Header Ads

WANAWAKE WAPO WAPI KWENYE SHERIA?

Happiness Katabazi

MACHI 8 kila mwaka huwa ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Kwa Tanzania maadhimisho hayo yalifanyika mkoani Tabora na Rais Jakaya Kikwete alikuwa mgeni rasmi.


Maadhimisho hayo yanazidi umaarufu na kujulikana kwa watu mbalimbali kwa sababu vyombo vya habari vimekuwa vikiyatangaza kwa muda mrefu sambamba na kufanya mahojiano na watu mbalimbali kuelezea umuhimu wa mwanamke katika jamii pamoja na changamoto zinazomkabili.

Lengo hasa la vyombo vya habari na wanaharakati ni kuhakikisha jamii inaachana na mfumo dume, ambao kwa muda mrefu umekuwa ukimuweka kando mwanamke katika nyanja za utawala na shughuli za kiuchumi.

Mfumo dume huu ndio ule unaomuona mwanamke kuwa ni pambo la nyumbani pamoja na mlezi wa familia, ambaye hata mumewe anapofariki dunia hapaswi kurithi mali alizochuma naye.

Sekta ya sheria nayo imeathirika na mfumo huo ambapo bado kuna idadi ndogo ya mawakili wanawake ndani ya serikali na wale wanaojitegemea kiasi cha kuwafanya hata waliopo wakose kujiamini katika utendaji wao.

Kutokujiamini huko kunawafanya mawakili wanawake wa serikali wasipangwe kuwa mawakili viongozi katika kuendesha kesi kadhaa za jinai ambazo zinavuta hisia za wananchi.

Kesi ambazo zimekuwa zikivuta hisia za wananchi wengi ni kesi za wizi wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara, kulawiti na mauaji, ambazo nyingi zimefunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama ya Wilaya ya Ilala na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Binafsi naamini mawakili wanawake hawana woga ila wengi wa washitakiwa au wadaiwa ni wanaume na pindi wafikiriapo kumtafuta wakili wa kuwatetea hujikuta wakifikia uamuzi wa kuwapa kazi mawakili wa kujitegemea wanaume ili wawatete mahakamani.

Wanaume wengi nao wamejenga dhana kwamba mawakili wanawake ni waoga, jambo linalowawia vigumu kuwapa kazi ya kuwawakilisha mahakamani.

Kwa mfano huo tunaona kwamba mfumo dume bado upo na unaendelea hadi kwa wananchi wanaohitaji huduma ya kisheria kutoka kwa mawakili wa kujitegemea, kwani wanaoshitakiwa wengi kila kukicha hapa nchini ni wanaume.

Pamoja na hilo, wanasheria wanawake nchini bado ni wachache ukilinganisha na wanaume.

Na inapotokea kesi zinazogusa hisia za wananchi unakuta Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi au Mwanasheria wa Kanda ya Dar es Salaam, Stanslaus Boniface au Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Ben Lincoln, wanawapanga mawakili wanaume kuongoza jopo la mawakili wa serikali na TAKUKURU kuendesha kesi hizo na mawakili wanawake kutoka taasisi hizo wanaishia kuwa wasaidizi wa mawakili hao wanaume.

Na hili si siri, kwani tunalishuhudia kila kukicha pale Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi za EPA na matumizi mabaya ya ofisi za umma tangu zilipoanza kufunguliwa Novemba 4, mwaka 2008 hadi leo, ni mawakili wa serikali wanaume ndio wanaongoza kuendesha kesi hizo na mawakili hao ni Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, Fredrick Manyanda, Oswald Tibabyekoma, Michael Lwena, Timon Vitalis, Ben Lincoln, Prosper Mwangamila, Justus Mulokozi na Biswalo Mganga.

Na mahakama huishia kuambiwa na mawakili hao wa serikali wanaume kabla ya kuanza kwa kesi hizo kwamba watasaidiwa na mawakili ambao wana jinsia ya kike, Tabu Mzee kutoka TAKUKURU na Arafa Msafiri, kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendesha kesi hizo.

Lakini wakati washitakiwa wa kesi hizo wanasomewa hati za mashitaka na maelezo ya awali (PH), tulishuhudia mawakili wanawake ndio walisoma hati hizo.

Kesi zinapofikia wakati wa mashahidi kuanza kutoa ushahidi, utaona mawakili wa serikali wanaume ndio wanaongoza jopo la mawakili wa serikali kuendesha kesi hizo.

Swali, je, kama mawakili wanawake wa serikali waliweza kuwasomea hati za mashitaka washitakiwa na kuwasomea maelezo ya awali (PH) ni kwanini inapofika wakati wa mashahidi kutoa ushahidi mawakili wanawake wa serikali hawapewi fursa na badala yake tunawaona mawakili wa serikali wanaume ndio wanawahoji mashahidi wa kesi hizo husika?

Ni kweli kwamba wanasheria wana kanuni moja isemayo katika kuendesha kesi mahakamani anapokuwepo Mwanasheria Kiongozi au Mwanasheria Mwandamizi, basi mwanasheria mchanga ambaye hajafikia ngazi hizo atabakia kuwa msaidizi katika uendeshaji wa kesi.

Si lengo langu kupingana na kanuni hiyo, ila kama mtindo huo utaendelea wa kesi zinazovuta hisia kwa jamii kuendelea kuongozwa na majopo ya mawakili wanaume wa serikali kwa kigezo kwamba wao ndio wana uzoefu na kazi hiyo si haki.

Je, hao mawakili wanawake kutoka TAKUKURU na wale wanaotoka Ofisi ya DPP ni lini watapata uzoefu wa kuongoza jopo la mawakili wa serikali katika kesi za aina hiyo ambazo zinavuta hisia katika jamii?

Ikumbukwe kuwa hapo kale hata kwenye ulingo wa siasa wanawake walionekana hawawezi na kwamba saizi yao ilikuwa ni kuwapigia kampeni wagombea wanaume tu. Lakini leo hii katika ulingo huo wanawake wamepewa nafasi za uongozi, wachache wao wameweza kuvunja dhana hiyo na kuthibitisha uwezo wao.

Kumekuwa na fikra za kimageuzi katika sekta ya elimu ambazo zinatambua wanawake wanahitaji mazingira tofauti na wavulana ili wanawake waweze kufanya vizuri. Hayo mabadiliko bado hayajawakomboa wanawake wengi kwani wanawake bado ni wachache sana.

Zamani ilionekana kazi ya uendesha mashitaka ni kazi ya wanaume lakini kutokana na mabadiliko ya kifikra,wanawake sasa wamekuwa wakifanya kazi hiyo ya uendeshaji mashitaka katika mahakama zetu.

Hili jambo ni la kulipa muda lakini hatua za makusudi zichukuliwe kuwajengea uwezo wanawake, kwa sababu hivi sasa wanawake ndio wanaanza kujitokeza kwa wingi kusomea fani ya sheria na wanapohitimu wanajikuta wanapata kazi sehemu zenye mvuto zaidi wa kifedha kuliko kushughulikia kesi za jinai mahakamani.

Ndiyo maana hatuwaoni kwa wingi mahakamani ila wanavyozidi kuhitimu wataonekana wengi mahakamani.

Kama wanawake wengi walivyoanza kujitokeza kusoma sheria, tunawahamasisha wale waliohitimu sheria wajiunge katika maeneo ambayo yamekuwa yakihodhiwa na mawakili wanaume kama vile uendeshaji mashitaka na uandikaji sheria. Hasa haya ndiyo maeneo nyeti mno.

Nitoe rai kwa DPP Feleshi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Hosea wawapokee wanasheria wanawake na wawape mafunzo na kipaumbele, tunaamini watafanya kazi vizuri.

Wanasheria wanawake waliopo kwenye taasisi zinazoongozwa na viongozi hao, tunaomba wapewe fursa sawa na wanaume ili mwisho wa siku serikali yetu iwe na mawakili wa serikali wanawake wengi mahiri, watakaoweza kuhakikisha wanakabana kisheria kikamilifu na mawakili wa kujitegemea.

Majura Magafu ni miongoni mwa mawikili wa kujitegemea ambao hivi sasa amejizolea sifa kemkemu nchini kutokana na umahiri wake wakati akiwa mahakamani, akiwatetea wateja wake (washitakiwa) na mwisho wa siku serikali inajikuta ikishindwa kesi nyingi za jinai, ambazo zilikuwa zikiwakabili washitakiwa waliokuwa wakitetewa na wakili huyo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili Machi 14 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.