NA KWINGINE

Na Happiness Katabazi

MACHI 12 mwaka huu, Baraza la Mawaziri chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete lilifikia uamuzi wa kujadiliana na Kampuni ya RITES ambao ndio waendeshaji Shirika la Reli Tanzania (TRL) ili iweze kununua hisa zinazomilikiwa na mwekezaji huyo.

RITES ni wawekezaji kutoka India, wenye hisa 51 ndani ya TRL huku serikali ikiwa na hisa 49, kutokana na wingi wa hisa mwekezaji huyo amekuwa na sauti kubwa zaidi kuliko serikali.

Pamoja na nguvu hizo bado mwekezaji huyo ameshindwa kuboresha huduma za TRL na kadiri siku zinavyosonga ndivyo mambo yanavyozidi kuwa mabaya kiasi cha kulifanya baraza la mawaziri kuamua kununua hisa za mwekezaji ili TRL irudi mikononi mwa serikali.

Ujio wa RITES umekuwa chanzo kikubwa cha kuzuka kwa migomo ya mara kwa mara kati ya wafanyakazi na menejimenti yao, ugomvi wa abiria na wafanyakazi na vitendo mbalimbali vyenye kushusha hadhi ya kampuni husika.

Hivi sasa si jambo la ajabu kusikia uahirishwaji wa safari, ubovu wa mabehewa na kero nyinginezo ambazo zimezorotesha usafiri pamoja na kukwamisha mizigo ya wateja.
Tathmini ya kiasi cha fedha kilichopotea kutokana na kulega lega kwa huduma za TRL ikifanyika, nina hakika tutapata mshtuko wa kile tutakachoelezwa hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu imekuwa ikipambana na kuondoka katika shimo la umaskini.

Kimsingi tukubaliane migomo iliyokuwa ikifanywa na wafanyakazi wa TRL imekuwa ikiipaka matope serikali yetu mbele ya wananchi walioiweka madarakani.

Binafsi nilikuwa miongoni mwa wananchi tuliokuwa tukiilalamikia serikali kwa kitendo chake cha kuendelea kuikumbatia RITES, ambapo wakati mwingine ililazimika kuttoa fedha kuwalipa mishahara wafanyakazi wa TRL.

Makala za kila aina kuilalalmikia serikali juuu ya kuibeba kampuni hiyo ziliandikwa, miongoni mwa makala za kuilalamikia serikali kuhusu mwekezaji huyo ni ile iliyochapishwa katika gazeti hili Aprili 27, mwaka 2008 iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Serikali isikumbatie wawekezaji wababaishaji’.

Binafsi nimefarijia na kusudio hilo la baraza la mawaziri lakini nimekaa na kutafakari kwa kina juu ya mtiririko mzima wa malalamiko ya wananchi dhidi ya mwekezaji huyo na ninajiuliza maswali yafuatayo:

Uamuzi huo wa baraza la mawaziri si janja ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutaka kupata kura za wafanyakazi wa TRL kiulaini kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba?

Je, uamuzi huo si wa kuwapaka mafuta Watanzania kwa mgongo wa chupa? Hivi serikali inataka kununua hisa 51 hewa? Hawa RITES hata mishahara ya kuwalipa wafanyakazi walishindwa kuitoa sasa wana kipi hasa?

Nimefurahia mawaziri kugutuka dhidi ya wawekezaji ‘uchwara’ na wanafanya taratibu za kisheria kutaka kununua hisa za RITES ambazo kwa maneno mengine naweza kuita kuwa serikali itavunja mkataba wa mwekezaji huyo.

Mara kadhaa tumeshuhudia maamuzi ya jazba yenye kukinzana na sheria yakitumika kuvunja mikataba mbalimbali ambayo mwisho wake huitokea puani serikali ambapo fedha za wavuja jasho hutumika kulipa fidia kwa wakezaji ambao mara wasikiapo maamuzi hayo huenda katika mahakama kudai haki zao kwa kuvunjwa kwa mikataba.

Itakumbukwa mara kadhaa sera ya ubinafsishaji wa mali za umma ilikuwa ikilalamikiwa kuwa ni mbovu lakini viongozi walionekana kuweka pamba masikioni.

Sera hii imejikita kwenye msingi wa kuwanyenyekea na kuwaona miungu watu wawekezaji wajao hapa nchini huku ikiwasahau wananchi ambao kwa muda mrefu ndio waliokuwa wakiuhudumia mradi, kiwanda au kampuni husika.

Kundi kubwa la wananchi limesahaulika, halitazamwi kuwa nalo linaweza kuwa wawekezaji wazuri zaidi kama litajengewa mazingira mazuri ambayo yatawafanya waungane kwa lengo la kupata mtaji mkubwa ili kununua mali inayobinafsishwa.

Inawezekana kabisa mali tulizokuwa nazo zingeweza kuwa mikononi mwetu kama tungejenga uwazi na mazingira mazuri ya kuwabinafsishia wazawa mali zao badala ya kuwafikiria wageni ambao kila kukicha wamekuwa na ghiliba mpya za kuchuma na si kuendeleza nchi.

Shirika la Reli limebinafsishwa kwa Kampuni ya RITES ambayo uwezo wake umeonekana mdogo, licha ya kuwa wakati likipewa zabuni ya ushindi kulikuwa na mbwembwe za kuuaminisha umma kuwa nguo imepata mvaaji.

Zipo nchi nyingi ambazo zinasifika kwa kuwa na teknolojia ya kuendesha reli kuliko India ambao ndiyo tumewapa TRL ili wagange njaa badala ya kuiboresha kwa viwango vinavyokubalika kwa watumiaji.

Ujerumani, Japan, China na Ufaransa ni miongoni mwa nchi zilizo mstari wa mbele katika teknolojia hiyo, inashangaza kwamba Watanzania tulijiingiza kwa mwekezaji asiye na uwezo mkubwa tena kwa miaka 25 ijayo.

Nyimbo zilizokuwa zikiimbwa tangu awali ni kuwa mwekezaji ataleta vichwa vipya, injini mpya na mabehewa mapya lakini matokeo yake wote tumeyaona, kwani hata kile tulichokuwa nacho awali sasa hakiwezi kutusaidia au kimepotea katika mazingira ya kutatanisha.

Tunapaswa kujiuliza, ni nani katuroga au tumekosa nini kwa Mungu? Kwa nini tunaendelea kujidhalilisha kwa rasilimali tulizonazo wenyewe?

Mara kadhaa serikali ilikuwa ikichota fedha za kuwalipa mishahara wafanyakazi wa TRL ambapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda ndiye alikuwa mstari wa mbele kutuliza hasira za wafanyakazi, je, fedha za wavuja jasho zitarudije baada ya RITES kuondoka?

Ni vema tukajulishwa kama fedha zetu zimekwenda na maji au tutalipwa kupitia ununuzi wa hisa hizo 51, la sivyo tutaendelea kuilaumu serikali yetu na watendaji wake kwa kuingia ubia na wawekezaji ‘wachovu’.

Kama mwekezaji anashindwa kutekeleza wajibu wake, kisha serikali inambebea mzigo wake, kuna sababu gani ya kuwapamba kwa jina zuri la mwekezaji wakati tukifahamu fika hana uwezo wala sifa hiyo?

Nimalizie kwa kuwaasa viongozi wetu kwamba hakuna sababu ya serikali yetu kuendelea kulea baadhi ya wanasheria na watendaji wake wanaoshiriki katika mchakato wa kuzichagua kampuni za uwekezaji zinazotaka kuwekeza hapa nchini.
Kuna faida gani ya kuendelea kuwalipa mamilioni ya fedha watendaji wanaoliingiza taifa katika hasara kubwa kwa kuingia mikataba mibovu na kampuni hewa ambazo mwisho wake mzigo unaliangukia taifa?
Serikali ni lazima ibadilike na iache tabia ya kuwalinda watendaji wake wanaoweka mbele masilahi binafsi kwa kukubali zawadi na kauli za kuwarubuni kutoka kwa wawekezaji uchwara wenye nia ya kutafuna rasilimali za nchi.
Watendaji wengine wamejikuta wakiingiza nchi matatizoni kwa sababu ya kutoisoma kwa makini mikataba wanayotaka kuingia na wawekezaji, tuna sababu gani ya kuendelea kuwa na watu wa aina hii?
Kuingiza nchi kwenye mikataba ya kinyonyaji ni uhujumu uchumi na uuaji, watu wanaofanya vitendo vya aina hiyo washughulikiwe kwa kuwa wanataka kuwaua wananchi kwa njaa.
Naamini hilo litakuwa funzo kwa wanasheria wa serikali ambao wamesomeshwa kwa kodi za wananchi na wanaendelea kulipwa mishahara na kupewa posho nono pindi wanaposafiri au wanapohudhuria vikao vya kuandaa mikataba hiyo halafu mwisho wa siku shukurani yao kwa serikali ni kuingiza nchi kwenye mikataba isiyo na masilahi ya taifa hili.
Baraza la mawaziri limeonyesha njia, sasa tupige hatua kwa kuanza kuwawajibisha mabingwa wa kuitumbukiza nchi kwenye mikataba mibovu kwa sababu tunawajua na tunaishi nao kwenye jamii yetu.
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema ‘inawezekana, timiza wajibu wako’, kauli hii kwa bahati mbaya haijapata mashiko kwa sababu watu hawatimizi wajibu wao lakini ndiyo hao wanaokuwa mstari wa mbele kulalamikia masilahi duni wanayopata katika kazi zao.

Litakuwa jambo la busara kwa serikali kama itaanza kuweka wazi mchakato wa kumpata mwekezaji pamoja na mikataba yao ili wananchi waweze kujua wanafaidika vipi na mwekezaji husika.

Zama za kuburuzana na kutumia fedha za walipa kodi zimepitwa na wakati, inapaswa kila mtu atimize wajibu wake kulingana na taratibu za kazi.

Uamuzi huu wa baraza la mawaziri usiishie kwa TRL pekee bali uangalie na miradi mingine ya uwekezaji ambayo mpaka sasa imekuwa ikisuasua kwenye uzalishaji kwa sababu ya mmiliki wake kutokuwa na uwezo wa kutosha.

Wananchi wanawajua wawekezaji uchwara na mikataba tata, kila kukicha wamekuwa wakipaza sauti zao hivyo ni vema serikali ikayafanyia kazi malalamiko haya badala ya kuonekana ni walalamishi na wasiowataka wawekezaji.

Halitakuwa jambo jema kama uamuzi huu wa baraza la mawaziri umefanywa kwa kukitafutia chama tawala sifa za kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu, nchi hii ni yetu sote, tunapaswa kuchukia aina zote za unyonyaji.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili,Machi 21 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.