Header Ads

UVCCM KUANDAMANA BODI YA MIKOPO IVUNJWE

• Kuwashirikisha wanafunzi wa sekondari

Na Happiness Katabazi

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umetishia kuitisha maandamano nchi nzima iwapo serikali haitoivunja bodi ya mikopo ya elimu ya juu na kuiunda upya.


Umesema kuwa bodi hiyo hivi sasa imekuwa ikiwanyanysa wanafunzi na kuwa chanzo cha migomo kwa wasomi wa vyuo vikuu hapa nchini.

Tishio hilo limetolewa jana jijini Dar es salaam na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Taifa, Beno Malisa muda mfupi baada ya kukubaliana na ombi la Shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu (CCM) mkoa wa Dar es Salaam lililotaka kufanyika kwa maandamano hayo .

Shirikisho hilo lilisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuona kila kukicha migomo ya wanafunzi imekuwa ikitokea na sababu kubwa ni watendaji wa bodi hiyo kutowajibika.
Malisa pamoja na Katibu Mkuu wa umoja huo, Martin Shigela waliishutumu vikali bodi ya mikopo kwamba imeshindwa kazi, na kuwataka viongozi wa bodi hiyo watumie busara zao kuziacha ofisi hizo kabla ya kufukuzwa.

Alibainisha kuwa bodi hiyo imekuwa ikiwanyanyasa wanafunzi na kuichonganisha serikali ya CCM na wasomi hapa nchini.

Alisema kama serikali haitokisikia kilio chao hicho watafanya maandamano ya nchi nzima wakiwashirikisha wanafunzi wa shule za sekondari kwa sababu wao ni wahanga watarajiwa wa bodi hiyo inayofanya ubaguzi na unyanyasaji wakati wa kutoa mikopo.

“Kimsingi tumekubaliana na tamko lenu lililoutaka uongozi wa UVCCM tukaiambie serikali iivunje bodi…sisi tumewaelewa na tunawaahidi kuanzia sasa UVCCM itaandaa maandamano makubwa nchini nzima kuishinikiza serikali iivunje bodi hiyo kwani imekuwa ikiropokaropoka hovyo na kuwanyanyasa wanafunzi.

“Serikali imekuwa ikiipatia fedha bodi ya mkopo kwa wakati, lakini kwa sababu inazozijua imekuwa ikiwacheleweshea wanafunzi hadi wamejikuta wakiishi maisha ya taabu na kuanza kuichukia serikali yao.

“Kila kukicha wanafunzi wamekuwa wakiilalamikia bodi na migomo haiishi…hivi bodi ni dudu gani hadi tuliruhusu liwanyanyase Watanzania wenzetu…tunasema hatukubali lazima tuandae maandamano ya kushinikiza bodi hii ivunjwe,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Salum Ally, alisema lengo la mkutano huo ni kutoa tamko la kuipongeza UVCCM la hivi karibuni lililotaka bodi ivunjwe na kuiomba UVCCM iandae maandamano nchi nzima kushinikiza bodi hiyo kuvunjwa na kwamba tamko hilo wamelitoa kwa niaba ya vyuo vikuu vyote nchini.

Ally alisema katika tamko hilo wameainisha matatizo yanayoikabili bodi hiyo likiwamo la kiutendaji kwamba bodi imekuwa na uwezo mdogo wa kuhakiki taarifa zinazotolewa na waombaji wa mikopo.

Pia alisema tatizo lingine ni la utunzaji mbovu wa kumbukumbu za waombaji, hali inayochangia usumbufu kwa wanafunzi.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Januari 31 mwaka 2011

No comments:

Powered by Blogger.