Header Ads

PETER NDEMBO:MCHORAJI ALIYEMDUWAZA JK


MAPEMA wiki iliyopita Rais Jakaya Kikwete alijikuta akipigwa butwaa, baada ya kukabidhiwa picha yake iliyochorwa kwa ustadi wa hali ya juu na mzee Paul Peter Ndembo (64).Mwandishi Wetu Happiness Katabazi aliyefanya mahojiano na mchoraji huyo, anaelezea siri ya mafanikio yake na jinsi alivyofanikisha azima ya kuifikisha picha hiyo mikononi mwa Rais Kikwete.

“Picha yenye sura ya Rais Jakaya Kikwete na Mwalimu Julius Nyerere ambazo nilimkabidhi rais siku hiyo pale Ikulu, nilizichora mimi mwenyewe kwa mkono wangu na hazikwenda pale kwa ajili ya biashara.

“Ukweli ni kwamba picha zile nilikwenda kumkabidhi Rais Kikwete ili zikae katika jengo la Ikulu na zitumike kuipamba Ikulu. Huo ndio mchango wangu mchango wangu kwa Ikulu yetu,” anaanza kwa kusema mzee Ndembo.

Swali: Hapa Tanzania wachoraji ni wengi na wengi wamekuwa wakimchora rais na viongozi wengine wa kitaifa. Unaweza kutueleza kwanini uliamua kuzipeleka picha zako Ikulu?
Jibu: Kwanza ieleweke zile picha nilizomkabidhi rais wetu, zilinichukua muda mrefu kuziandaa na kuzikamilisha kuliko picha zote nilizowahi kuzichora maishani mwangu.
Picha ya Kikwete imenichukua takriban mwezi mmoja na kisha kuihifadhi nyumbani kwangu na hata ukiangalia fremu zake, utabaini kuwa niliziandaa kwa heshima sana kwa kujua siku moja zitaenda kupamba Ikulu yetu.
Lakini likanijia wazo la kuziweka wazi kabla ya kuzifikisha Ikulu ili jamii izione. Mtu ambaye niliona anaweza kuziangalia na kumshawishi ili azima yangu ya kuzifikisha Ikulu itimie ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika.
Niliamua kumpelekea picha hizo mwanzoni mwa Februari mwaka huu. Mkuchika alipoziona, aliniambia nimefanya kazi nzuri na akaniahidi kwamba lazima picha zile zipelekwe Ikulu kwa Rais Kikwete.
Basi, waziri baadaye akafanya mawasisilino na Ikulu na hatimaye nilipangiwa siku ya kwenda nazo Ikulu na kumkabidhi rais. Hakika nimefarijika sana kwani nimetimiza ndoto yangu ya kutaka kuipamba Ikulu yetu.

Swali: Kwanini unapenda kuchora picha za wanasiasa?
Jibu: Nachora picha nyingi, lakini hasa picha za viongozi wa siasa kwa sababu zinakuwa kumbukumbu kubwa ya viongozi waliopo na wastaafu.
Na katika hilo inaonyesha ni jinsi gani tunathamini michango ya viongozi hao. Ikulu yetu na ofisi nyingi za serikali kama mawizara zimejaa picha za viongozi zilizopigwa.

Nilipotembelea Ikulu ya Korea Kaskazini na Uganda miaka ya nyuma, niliona ukutani zimebandikwa picha za viongozi wa nchi zilizochorwa na wasanii wa nchi husika.
Ni picha za kuvutia na hazichoshi kuzitazama, tofauti na picha za kupigwa na kamera hata kwa kutumia kamera za kisasa.

Swali: Tangu ulipomkabidhi Rais Kikwete ile picha uliyoichora sura yake, baadhi ya wananchi wamekuwa wakipiga simu kwenye chumba chetu cha habari wakidai si picha ya kuchora. Unalisemeaje suala hilo?
Jibu: Si kweli kwamba picha ile ni ya kupigwa na kamera. Naomba kuwathibitishia wenye hofu hiyo kwamba, picha ile nimeichora mimi kwa kuigiza moja ya picha za rais zilizotumika kwenye kampeni wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Hivyo nilichukua ‘pozi’ la rais kutoka kwenye picha halisi na kuibadilisha kitaalamu.

Kuna vitu vichache nilivifanya katika picha ya rais, moja ni kuongeza nywele nyingi kwenye picha ya kuchora tofauti na picha halisi.
Macho yake kwenye picha niliyoichora, nimeyafanya yamekuwa angavu, sikio lake linaonekana kukolea rangi ya blauni na koti la sasa lina rangi ya daki blue wakati katika picha halisi, linaonekana alikuwa na rangi ya kijani na nyuzi zilizotumika kutengeneza kitambaa kile cha koti zilikuwa zikionekana, lakini kwenye picha yangu hazionekani hivyo.

Kwa kifupi, picha niliyoichora na kumkabidhi rais, ukiiangalia vizuri inajionyesha kabisa kwamba ni ya kuchora ila kutokana na ustadi nilionao, inaweza kukuchukua muda kubaini hilo.
“Nawashangaa sana hao wanaopinga kwamba ile picha si ya kuchora, kwani hata kuiona kwa macho yao hawajaiona, wameishia kuona runingani,” alisema.

Swali: Unapendelea kuchora picha za aina gani?Jibu: Ninachora portraits (sura za watu), nachora picha za maharusi bila maharusi kujua na siku ya harusi kamati za harusi hizo wanawakabidhi maharusi picha kama surprise, nachora picha za wafiwa.
Kwa mfano kuna watu waliofiwa na waume au wake zao, wapo waliokuja kwangu wakitaka picha za kuchorwa za wenzi wao kama kumbukumbu, nami hufanya hivyo.
Pia nachora picha za stempu na kwa sasa ninapewa kazi ya kuchora stampu na Shirika la Posta. Shirika la Posta liliikubali kazi yangu likaamua kuingia nami mkataba hadi sasa.

Nikishachora shirika hilo hupeleka michoro hiyo nje ya nchi kwa ajili ya kuchapisha stempu tunazotumia.

Ndembo alianza kuchora picha za stempu mwaka 1978, ambazo alizichora picha za maadhimisho ya CCM kutimiza mwaka mmoja. Baada ya hapo alitumika kuchora stempu za matukio mbalimbali.

Kwa mfano amewahi kuchora stempu za sensa, stempu za uskauti, stempu za Azimio la Arusha, stempu za michezo ya Olimpiki, stempu za miaka kumi ya SADC, stempu za uwindaji wa asili, stempu za miaka 20 ya Mapinduzi ya Zanzibar, stempu za ujio wa Papa Paul John wa Pili na zingine nyingi.

“Kwa ujumla uchoraji wa stempu una umuhimu wake kwani stempu huhifadhi picha za matukio ya kihistoria, pia stempu huelimisha watu wa nje matukio mbalimbali yanayotokea hapa nchini,” anasema.

Kutokana na umuhimu huo, Ndembo anasema kuchora stempu kulihamasisha baadhi ya Watanzania kuanzisha chama cha ukusanyaji stempu ambacho yeye mwenyewe alikuwa katibu.

Lengo la kukusanya stempu za ndani na nje, lilikuwa kwa ajili ya kufanya maonyesho ya stempu na kutoa elimu inayohusiana na stempu kwa wanafunzi nchini.


Kabla ya kushughulika na sanaa ya uchoraji wa stempu alitumiwa sana na Umoja wa Vijana wa CCM kuchora picha katika matamasha mbalimbali, kazi hiyo ilimchukua hadi kwenye matamasha yaliyofanyika Libya, Urusi na Korea Kaskazini, ambako waliandaa maonyesho ya kazi za sanaa za Tanzania, ambayo yalizinduliwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Nyerere.

Mwaka 1987, picha alizozichora katika ukumbi uliofanyika mkutano mkuu wa CCM Kizota mjini Dodoma, zilimletea sifa ya hali ya juu na kuanzia hapo alizidi kupata kazi za uchoraji.

Swali: Unaridhika na maendeleo uliyofikia katika shughuli zako za uchoraji?
Jibu: Naridhika na maendeleo niliyofikia ila hata hivyo kazi yangu pia ina matatizo yake.

Moja ya matatizo hayo ni ukosefu wa vitendea kazi vya kutosha. Kwa mfano, nina kamera moja ya kisasa lakini haitoshi.
Nataka niwe na kamera zitakazoniwezesha kutembelea mbuga za wanyama ambako nitaweza kupiga picha za sura za wanyama kwa kadiri ya matakwa yangu na kuzichora
Swali: Unavutiwa na mchoraji gani kwa sasa hapa nchini au nje?

Jibu: Navutiwa sana na mchoraji wa nje aitwaje Leonardo Da Vichi. Huyu ni msanii wa zamani aliyechora picha ya Monalisa 1503-1506.
Huyu ndiye mchora ninayempenda mimi kwani kazi zake zinavutia sana na natamani kuwa kwenye kiwango chake.

Swali: Unawashauri nini wachoraji wenzako?
Jibu: Nawashauri wasiigane katika mitindo yao ya uchoraji kwa sababu si rahisi wao kupata utambulisho wa kazi zao.
Swali: Unaiambia nini serikali?

Jibu: Naiomba serikali ituwezeshe wachoraji ili sanaa yetu ya uchoraji iweze kukubalika ndani na nje ya nchi, kwani kwa kufanya hivyo wachoraji wataweza kujiongezea kipato.

Ndembo, alizaliwa katika Kijiji cha Mumbaka, Wilaya ya Masasi. Alisoma katika Shule ya Msingi Masasi kuanzia mwaka 1962-1965.

Baadaye alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Chidya wilayani Masasi. Alipata Diploma ya Ualimu, kisha alichukua shahada ya uchoraji katika Chuo cha Sanaa cha Margaret Trowell School of Art na mwaka 1966-1970, alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda.

Mwaka 1972-1975, aliajiriwa na Wizara ya Elimu katika Idara ya Utamaduni. Pia alifundisha katika Chuo cha Ualimu Chang’ombe.

Wapenzi wa picha zake wanaweza kuona kazi zake kupitia www.ndembo.blogspot.com

0716 774494

Chanzo:Gazeti la
Tanzania Daima la Jumatano Machi 24 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.