Header Ads

UTEUZI WA WABUNGE CUF NDIYO MWISHO WA SAFARI?

Happiness Katabazi

KWA zaidi ya miongo miwili sasa Tanzania imekuwa na siasa za vyama vingi.
Vyama hivi vimegawanyika katika chama tawala na kwa upande wa pili vyama vya ushindani.


Lengo la kuwa na vyama vingi ni kuwapa wananchi demokrasia pana ya kushiriki katika uongozi wa nchi yao. Kila chama kina sera zake, maono, itikadi na utamaduni wake wa kisiasa.

Kwa mfano kipo Chama NCCR-Mageuzi ambacho kinajitambulisha kuwa na itikadi ya demokrasia ya kijamii, sera zake katika maeneo mengi zinalenga kuleta mageuzi katika mifumo ya utawala, katiba, sheria na jinsi ya kutoa huduma ya ustawi wa jamii.

Viko vyama ambavyo vipo kambi ya ushindani ama vina sera za utajirisho ama mapesa. Vyama hivyo ni kama Chama cha Wananchi (CUF), Chama Cha Mapinduzi (CCM), United Democratic (UDP na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mchanganuo huu unatuonyesha kwamba ukiondoa zana ya chama tawala kwa upande mmoja na vyama vya ushindani kwa upande wa shilingi. Siasa za kweli za vyama ziko katika itikadi, sera na utamaduni wake kisiasa.

Ndiyo maana mijadala ya kitaifa kuhusu masuala nyeti ya kitaifa inabidi itazamwe katika muktadha huu wa sera, itikadi na utamaduni wa kisiasa.

Ni vyama gani vipo kwenye kundi moja, jukwaa moja na vinaweza kuendesha serikali pamoja? Maridhiano ya Zanzibar kati ya CCM na CUF yanaonyesha kuwa tofauti kuu kati ya vyama hivi haipo katika itikadi, sera, wala utamaduni wa kisiasa bali katika ubinafsi uliojengeka katika maudhui ya falsafa za kihafidhina za ubepari. Ambao wengine wanauita utajirisho au mapesa.

Hakuna jipya linaloweza kuletwa kimageuzi na CUF, UDP au CHADEMA ambalo haliwezi kuletwa na CCM kwani hawa ni ndugu moja. Hawa wanaweza kutawala pamoja. Wakigombana kwa uroho na ubinafsi uliojengeka ndani ya familia moja.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, chama cha ushindani kilichokataa kuweka saini makubaliano ya ushirikiano wa pamoja wa vyama vya ushindani kilikuwa ni CUF. Kilirejea kwenye kambi ya ushirikiano baada ya kushindwa.

Kila mara CUF inakubali ushirikiano na chama kingine, mfano wa CHADEMA, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, ilijihakikishia ushindi si wa pamoja bali wake binafsi.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, kila chama cha upinzani kiligombea kivyake kwa vile si CUF wala CHADEMA walikuwa tayari kushirikiana na chama kingine.

Walikuwa tayari kununua wagombea wa vyama vingine na kuwafanya wagombea wa vyama vyao.

Mfano, marehemu Chacha Wangwe kutoka NCCR-Mageuzi akiwa diwani na mgombea wa chama hicho, ghafla alikihama akiwa na nyadhifa hizo.

Ilidaiwa alinunuliwa na kwenda kugombea ubunge Tarime kupitia CHADEMA katika Jimbo la Tarime.

Lakini si huyo tu, hata aliyekuwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi wakati huo Mosena Nyambambe, alijitosa kugombea ubunge katika Jimbo la Serengeti kupitia CUF.

NCCR -Mageuzi haikulalamika wala kuwawekea pingamizi wagombea hao, japo ikumbukwe uchaguzi wa mwaka 2000, Naila Jiddawi, alipoondoka CUF na kujiunga na NCCR kisha kugombea urais wa Zanzibar aliwekewa pingamizi na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Uchaguzi Mkuu ujao, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, unatupa hisia kali kuhusu mustakabali wa siasa za mageuzi nchini.

Tayari vyama vinavyojiita vigogo wa upinzani vikirubuniwa na CCM. Sasa CUF ni CCM. Waliojifanya wana ‘ngangari’ sasa hawafui dafu kufukuza kuku mbele ya CCM.

Hatujui mambo yatakwenda vipi kwa vyama kama CHADEMA, UDP, kwani vyama hivyo vina wabunge kwenye Bunge la sasa, vilijiita wao ndio vigogo.

Kama siasa za maridhiano za kwenda kutembeleana, kula biriani na CCM zitatawala siasa za mageuzi, je, wananchi wategemee nini sasa kama mustakabali wa nchi yao?

Msemaji wa Ikulu, Salva Rweyemamu alishataadharisha kwamba utabiri wa Sheikh Yahya Hussein uheshimiwe. Hatujui matamshi ya Rweyemamu ndiyo msimamo rasmi wa rais wetu kuhusu jambo hilo au la.

Lakini kwa kuwa rais hajalikanusha hilo, tunapata sababu ya kuwa na mashaka kuwa rais wetu ni mshabiki au mfuasi wa utabiri wa mnajimu huyo.

Wapinzani kula matapishi yao: mjadala huu kuhusu mastakabali wa mageuzi hautanoga kama tusipojikumbusha yaliyowahi kusemwa kuhusu Serikali ya Awamu ya Nne.

Tunachokiona hapa katika matukio ya hivi karibuni, ni pamoja na maridhiano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar na kuteuliwa viongozi wawili wa CUF kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Rais Amani Abeid Karume.

Lakini pia Rais Kikwete naye alimteua Ismail Jussa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Haya yote yametosha kuziba midomo, kelele na kebehi nyingi kutoka CUF dhidi ya utawala wa Rais Kikwete.

Ghafla Kikwete na Rais Karume wamegeuka waungwana, wasikivu, malaika, viongozi bora, hawakumbatii mafisadi, si wezi wa kura.

Nadhani tatizo lilikuwa ni njaa ya wenzetu, wala wasitudanganye kitu, sasa tumeelewa wazi kwamba kelele tulizozisikia miaka nenda rudi, kejeli na majigambo vimezikwa.

Lakini CUF kukubali kupewa vyeo hivi dakika za majeruhi wakati taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu zitawapeleka pabaya.

Ikitokea hivyo, CUF isigeuke nyuma kuomba huruma ya wana mageuzi wengine kwani wamepiga jaramba huku wakijiona. Hongera CCM kwa ‘usanii’ na ufundi mkubwa kwa kufunga bao dakika za majeruhi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Machi 21 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.