Header Ads

MAHAKAMA IBADILIKE,IENDE NA WAKATIMahakama ibadilike,iende na wakati
Na Happiness Katabazi

KESHO Februali 3 mwaka huu, Mahakama ya Tanzania,inasherehekea siku ya Mahakama(Law Day). Sherehe hii ufanyika mara moja kwa mwaka na ufanyika tarehe za mwanzoni za mwezi Februali.

Kufanyika kwa sherehe hiyo ni ishara ya ufunguzi rasmi wa shughuli za mahakama kwa mwaka huu wa 2012. Itakumbukwa kuwa mahakama yetu imejiwekea utaratibu wa mwezi Desemba-Januari , Majaji na mahakimu uenda likizo kwaajili ya mapumziko na kisha kurejea maofisini rasmi mwanzoni Februali, baada ya sherehe hiyo kufanyika.

Mwaka huu sherehe hiyo ambayo itafanyika kesho na Rais Jakaya Kikwete atakuwa mgeni rasmi na mwenyeji wake atakuwa Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman katika maazimisho hayo yatakayofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam.

Kauli mbiu ya sherehe hiyo kwa mwaka huu inasema “Adhabu mbadala katika kesi za jinai:Faida zake katika Jamii”
Ni wazi kauli mbiu hiyo kwa wale wadau wa mahakama na utawala wa sheria itakuwa ni changamoto kwao.

Hakuna ubishi kuwa mhimili wa mahakama hapa nchini hivi sasa umeweza kupiga hatua za kimaendeleo kwa kadri ilivyoweza na unakuza utawala wa sheria kila kukicha kutokana na kutoa maamuzi mbalimbali ambayo mengine yamekuwa yakiripotiwa katika vyombo vya habari.

Baadhi ya hatua za maendeleo yaliyopigwa ni ukarabati na ujenzi wa baadhi ya mahakama, baadhi ya mahakama kufungwa teknolojia ya ya kisasa ya kurekodi mwenendo wa kesi,watumishi wengi kujiendeleza kielimu, kutoa hukumu mbali zilizohusisha kesi zilizokuwa zikiwahusu watu wenye majina makubwa kwenye jamii na kisha wengine mahakama ikawatia hatiani na wengine kuachiliwa huru.

Hatua nyingine ni ile iliyochukuliwa chini ya uongozi wa Jaji Mkuu Mstaafu Agustino Ramadhani enzi za uongozi wake kuweka kanuni amewafanya majaji wote wa mahakama kuu kuwa ni majaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi. Kwani kwa mujibu wa Jaji Ramadhani nakumbuka mwaka juzi nilivyofanya mahojiano naye alisema alifikia uamuzi huo baada ya kuona mahakama kuu kitengo cha Ardhi kina majaji wachache wakati mashauri ya ardhi katika mahakama hiyo ni mengi hali inayosababisha kesi kuchelewa kumalizika kwa wakati.
Na hata Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi Lameck Mlacha katika mkutano wake na waandishi wa habari ofisini wake mapema mwaka jana, alisema hivi sasa mlundikana wa mashauri ya migogoro ya ardhi katika mahakama hiyo unapungua kwa kasi ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Katika hili mahakama inastahili pongezi kwani migogoro ya ardhi imekuwa ikiibuka kila kukicha mahakamani, katika mabaraza ya Kata, Wizarani.

Tukiachana na hilo baadhi ya hatua hizo za maendeleo zilizopigwa, lakini bado mhimili huo wa mahakama ambao umepewa jukumu la kutoa haki katika Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ni kama zifuatazo.

Uhaba wa vyumba vya kuendeshea kesi, bado idadi ya mahakimu ni ndogo ukilinganisha na mahitaji ya kila siku,baadhi ya mahakama huko mikoani ngazi ya wilaya na mahakama za Mwanzo zipo katika mazingira mabovu ambayo yanaitaji kufanyiwa marekebisho ili hata watendaji wa mahakama waweze kujisikia wanafanyakazi kwenye ofisi zenye hadhi ya kuwa ofisi ya mahakama.
Nikiwa mwandishi wa siku nyingi wa habari za mahakamani hapa hususani zile za mahakama za mkoa wa Dar es Salaam, nimeshuhudia mahakama za mji huu ambao karibu mahakama zote zenye hadhi ya wilaya, Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama Kuu na Rufaa,waandishi wa habari uweka kambi kwa siku zote za juma kwaajili kuripoti kesi mbalimbali zinafunguliwa na kuendelea katika mahakama hizo.
Hakuna ubishi hivi sasa mhimili wa mahakama hivi sasa kupitia majaji na mahakimu wanatambua kazi ya waandishi wa habari ndiyo maana uwaruhusu waandishi wa habari kuingia ndani ya vyumba vya mahakama kusikiliza kesi wanazoziendesha kwa kuwapatia nafasi za viti, kuwapatia ushirikiano wa kuwafafanulia baadhi ya maneno ya kisheria ambayo wamekuwa hawayaelewi,kuwapatia majalada ya kesi kuyasoma na katika kesi ambazo zimekuwa zikufuatiliwa na umma Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Elvin Mugeta na Msajili wa Mahakama ya Rufaa Francis Mutungi siku moja kabla uwa wanatoa maelekezo kwa watendaji wao chini wa kuwatengea sehemu maalum ambapo mabechi kwaajili ya waandishi wa habari kuja kuketi ili waweze kuripoti kesi hiyo.

Na mfano hai wa viongozi hao wa mahakama kutoa ushirikiano wa aina hiyo kwa waandishi wa habari za mahakama ni siku mwaka juzi siku ile jopo la majaji saba wa mahakama ya Rufaa lilokuwa likiongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Agustino Ramadhani, kesi ya mauji iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Dar es Salaam, (ACP),Abdallah Zombe na wenzake, kesi ya kulawiti iliyokuwa ikimkabili mwanamuzi nguli wa Dansi, Nguza Vicking na mwanae Papii Kocha , kesi ya kula njama na kuomba rushwa ya shilingi milioni 10 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirikila la Utangazaji la TBC1,Jerry Murro.
Binafsi nilishiriki kuwasilisha mara kadhaa maombi ya kuomba mahakama iwawekee nafasi waandishi wa habari za mahakama kwa Hakimu Mugeta na Mutungi kwa njia simu na kweli viongozi hao waliweza kutekeleza ombi hilo kwa vitendo.

Tunashukuru sana na hiyo ni ishara kwamba hivi sasa mahakama inatambua mchango wa waandishi wa habari katika utendaji wa kazi wa mhimili huo ambao kwanjia moja au nyingine vinashirikiana na vyombo vya habari na wadau wengine kukuza utawala wa sheria na kuubarisha umma maamuzi yanayotolewa na mhimili wa mahakama.

Hivyo wakati mahakama kesho ikianza mwaka mpya wa Mahakama,sisi waandishi wa habari za mahakama tunamuomba Jaji Mkuu Mohamed Chande na timu yake iweke mashine (Photocopy mashine)ya kutolea nakala katika mahakama zake ambazo tutakuwa tukilipia ili wadau wa mahakama waondokane na usumbufu wa kwenda umbali mrefu kusaka huduma hiyo, pia sisi waandishi wa habari tunaomba tutengewe angalau chumba kimoja pale Mahakama ya Kusitu na Mahakama Kuu ambacho kitakuwa na kompyuta kwaajili ya kuweza kuwasaidia kuandika habari za mahakama na kuzituma maofisini kwao mapema, wakati wakisubiria kuingia mahakamani kuudhulia mashauri mengine yanayoendeshwa mchana na kumalizika wakati mwingine jioni.Naamini hayo yakifanyika na mengine zaidi yakiboreshwa mahakama yetu itakuwa inazidi kwenda na wakati.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 2 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.