Header Ads

MAKALA YAMFIKISHA KORTINI KADA WA CHADEMA

Na Happiness Katabazi


MWANDISHI wa Safu ya ‘Kalamu ya Mwigamba (36)’ inayochapishwa kila siku ya Jumatano na gazeti la Tanzania Daima , Samson Mwigamba (36), jana alijikuta akifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwa kosa la kuandika makala inayowashawishi maaskari na maofisa wa majeshi ya hapa nchini kuacha kuitii serikali iliyopo madarakani kwa sasa.


Mwigamba ni Mhasibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Makao Makuu na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha na si mwandishi wa habari kitaaluma, alifikishwa hapo jana saa tatu asubuhi chini ya ulinzi mkali wa makachero wa Jeshi la polisi na kisha kuifadhiwa katika mahabusu ya mahakama hiyo wakati akisubiri kupandishwa kizimbani na kusomewa shtaka moja la kesi ya jinai Namba 289 ya mwaka huu.

Ilipofika saa 6:21 mchana Mwigamba ambaye si Mwandishi wa Habari Kitaaluma aliondolewa katika mahabusu ya mahakama huyo huku akisindikishwa na askari polisi na kisha kuuingizwa ndani ya chumba cha mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema na kisha Wakili Mwandamizi wa Serikali Elizabeth Kaganda alianza kumsomea shtaka linalomkabili.

Kaganda alidai mshtakiwa huyo anakabiliwa na kosa moja la kuwashawishi askari na maofisa wa jeshi la polisi, magereza na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) kutoendelea kuitii serikali iliyopo madarakani kwa sasa ambayo inaongozwa na Rais Jakaya Kikwete kinyume na kifungu cha 46(b),55(10(a) na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Wakili Kaganda alidai Novemba 30 mwaka huu,gazeti la Tanzania Daima la siku hiyo toleo Na.2553 lilichapisha waraka uliokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Waraka Maalum kwa Askari wote” ambao uliandikwa na mshtakiwa huyo kupitia safu yake ijulikanayo kwa jina la ‘Kalamu ya Mwigamba’.

Wakili huyo wa serikali alidai kuwa mshtakiwa huyo kupitia walaka wake huo kwa makusudi na kwa nia kuvunja sheria za mamlaka ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliwashawishi askari na maofisa wa jeshi la polisi, Magereza na JWTZ kutoendelea kuiiti serikali iliyopo madarakani.

Hata hivyo mshtakiwa huyo ambaye alikuwa amevalia magwanda ya chama hicho alikana kosa hilo na wakili Kaganda alidai upande wa jamhuri hauna pingamizi la mshtakiwa kupewa dhamana kwasababu kosa linalomkabili lina dhamana kwa mujibu wa sheria nakuongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Kwa upande wake Hakimu Waliarwande Lema alisema ili mshtakiwa apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambao kila mmoja atatakiwa asaini bondi ya shilingi milioni tano na mdhamini mmoja kati ya hao wadhamini wawili atapaswa awasilishe hati ya mali isiyoamishika yenye thamani ya shilingi milioni tano.

Hakimu Lema alisema sharti jingine ni kwamba mshtakiwa huyo atatakiwa kila mwisho wa mwezi aende kuripoti katika kituo Kikuu cha Polisi Kati(central) na mshtakiwa huyo atatakiwa asalimishe hati yake ya kusafiria mahakamani hapo.

Aidha wakili wa mshtakiwa Edson Mbogoro alieleza kuwa mshtakiwa ana wadhamini wawili ambao ni madiwani wa wilaya ya Ilala ambao wamekuja na barua zinazowatambulisha kuwa wao ni madiwani na kwamba hati hiyo ya mali isiyoamishika hawakuja nayo ila akaiomba mahakama impatie dhamana mteja wake.

“Ni hivi hapa hakuna kuombana omba masharti ya dhamana ndiyo hayo hapo juu nimeishayataja kwahiyo ninachotaka masharti hayo yatekelezwe kwa vitendo na siyo kuniomba sijui nini….kwanza nina kazi nyingi za kufanya siyo kesi hii moja…kwasababu mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana naamuru amepelekwe gerezani hadi Desemba 20 mwaka huu, kesi hii itakapokuja kwaajili ya kutajwa”alisema kwa ukali Hakimu Lema na kufanya Mwigamba kunyong’onyea.

Baada ya hakimu huyo kusema hayo askari hao walimtoa kizimbani Mwigamba na kisha kumrudisha katika mahabusu ya mahakamani hapo tayari kwaajili ya kusubiri gari la kumpeleka gerezani.Gazeti hili lilimshuhudia mmoja wa ndugu wa mshtakiwa huyo akitoka ndani ya viwanja hivyo akienda kwenye maduka ya jirani na mahakama hiyo na kumnunulia maboksi ya juice mbili na kisha kumpelekea mstakiwa katika mahabusu hayo kabla ya kupakizwa kwenye gari na kupelekwa gerezani.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kumfungulia kesi ya kushawishi au uchochezi mchangiaji wa makala kweny magazeti ya hapa nchini. Pia hii itakuwa ni mara ya pili kwa serikali kumfungulia kesi ya jinai Mwigamba tangu mwaka huu ulipoanza.

Kwani Mwigamba na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dk.Wilbroad Slaa , mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema na Mbunge wa Moshi Mjini Philemon Ndesamburo na wanachama wengine wanakabiliwa na kesi ya mkusanyiko na maandamano haramu waliyoyafanya Januari 5 mwaka huu, katika jiji la Arusha na kesi hiyo ipo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na imefikia hatua ya kuanza kusikilizwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Desemba 9 mwaka 2011.

1 comment:

Anonymous said...

Unajaitahidi.....but mtu asiijua hiyo story hawezipata background ya story in dtail...weaknss

Powered by Blogger.