Header Ads

MWANZO,MWISHO WA KESI YA JERRY MURRO


Na Happiness Katabazi


NOVEMBA 20 mwaka 2011: Jerry Murro alifunga ndoa na Jeniffer John katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT) Usharika wa Azani Front jijini Dar es Salaam.



Oktoba 28 mwaka huu, upande wa Jamhuri uliwaowakilishwa mwanzo hadi mwisho wa kesi hii na Mkurugenzi Msaidizi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface uliwasilisha majumuisho yao kwa njia ya maandishi ambayo yaliomba mahahakama imuone Murro na wenzake wanahatia.


Boniface alidai hoja ya Wakili wa Murro, Richard Rweyongeza inayodai kuwa Murro hakutenda makosa hayo na kwamba anashangaa ni kwanini polisi walifanya haraka kumkamata Murro wakati alikuwa hajapokea kiasi hicho cha fedha,ni dhahifu kwasababu kabla ya Murro kukamatwa tayari Wage alishafika kituo cha polisi na kutoa taarifa kuwa mshtakiwa huyo amemwomba rushwa.

“Na kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 kinasema kitendo cha kuomba rushwa ni kosa chini ya kifungu hicho ….sasa namshangaa sana wakili Rweyongeza anavyo dai ni kwanini polisi wasingesubiri Murro apokee zile Sh milioni 10 za rushwa.
Tunaiomba mahakama iipuuze hoja hiyo ya wakili Rweyongeza kwasababu haina msingi kwani sheria hiyo ya kuzuia rushwa inatamka bayana mtu yoyote atayeomba rushwa, kupokea rushwa, kula njama ni makosa matatu yanayojitegemea na kitendo cha Murro kuomba rushwa tayari alikuwa ameishatenda kosa na ndiyo maana polisi walimkamata”alidai wakili Kiongozi wa Serikali Boniface.

Aidha Wakili Boniface aliomba mahakama hiyo iikate hoja wakili wa Murro iliyokuwa ikidai kuwa Murro alikamatwa katika Hoteli ya City Garden Februali mwaka jana wakati mshatiwa huyo hotelini hapo kwaajili ya kuudhulia mkutano nma waandishi wa habari, hoja ambayo wakili hiyo wa seriakali ni ya uongo kwani siku hiyo hapakuwepo na mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika hapo na ndiyo maana si Murro wala wakili wake Rweyongeza wameweza kuleta ushahahidi unaonyesha siku hiyo hotelini hapo ulifanyika mkutano na waandishi wa habari na pia wameshindwa kumleta mtu aliyekuwa ameuitisha mkutano huo ili aje kuidhibitishia mahakama kuwa alikuwa ameitisha mkutano siku hiyo na kwamba ni yeye ndiye alikuwa amempigia simu Murro ili aje hotelini hapo kuudhulia mkutano.

“Ni rai ya upande wa Jamhuri kuwa tumeweza kuithibitisha kesi yetu na tunaiomba mahakama imuone Murro na wenzake wana hatia katika kesi hii inayowakabili kwani ushahidi, vielelezo na utetezi waliotuoa mahakamani hapa umedhibitisha kuwa washtakiwa hao walitenda makosa yanayowakabili hivyo tunaiomba mahakama hii tukufu iwatie hatiani”alidai Wakili Boniface.
Oktoba 21 mwaka huu, upande wa utetezi unaowakilishwa na mawakili wa kujitegemea Rweyongeza, Majura Magafu nao waliwasilisha majumuisho yao kwanjia ya maandishi na kuiomba mahakama iwaachilie huru washtakiwa hao kwasababu hawana hatia kwani ushahidi ulioletwa na Jamhuri ni wa kuunga unga na hautoshelezi kuishawishi mahakama kuwatia hatiani.
Wakili Rweyongeza alidai kuwa alisikilizwa kwa makini ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa Jamhuri lakini hajasikia kitu chochote kinacho muunganisha Murro na washtakiwa wengine wasiojulikana kula njama kutenda kosa hilo kama shtaka la kwanza kwanza linavyodai kuwa Murro na washtakiwa wenzake ambao ni Deo Mugassa na Edmund Kapama na watu wengine wasiyofahamika walitenda kusa la kushawishi ili wapewe rushwa Sh milioni 10 toka kwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage Karoli , Januari 20 mwaka 2010 ili asiwe kurusha tuhuma zake za ubadhilifu wa fedha za umma katika kipindi cha Usiku wa Habari kinachorushwa na Televisheni ya TBC1.

“Shtaka la kwanza katika hati ya mashtaka, linasomeka kuwa kosa lilitendeka Januari 28 mwaka 2010.Lakini ushahidi ulitolewa na Jamhuri ulionyesha kosa lilitendekea Januari 29 mwaka 2010…na hadi mapema Oktoba mwaka huu washtakiwa walimaliza kujitetea na hivyo kesi upande wa utetezi ikawa imefungwa , hati ya mashtaka ilikuwa ikisomeka Murro alitenda kosa hilo Januari 28 mwaka 2010 ndipo upande wa Jamhuri siku hiyo kabla ya utetezi kufunga kesi yao ukaamua kubadilisha hati ya mashtaka na mahakama ilikubali hati hiyo kubadilishwa kutokana na utofauti uliopo kati ushahidi na maelezo yaliyokuwa yameandikwa kwenye hati ya mashtaka.

“Kwa hali hiyo naona upande Jamhuri hauna maelezo ya uhakika yanayoonyesha mteja wangu alitenda makosa hayo na badala yake ikaamua kuleta ushahidi wa kuungaunga na matokeo yake ndiyo maana Murro aliyakana mashtaka yote yanayomkabili mahakamani hapa”alidai Rweyongeza.

Alidai kuwa kesi ya Jamhuri imesimama na kutegemea ushahidi wa shahidi wa tatu (Michael Wage) jambo linawapotosha kwa sisi upande wa utetezi tunamuona Wage siyo shahidi wa kuaminika na wanaoimba mahakama iupuuze ushahidi wake.

Wakili Rweyongeza alidai kuwa katika ushahidi mashahidi wa Jamhuri walidai kuwa shahidi wa tatu(Wage) kwakuanzia aliwapatia washtakiwa wote rushwa ya Sh 9,000,000 katika sehemu ya rushwa ya Sh milioni 10 aliyokuwa ameombwa na washtakiwa, na wakili huyo akadai kuwa kama hivyo ndivyo ni kwanini polisi wasingesubiri Murro apokee rushwa hiyo ndiyo wakamkamate na kuongeza ni kwanini polisi ilifanya haraka kumkamata Murro wakati bado hajapokea rushwa hiyo ya Sh milioni?
Kuwasilishwa kwa majumuisho hayo ya pande hizo mbili kwa tarehe tofauti yalitokana na amri iliyotolewa na Hakimu Moshi, Oktoba 4 mwaka huu, ambapo siku hiyo alizitaka pande zote kufanya hivyo.
Na siku ndiyo shahidi wa Murro alitoa ushahidi wake na washtakiwa wawili Deogratius Mugassa na Edmund Kapama nao walitoa utetezi wao na siku hiyo hiyo wakili wa utetezi Richard Rweyongeza aliambia mahakama kuwa huo ndiyo mwisho wa ushahidi wao.
Na kabla ya washtakiwa hao kuanza kutoa utetezi wao wakili wa serikali , Boniface aliwasilisha ombi la kutaka kubadilisha hati ya mashtaka ambapo ombi hilo lilikubaliwa na hakimu huyo ambapo alisema kuanzia siku hiyo hati ya mashtaka itasomeka kuwa washtakiwa waliomba rushwa Michael Wage Januari 29 mwaka jana katika hoteli ya Sea Cliff, tarehe ambayo inaoona na picha za CCTV ambazo zinawaonyesha washtakiwa hao walifika katika hoteli hiyo wakiwa na Wage.
Kabla ya kubadilisha hati hiyo,hati ya mashtaka ilikuwa ikisomeka kuwa washatkiwa hao walitenda kosa hilo Januari 28 mwaka jana, tarehe ambayo ilikuwa ikitofautiana na tarehe iliyokuwa ikionekana kwenye nakala ya picha ya CCTV kamera.
Agosti 18 mwaka 2011; Murro alipanda kizimbani na kujitetea ambapo aliiomba mahakama imuone hana hatia kwasababu kesi inayomkabili amebambikiziwa na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi.
Mei 2 mwaka 2011, kesi hiyo ilipata hakimu mpya ambaye ni Hakimu Moshi baada ya hakimu mkazi wa awali Gabriel Mirumbe aliyekuwa akiisikiliza kesi hiyo kuamishiwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Machi 8 mwaka 2011, Hakimu Gabriel Mirumbe aliwaona washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.Uamuzi huo ulitolewa ikiwa ni dakika chache baada ya shahidi wa saba wa upande wa Jamhuri D/C Koplo Lugano Mwampeta kumaliza kutoa ushahidi wake siku hiyo na Wakili wa Serikali Kiongozi Boniface kuieleza mahakama kuwa huo ndiyo ulikuwa mwisho wa ushahidi wao na kwamba wanafunga kesi yao.
Inspekta Lugano Mwambeta akitoa ushahidi wake siku hiyo alieleza kuwa yeye alisaidiana na SSP-Duwani Nyanda kupekua gari la Murro na katika upekuzi wao walikuta miwani ya kusomea ya Wage na pingu moja iliyokuwa ikimilikiwa na Murro ambapo vitu vyote hivyo viwili vilipokelewa mahakamani hapo kama kelelezo namba sita na saba.


Januari 26 mwaka huu; Shahidi wa sita ambaye ni Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Ilala, (SSP) Duwani Nyanda alitoa ushahidi siku hiyo hiyo na akaieleza mahakama jinsi alivyoongoza zoezi la upekuzi katika gari la Murro ambapo alidai alikuta pingu na miwani ya kusomea ambayo ni mali ya Michael Wage.
SSP-Nyanda alieleza kuwa Januari 31 mwaka 2010 saa 12 jioni akiwa ofisini aliamriwa na aliyekuwa Mkuu wake, Charles Mkumbo, kwenda kulipekua gari la Murro lenye namba za usajili T 545 BEH Toyota Cresta lililoegeshwa kwenye viunga vya Kituo Kikuu cha Polisi Kati(Central) Dar es Salaam.
Nyanda alieleza kuwa katika upekuzi wake alifanikiwa kupata pingu ambazo Wage alizibaini kuwa ndizo alizotishiwa nazo na Murro na miwani ya kusomea ambayo anadai ni yake aliiisahau kwenye gari hilo Januari 30 mwaka jana na kuongeza kuwa alikuwa na hato ya polisi ambayo Murro na Wage walisaini kuthibitisha kushuhudia upekuzi huo na kuitoa mahakamani kama kielelezo namba tano ambacho kilipokelewa na Hakimu Mirumbe.
Januari 25 mwaka huu; Shahidi wa tano, Mkaguzi wa Polisi, Antony Mwita(45) ambaye alitoa ushahidi wake siku hiyo hiyo alieleza mahakama kuwa kitabu cha kumbukumbu ya kupokea wageni cha Hoteli ya Sea Cliff kinaonyesha kuwa Januari 29 mwaka jana, Murro alifika hotelini hapo siku hiyo.
“Na kitabu hicho kinaonyesha mgeni wa 25 alikuwa ni Jerry Murro na alifika hotelini hapo kwa kutumia gari lake lenye namba za usajili T545 THE aina ya Cresta na mlinzi huyo aliipatia kadi Na.673 na aliingia hotelini hapo saa 7:33 na kuondoka saa 8:48 mchana. ”alidai Mkaguzi Mwita.

Aliendelea kuieleza mahakama kuwa licha ya yeye kukusanya kielelezo hicho cha kitabu pia katika upelelezi wake katika kesi hiyo alienda duka la Mizinga lililopo Upanga jijini, kujiridhisha kama ni kweli Murro alinunua pingu katika duka hilo, na upelelezi wake ulibaini kwamba ni kweli duka hilo lilimuuzia pingu hiyo Mei 26 mwaka 2009 kwa Sh 25,000 na akapewa risiti yenye kumbukumbu na. 34357410. Kwamba mahakama ilipokea risiti ya pingu hiyo kama kielelezo cha nne.
Na siku hiyo hiyo ya Januari 25 mwaka 2011; shahidi wa nne ambaye ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Issa Seleman Chabu (37) alitoa ushahidi wake ambapo aliieleza mahakama jinsi yeye na makachero wenzake walivyoweka mtego na kufanikiwa kumkamata Murro Januari 31 mwaka 2010.
Mpelelezi huyo kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Ilala alieleza kuwa Januari 30 mwaka jana, saa nne asubuhi akiwa kwenye kazi za nje alipigiwa simu na Station Sajenti Gervas akimwarifu kuwa amepokea taarifa toka kwa Michael Wage kuwa kuna watu wamemtishia kwa silaha na kumwomba rushwa ya sh milioni 10 akanitaka nirudi ofisini.

Alidai kuwa siku hiyo Gervas alikuwa zamu ofisini kwake katika ofisi za RCO-Ilala na yeye akafika ofisini hapo saa nane mchana akamkuta Wage na Gervas wakampatia taarifa za malalamiko hayo kwa kirefu na kuongeza kuwa yeye alifikia uamuzi wa kuwasiliana na Mkuu wake wa kazi-RCO wa Ilala-Duwani Nyanda na kumueleza malalamiko hayo na kwamba mlalamikaji yupo ofisini kwao na kumuomba atupe utaratibu wa kulishughulikia tatizo hilo.
“RCO-Nyanda akanielekeza kwamba nifungue jalada la malalamiko na watuhumiwa wasakwe na wafikishwe kituoni.Na Wage alikuwa akilalamika kuwa kuna watu wawili wamejitambulisha kwake kuwa ni maofisa wawili wa (TAKUKURU )hakuwataja majina na mwingine akamtaja ni Jerry Murro ambaye ni mtangazaji ...na mimi nilitekeleza maagizo kwa kufungua jalada la uchunguzi;

“ Na nikamwelekeza afande Masika achukue maelezo ya Wage na nikamwomba Wage awapigie simu watu hao waliokuwa wakimtisha na kumwomba rushwa na akampigia mmoja wao ambaye alimtaja kuwa ni Murro na simu yake aliiweka kwenye Loud Speaker’ na Wage akamtaka Murro wakutane na Murro akamtaka Wage aje ofisini kwake TBC1 au Bamaga.”alidai Mkaguzi Msaidizi Chabu.

Chabu alidai hata hivyo yeye aliairisha zoezi hilo la Murro kutaka akutane na Wage ofisi za TBC1 na akamwomba RCO-Nyanda zoezi hilo la kuwamata lifanyike kesho yake ombi ambalo lilikubaliwa na mkuu wake wa kazi nakuongeza kuwa Januari 31 mwaka jana,saa nne asubuhi yeye na Wage walitoka katika ofisi za RCO-Ilala na kabla ya kutoka alimwomba Wage awapigie watu hao ili wajue wanakutana nao katika mgahawa wa City Garden.

“Wage akampigia Murro na kumweleza aje amkute katika mhagawa huo ili ampatie mzigo ambao ni sh milioni tisa na Murro akakubali na mimi nikawachukua askari wapelelezi watatu tukafanye mtego katika mgahawa huo na wapelelezi hao ni Station Sajenti Gervas, Sajenti Omary na Koplo Masawe na na tulipofika mimi nilikuwa kiongozi wao na Gervas na Masika niliweka nje ya mgahawa huo na mimi na Gervas tuliingia tuliingia na kukaa ndani ya mgahawa huo saa tano asubuhi;

“Nilipoona Murro atokeo nikamwambia Wage ampigie tena kumwarifu kwamba ameishafika na Wage akampigia huku simu yake ikiwa kwenye Loud Speaker wote tunasikia, Murro akamjibu Wage kuwa anakuja baada ya dakika tano na ndani ya muda huo Murro akafika nje ya mgahawa huo akampigia simu Wage akimtaka atoke nje ya mgahawa ili amkabidhi mzigo huo;

“Wage kabla hajatoka nje nikamkataza asitoke kwanza asubili sisi wapelelezi wawili tuko nje tukawaongezee nguvu wapelelezi wetu wawili tuliowacha nje kwaajili ya mtego, na tulivyotoka na nikamwona Murro akiwa nje ya gari lake amesimama na mimi na wale wapelelezi wenzangu tukapeana ishara zetu za Kiintelijensia na Wage ndiyo akatoka ndani ya mgahawa huo kuja nje na akakutana na Murro ambaye alikuwa akimuita kwa mkono Wage ambaye alikuwa amebeba mkoba ambapo alifungua mlango mwingine wa gari la Murro na kuingia ndani ya gari hilo.

Inspekta Chabu aliendelea kueleza kuwa baada ya Wage kuingia ndani ya gari la mshatakiwa huyo alifunga mlango haraka na kutaka kuondoka nikamweleza dereva wetu ambaye alikuwa akiendesha gari lenye namba za kiraia akaenda kulizuia gari la Murro ili lisiondoke na ndipo Murro aliposhtuka akamtaka Wage atelemke kwenye gari lake na yakazuka malumbano baina yao wawili na kutokana na hali hiyo yeye alisogea kwenye gari la mshtakiwa huyo na kumuuliza Murro kama alikuwa akimfahamu Wage, mshtakiwa huyo alikana kutomfahamu Wage.

Aidha aliieleza kuwa alimuuliza pia Wage kama alikuwa akimfahamu Murro na Wage alikiri kumfahamu mshtakiwa huyo na kusema kuwa ndiye miongoni mwa aliyemtishia kwa pisto na pingu na kumuomba rushwa y ash milioni 10 na kuongeza kuwa baada ya hapo alijitambulisha kwa Murro kuwa yeye ni ofisa wa polisi na kumweleza kuwa anakabiliwa tuhuma zinazomkabili la na kumtaka afungue gari lake ili yeye na wapelelezi wengine wapande gari lake na aliendeshe kuelekea kituo Kikuu cha Polisi Kati kwa mahojiano zaidi.

“Baada ya kumpa maelezo hayo kwanza Murro alinyamaza akasema haiwezekani kwani katika mgahawa huo yeye alifuatilia habari ya Mchina...nikapanda kiti cha mbele katika gari lake na kumtaka aendeshe gari hadi Kituo cha Kati na alitii amri hiyo na tulipofika nilimwambia afunge gari lake vizuri na anifuatwe kwenye ofisi za RCO-Ilala , tulipofika ofisini nikamuhoji kuhusu tuhuma hizo na alikana na baada ya hapo nikatoa taarifa kwa wakubwa wangu wa kazi kwamba tayari nimeishamata. Shahidi wa sita anaendelea leo kutoa ushahidi wake.
Januari 24 mwaka 2011;shahidi wa tatu ambaye alikuwa ni Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ,Michael Wage alikiri kutoa rushwa ya shilingi milioni moja baada ya kutishiwa kwa pingu na bastola.
Alidai kuwa alilazimika kutoa rushwa hiyo kwa sababu alitishwa na Murro na mshtakiwa wa pili Kapama aliyejitambulisha kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Takukuru na mshtakiwa wa tatu Deogratius Mugassa alijitambulisha kuwa ni msaidizi wa mkurugenzi huyo.

Shahidi huyo ambaye alikuwa mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kabla ya hajasimamishwa kazi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Januari mwaka jana, alidai kuwa washtakiwa hao wote watatu Januari 31 mwaka jana, katika Hoteli ya Sea Cliff walimtaka awapatie sh milioni 10 ama sivyo wangembambikia kesi kama alivyobambikiwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, kwa kumwambukiza maradhi mpenzi wa rafiki wa Kapama ndiyo maana akabambikiziwa kesi iliyomfanya ahukumiwe kwenda jela miaka miwili.

Wage aliieleza Mahakama kuwa Januari 28 mwaka jana akiwa nyumbani kwake Bagamoyo alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa mtangazaji wa TBC1 na hakuwa hakimfahamu, akimtaka kesho yake aje Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kwani amepata taarifa kuwa anakabiliwa na tuhuma za ufisadi katika Halmashauri ya Bagamoyo.

Katika hilo Wage alieleza kuwa alikubaliana na ombi hilo na Januari 29 mwaka jana, saa tano asubuhi alifikia katika mgahawa wa Califonia ulioko jijini hapa akiwa na dereva wake.

Alieleza kuwa akiwa njiani alimpigia simu Murro ili aje aungane naye na baada ya dakika chache Murro aliwasili katika mgahawa huo akiwa na gari ndogo na akamweleza watafute meza nyingine ili wakae mbali na dereva wake na walipohamia kwenye meza nyingine ndipo Murro alipoanza kumueleza tuhuma za ufisadi zinazomkabili na kwamba anataka kuzitangaza kwenye kipindi cha Usiku wa Habari kinachorushwa na TBC1.
“Baada ya Murro kunieleza tuhuma hizo akaniambia mahojiano kamili yangefanyika katika Hoteli ya Sea Cliff kwani huko ndiko walikokuwa mabosi wake na kunitaka nimwache dereva wangu kwenye mgahawa huo nikapande gari lake twende nae Sea Cliff na nilifanya kama alivyonielekeza nikapanda na tulipokuwa njiani akampigia simu mtu akawa anazungumza naye na akanitaja jina langu… alivyokata simu nikamuuliza ni kwa nini alikuwa akitaja jina langu akasema alikuwa akizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa PCCB (Kapama) naye pia atanihoji.

Wage aliendelea kueleza kuwa walipofika tu Hoteli ya Sea Cliff walipokelewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa PCCB, anaitwa Mussa ambapo hata hivyo Wage alimtambua mtu huyo mahakamani kuwa ni Mugassa na akaongeza mtu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Dokta ambaye Wage jana alimtambua mahakamani kuwa ni Kapama na kuongeza kuwa baada ya hapo mahojiano yakaanza na Dokta akaanza kumueleza kuwa yeye ni fisadi mkubwa na kwamba kama alihitaji msaada wao angesema mapema ili mahojiano yao yasiweze kurushwa kwenye kipindi cha Usiku wa Habari cha TBC1.
Alisema mara baada ya kutoa taarifa hizo polisi wakamtaka ampigie simu Murro na amweleze kuwa tayari ameishafika kwenye mgahawa wa City Garden.

Wage alieleza kuwa alifanya hivyo na baada ya dakika chache Murro aliwasili kwenye mgahawa huo lakini alivyomuona Wage ameambatana na watu wengine watatu alishtuka na polisi waliwahi kuzuia gari lake lisitoke katika viwanja vya mgahawa huo na askari kanzu hao walimwamuru aendeshe gari lake na kulipeleka kituo cha polisi Kati na Murro alitii amri hiyo na wote walifika kituoni hapo.

Alisema Murro alipoulizwa kama alikuwa akimfahamu Wage alikana kumfahamu na polisi hao walipopekuwa gari la Murro walikuta bastola, pingu na miwani ya kusomea ambayo Wage alidai ni yake na aliisahau jana yake wakati alipopanda katika gari hilo wakati anapelekwa Sea Cliff.
Vitu hivyo vyote pingu, bastola na miwani ilipokelewa mahakamani hapo kama utambulisho.

Kwa upande wake wakili wa Murro, Richard Rweyongeza, na Majura Magafu, anayemtetea Kapama na Muggasa akimhoji shahidi huyo alidai kuwa shahidi huyo haoni kwamba Murro alikuwa akitangaza habari za hatari hatari za kuligusa jeshi la polisi na alikuwa akitaka kurusha tuhuma za ufisadi zinazomkabili Wage ndiyo maana alishirikiana na polisi kumbambikizia kesi mteja wake, hoja hiyo ilipingwa vikali na shahidi huyo.

Novemba 12 mwaka 2010; shahidi wa pili Kumar Aluru Pournama alitoa nakala za picha za CCTV kamera katika mtandao wa Hoteli ya Sea Cliff kama vielelezo vya ushahidi katika kesi hii zinazowaonyesha washtakiwa hao watatu pamoja na Wage ambaye wanadaiwa kumuomba rushwa,wakiwa katika eneo hilo la Hoteli ya Sea Cliff na nakala hizo za picha za CCTV zilipokelewa na mahakama kama kielelezo.

Agosti 18 mwaka 2010; shahidi wa kwanza Staff Sajenti Peter Jumamosi alidai kuwa yeye ndiye alimchukua maelezo ya onyo mshtakiwa wa tatu(Muggasa) na akaomba mahakama iyapokee maelezo hayo ya onyo kama kielelezo.
Lakini hata hivyo wakili wa mshtakiwa huyo, Majura Magafu alidai mteja wake (Mugassa) anaiomba mahakama isipokee maelezo hayo kama kielezo kwasababu Februali 3 mwaka huo ,wakati anachukuliwa maelezo hayo na mshtakiwa wa kwanza Staff Sajenti Peter Jumamosi, aliteswa na alikuwa akishinikizwa na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam(ZDCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi, Charles Mkumbo na Kamishna Kasala ambao walimtaka mshtakiwa huyo atoe maelezo yatakayomgandamiza mshtakiwa wa kwanza (Murro) ambaye jeshi la polisi limekuwa likimsaka kwa muda mrefu kwasababu amekuwa akilidhalililisha jeshi hilo kwenye vyombo vya habari..
Hali iliyosababisha Hakimu Mirumbe kutoa amri ya kusimamishwa usikilizwaji wa kesi ya msingi na akaamuru kufanyika kwa kesi ndogo (trial within a trial) ambapo ilifanyika na kila pande zikaleta mashahidi wake lakini mwisho wa siku mahakama hiyo ilitupilia mbali ombi la wakili Magafu na ikapokea maelezo hayo kama kielelezo.
Agosti 12 mwaka 2010; mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Deogratius Mugassa kwa mara nyingine alifikishwa mahakamani hapo kwa kesi nyingine mpya ya kujifanya ni Ofisa wa Jeshi la Polisi na kisha kujipatia shilingi milioni 19 kwa njia ya udanganyifu.,
Mbele ya Hakimu Mkazi Devota Kisoka, Wakili wa serikali Zuberi Mkakatu alidai kuwa Mugassa anakabiliwa na mashtaka matatu.Shitaka la kwanza ni la kula njama na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwamba mshtakiwa huyo na wenzake ambao hawapo mahakamani.

Wakili Mkakatu alidai shtaka la pili ni la Mugassa kujifanya Ofisa wa Jeshi la Polisi kwamba Aprili 28 mwaka huu, katika Bar ya Rose Garden huko Mikocheni, yeye na wenzake walijitambulisha kwa Rose Azizi kuwa wao ni maofisa wa jeshi la polisi.

Mkakatu alidai shitaka la tatu ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwamba kati ya Mei na Aprili mwaka huu, katika Bar hiyo ya Rose Garden walijipatia sh milioni 19 kutoka kwa Rose Azizi baada ya kujifanya wao ni maofisa wa jeshi hilo na kwamba fedha hizo walizopewa watazitumia kuweka mtego wa kuwakamata wezi walioiba matofari mawili wa madini ya dhahabu wilayani Nzega.Katika kesi hii pia alipata dhamana.
Februali 5 mwaka 2010, ndiyo siku ya kwanza washtaki
wa hao kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Gabrile Mirumbe ambapo wakili Kiongozi wa Seriakali, Stanslaus Boniface alidai Murro anakabiliwa na makosa mawili ya kula njama na kuomba rushwa ya shilingi 10 toka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamayo,Michael Karoli Wage.

Wakati Mugassa na Kapama wanakabiliwa mashtaka hayo kama yanayomkabili Murro na shtaka jingine la tatu ambalo ni la kujifanya wao ni maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), jambo ambalo si la kweli.Na kwa kipindi chote hicho washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

0716- 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 30 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.